Archive for July, 2009

Soko kuu la Matunda Zanzibar

MANENO YA HEKIMA

Maneno ya Hekima

Mwenyezi Mungu asipoombwa hughadhibika

Mwanadamu anapoombwa hukasirika

Wacha kumuomba mwenye kusikitika

Umuombe yule ambaye milango Yake iwazi wala haitofungika

Ali bin Abu Talib (RA)

Amali bora kupita zote ni Sala kwa wakati wake

Hadithi ya Mtume (SAW)

“Nilipotambua kuwa amali zangu hawezi kunifanyia mwengine, nikapania kuzifanya mwenyewe.

Na nilipotambua kuwa riziki yangu hawezi kuichukuwa mwengine, moyo wangu ukapata utulivu.

Na nilipotambua kuwa Mola wangu ananiona, nikaona haya asinione nikimuasi”.

Al Hassan al Basry

NAMNA YA KUHUKUMU BAINA YA WATU
Omar (RA) alimuandikia Abi Musa Al Ash ary (RA) yafutayo akimfundisha hekima za kuhukumu baina ya watu kwa uadilifu;

“Kutoka kwa Mja wa Mwenyezi Mungu Amiri wa Waislamu kwa Abdullahi bin Qays; kwa hakika kuhukumu baina ya watu ni fardhi iliyo wazi na mwenendo unaowajibika kufuatwa. Fahamu pale unapotolewa ushahidi na uamue unapokubainikia ukweli, kwani haki bila ya kuamuliwa haina faida. Wapoze watu katika majlis yako, ….Mwenye kudai anawajibika kutoa ushahidi, na mwenye kukanusha wajibu wake kula kiapo.

Suluhu ni bora baina ya Waislamu, lakini isiwe suluhu inayohalalisha haramu na kuharamisha halali.

Usije ukakuzuwia uamuzi ulouamuwa jana, kisha Mwenyezi Mungu akakuongoza ukatambua kuwa ulikosea katika uamuzi ule, ukakufanya uogope kuiweka sawa haki, kwani haki ni haki na haibatilishwi na chochote. Na kuirudisha haki kwa wenyewe ni bora kwako kuliko kuendelea kuinyamazia batili.

Ushahidi wa Waislamu baina yao ni haki, isipokuwa yule aliyewahi kuhukumiwa kupigwa mjeledi kwa kosa kubwa au aliyewahi kutoa ushahidi wa uwongo au anayetiliwa shaka kwa sababu ya kumpendelea mshitaki au mshitakiwa kwa ajili ya undugu wa nasaba, (hawa ushahidi wao haukubaliwi), na Mwenyezi Mungu ndiye ajuwae siri za moyoni.

Usiwatishe watu au kuingiza uwoga nyoyoni mwao, kwani yule anayeihusisha nia kwa ajili ya kumridhisha Mwenyezi Mungu basi Mwenyezi Mungu anamtosheleza. Ama mwenye kuamua kinyume na haki kwa ajili ya kutaka kujipendekeza kwa watu, MwenyeziMungu humuacha alivyo, na iko siku atamfedhehesha. Unaonaje mtu akizikimbilia thawabu za Mola wake na Rehema Zake?

Wassalaam”.

Omar bin Khattab (RA)

Luqman mwenye Hekima

Siku moja mfalme wa Luqman mwenye hekima “Luqman al Hakiym” alichinja mbuzi wawili na kumtaka Luqman achaguwe kutoka katika mbuzi wawili hao vipande viwili vibaya kupita vyote na viwili vingine vizuri kupita vyote

Luqman akachagua moyo na ulimi kutoka katika kila mbuzi. (yaani alitoa kutoka katika mbuzi wa kwanza moyo na ulimi, na kutoka katika mbuzi wa pili akatoa pia moyo na ulimi).

Mfamle akamuuliza;

“Nilikwambia uchague kutoka KILA mbuzi sehemu mbili, mbona umechagua mbili hizi tu (Moyo na ulimi)?”

Akajibu;

“Hakuna vibaya kuliko hivi vikiharibika na hakuna vizuri kuliko hivi ikitengenea”.

FUNGUO ZA KHERI
Kheri yote inapatikana pale Mwenyezi Mungu anaporidhika na mja wake, na funguo za kheri zimo katika Dua pamoja na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu na kuonesha kumpenda kwa kutenda yale yanayomridhisha na pia kumuogopa kwa kuepukana na makatazo yake.

Mja anapokabidhiwa na Mola wake funguo hizi basi ajue kuwa Mola wake anamtakia kheri, na anaponyimwa basi ajue kuwa amefungiwa milango ya kheri.”

Omar bin Khatab(RA) anasema;

“Mimi sijishughulishi na majibu ya dua yangu, bali najishughulisha na kuomba Dua, wakati wowote Mola wangu anaponikabidhi funguo za dua, basi huwa na uhakika kuwa majibu yake yatakuja tu”

Makosa ndani ya Swala

Makosa ndani ya Swala

Imekusanywa na Muhammad Faraj Al Saiy
Utulivu.. 1
Kudokoa.. 1
Kuichelewesha
Isha na Alfajiri

Kuikimbilia

Kumsubiri Imamu.. 3
Kushindana na Imamu.. 3
Unapomaliza Tahiyatu.. 3
Kuunyosha mgongo. 4
Kusujudu.. 4

Vyakula vyenye harufu.. 4
Nguo nzuri 4
Sitra.. 5
Msitari 5
Sunna ya Alfajiri 5

Baada ya Swala.. 6
Kuiwahi Rakaa.. 6
Kwenda haja.. 6
Kunyanyua macho. 6
Kutoa salam… 7

Utulivu (Tumaaniyna)
Utulivu (Tumaaniyna) ni nguzo muhimu sana katika nguzo za Swala, na bila ya utulivu Swala haiwi kamilifu.

Siku moja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa amekaa msikitini, akaingia mtu mmoja na kuswali. Baada ya kumaliza akainuka na kwenda kumsalimia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam). Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamuambia:

“Rudi kaswali tena, wewe bado hujaswali.”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alimrudisha mtu huyo mara tatu, na kila anapomaliza kuswali alikuwa akimuambia:

“Rudi kaswali tena, wewe bado hujaswali”.

Yule mtu akamuambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam):

“Sijuwi kuswali vizuri kuliko hivi, (bora) nifundishe”.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamuambia:

“Unapotaka kuswali tia udhu, kisha elekea kibla, kisha soma utakachoweza kusoma katika Qurani, kisha ruku-u mpaka utulie (Tumaaniyna) na uwe na uhakika kuwa umerukuu (sawa), kisha inuka usimame sawa sawa(Tumaaniyna), kisha usujudu mpaka utulie (Tumaaniyna) na uwe na uhakika kuwa umesujudu sawa, kisha kaa vizuri mpaka utulie katika kikao chako(Tumaaniyna), kisha sujudu na utulie (Tumaaniyna) mpaka uwe na uhakika kuwa umesujudu sawa, kisha ufanye hivyo hivyo mpaka umalize kuswali”

Bukhari, Muslim, AbuDaud, Attirmidhy, Annasai na Ibni Majah

Hadithi hii na nyingi kama hizi zinatujulisha kuwa Swala haiwi kamili bila ya utulivu (Tuma – aniyna). Nako ni kutulia katika kila kitendo cha Swala. Mtu anatakiwa atulie mpaka awe na uhakika kuwa ametulia.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amempa jina la ‘Mwizi’ mtu anayeswali bila utulivu.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:

“Katika wezi wabaya kabisa ni wale wanaoiba katika Swala zao, hawarukuu kwa ukamilifu wala hawasujudu kwa ukamilifu na hawawi na khushuu.”

Na katika riwaya nyingine amesema juu ya ‘Mwizi wa Swala’:

“Na wala haunyoshi mgongo wake sawa pale anaporukuu na anaposujudu.”

Imam Ahmad, Al Hakim na imesahihishwa na Imam Al Dhahabi.

Rudi juu

Kudokoa
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amekataza kudokoadokoa katika Swala. Kwa sababu anayeswali kwa pupa bila ya utulivu anakuwa mfano wa kuku anayedokoa mtama, na huwa haipi haki yake Swala, wala hakipi kila kitendo haki yake. Bali hampi Mola wake haki Yake.

Kumbuka kuwa ndani ya Swala yanapita mazungumzo baina yako na Mola wako Subhanahau wa Taala.

Katika hadithi ambayo sehemu ya mwanzo yake ni Hadith Al Qudusiy, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenyezi Mungu anasema; ‘Nimeigawa Swala baina yangu na baina ya mja wangu sehemu mbili, na mja wangu (ninampa) anachoniomba’. Mja anaposema:

“الْحَمْدُ للّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ”

,MwenyeMungu Husema: “Mja wangu amenishukuru”.

Na anaposema:

“الرَّحْمـنِ الرَّحِيمِ”,

Mwenyezi Mungu Husema:“Mja wangu amenipa sifa yangu”.

Na anaposema:

“مَـلِكِ يَوْمِ الدِّينِ”,

Mwenyezi Mungu Husema:

“Mja wangu amenitukuza”, au Husema:“Mja wangu amejisalimisha kwangu ”.

Na anaposema;

“إِيَّاكَ نَعْبُدُ وإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ”,

Mwenyezi Mungu Husema:

“Haya ni baina yangu na baina ya mja wangu na mja wangu atapata atakachoniomba.”

Na anaposema:

“اهدِنَــــا الصِّرَاطَ المُستَقِيمَ. صِرَاطَ الَّذِينَ أَنعَمتَ عَلَيهِمْ غَيرِالمَغضُوبِ عَلَيهِمْ وَلاَ الضَّالِّينَ”.

Mwenyezi Mungu husema:

“Hii ni ya mja wangu na mja wangu atapata anachoniomba”

Mtu anapozungumza na mzee wake au mkubwa wake wa kazini au anapozungumza na mfalme katika wafalme wa dunia, huzungumza naye kwa heshima na utulivu kubwa.

Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala anastahiki zaidi heshima na utulivu huo kuliko viumbe hao dhaifu.

Mmoja katika maulama amemfananisha anayeswali kwa pupa bila ya utulivu kuwa ni sawa na mwenye kunywa dawa chungu anapoweka chungwa lake tayari apate kula mara baada ya kunywa dawa kwa ajili ya kuuondoa uchungu wa dawa. Lakini yule anayestarehe ndani ya Swala yake, mfano wake ni mfano wa mtu anayekunywa kinywaji kitamu. Anakunywa taratibu, akistarehe nayo huku akitamani kinywaji hicho kismalizike.

Mtu anapomjuwa Mola wake, na kuzijuwa neema alizopewa, kisha akaujuwa uwezo wa Mola wake juu yake, huyo ndiye anayemjuwa Nani anayemuabudu, na anampa heshima anayostahiki.

Ibni l Qayim amepiga mfano wa mtu anayemuabudu Mola wake bila ya kumpa heshima anayostahiki kuwa ni mfano wa panya aliyemouwa ngamia, kisha akamchukuwa ngamia huyo na kumpeleka penye tundu lake (tundu la panya) na kumtaka mkewe (ngamia) aingie ndani humo.

Ngamia akamwambia panya:

“Sikiliza bwana, nitafutie nyumba kiasi changu, au tafuta mke kiasi chako”

Ibni l Qayim alimaliza kwa kusema:

“Na hivi ndivyo ilivyo, mtu ama amuabudu Mwenyezi Mungu kama Anavyostahiki kuabudiwa, au atafute kijiungu chake akiabudu kama anavyotaka yeye.”

Rudi juu

Kuichelewesha Swala
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema juu ya wenye kuichelewesha Swala ya Alasiri na kuiswali karibu na Magharibi:

“Hiyo ni Swala ya wanafiki. Anasubiri, analitegea jua mpaka linapokuwa baina ya pembe mbili za shetani, hapo huinuka na kuzidokoa (rakaa) nne, (ndani yake) hamtaji Mwenyezi Mungu isipokuwa kidogo sana.”

Muslim, Attirmidhy na Annasai

Baadhi ya watu wanao mtindo huu wa kuichelewesha Swala ya Alasiri. Wanaiacha mpaka jua linapokaribia kutuwa, ndipo wanapoinuka na kuzidokoa raka nne za Alasiri haraka haraka kabla ya kuadhini Magharibi kwa muda mchache sana, ili abaki na udhu wake apate kuuswalia Magharibi.

Kumbuka kuwa unapokuwa ndani ya Swala, unazungumza na Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, wakati wewe ni dhaifu. Mwenyezi Mungu Mwenye kutowa, wakati wewe ni masikini, muhitaji. Mwenyezi Mungu Mwenye funguo zote za hazina za mbinguni na ardhini. Kwa hivyo swali katika wakati wake na kuwa na utulivu ndani yake huku ukimshukuru na kumuomba, kwani mlango Wake uko wazi wakati wote.

Rudi juu

Isha na Alfajiri katika jamaa
Kuzikosa jamaa mbili hizi ni kujikosesha kheri nyingi sana. Watu wengi baada ya machofu ya kazi ya mchana kutwa huona tabu kuinuka juu ya kiti au mbele ya television na kujikokota kwenda msikitini kuswali Swala ya Isha jamaa pamoja na Waislam wenzake. Hii inatokana na kutokujuwa umuhimu wa kuswali jamaa, pamoja na kutokujuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema nini kuhusu wale wasioziswali Swala hizo katika jamaa na nini wanachokikosa.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:

“Swala nzito kwa wanafiki kuziwsali jamaa ni Swala za Isha na Alfajiri, na lau wangelijuwa faida iliyomo basi wangelikuja hata kwa kusota”.

Muslim, Imam Ahmad, Attabarani, Annasaiy, Ibni Majah na wengine

Na akasema:

“Na atakayeswali Isha katika jamaa, anaandikiwa thawabu ya aliyeswali nusu ya usiku, na atakayeziswali zote mbili katika jamaa (Magharibi na Isha), anaandikiwa thawabu za aliyeswali usiku kucha”.

Muslim, Ibni Hibban, Al Jamia al Kabiyr.

Rudi juu

Kukimbilia Swala
Katika makosa yanayofanywa na baadhi ya wanaoswali ni kule kukimbia wanapokwenda msikitini kwa ajili ya kuiwahi raka-a isiwapite.

Mtume wa Mwenyezi Mungu wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amekataza kitendo hicho pale aliposema:

“Mnaposikia Iqamah, ziendeeni Swala zenu (nendeni msikitini) kwa utulivu na kwa uchaMungu (msiende mbio). Raka-a mtakazoziwahi swalini na mtakazozikosa kamilisheni”.

Bukhari na Muslim

Rudi juu

Kumsubiri Imamu
Baadhi ya watu wanapoingia msikitini na Imamu amesujudu au amekaa, huwa hawafungi Swala na kuingia katika jamaa moja kwa moja. Husubiri mpaka Imamu ainuke ndipo wanapofunga Swala na kujiunga na jamaa.

Kitendo hicho kimekatazwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam).

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:

“Mmoja wenu anapoingia (msikitini) akamkuta Imamu amesujudu au amekaa basi naye amfuate Imamu huyo kwa kujiunga naye katika kile kitendo alichomkuta nacho.”

Attirmidhy

Rudi juu

Kushindana na Imamu
Katika kitendo asichokipenda Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) na kilichokuwa kikimchukiza sana ni kumtangulia Imamu katika kurukuu au kusujudu au kuinuka nk.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amemfananisha mwenye kitendo hicho kuwa sawa na punda.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:

“Haogopi mmoja wenu anapomtangulia Imamu akageuzwa kichwa chake kuwa sawa na kichwa cha punda?”

Addarimy na Ibni Majah

Na akasema:

“Imamu amewekwa ili afuatwe. Akisema: “Allahu akbar” na nyinyi semeni kama yeye. Anaposoma na nyinyi mumsikilize. Anaporukuu nanyi murukuu. Anaposema: “Samia llahu liman hamidah”, semeni: “Rabana laka l hamd”. Na anapokua amekaa nanyi nyote kwa pamoja pia kaeni (kama yeye)”.

Maimamu wote watano isipokuwa Attirmidhiy

Na akasema:

“Hakika mimi ni Imamu wenu. Msinitangulie katika kurukuu wala kusujudu wala kusimama wala kutoa salamu”.

Muslim – Ibni Khuzayma – Al Bayhaqi na wengineo

Maulamaa wanasema kwa vile Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) katika hadithi hii ametumia neno la kiarabu ‘Idhaa’ katika kuunganisha utaratibu wa kumfuata Imamu (FAIDHA kabbara fakabbiru wa idhaa qara-a faansitu), akitufahamisha kuwa ni lazima tuufuate utaratibu huu bila kuchelewa.

Rudi juu

Unapomaliza Tahiyatu
Unapomaliza kusoma Tahiyatu na Imamu bado hajamaliza, badala ya kukaa kimya ni bora mtu asome baadhi ya dua alizotufundisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam).

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alipoulizwa nini mtu afanye anapomaliza kusoma tahiyatu na Imamu bado hakumaliza, akasema:

اللَّهُمَّ إني ظَلَمْتُ نَفْسِي ظُلْماً كَثِيراً وَ لا يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلاَّ أَنْتَ، فاغْفِرْ لِي مَغْفِرَةً مِنْ عِنْدِكَ وَارْحمْنِي إنَّك أَنْتَ الغَفُورُ الرَّحِيم”

“Sema; “Allahumma inniy dhalamtu nafsiy dhulman kathiyraa, walaa yaghfiru dhunuuba illaa anta. Fa- aghfirliy maghfiratan min indika warhamniy, innaka anta l ghafuwru rrahiym”

Bukhari na Muslim

Na maana yake ni;

“Mola wangu mimi nimejidhulumu nafsi yangu dhulma nyingi sana, na hapana anayesamehe madhambi isipokuwa wewe, kwa hivyo nighufirie maghfira kutoka kwako na nirehemu, hakika Wewe ni Mwenye Kusamehe, Mwenye Huruma.”

Na katika hadithi nyingine akasema:

“Mtu anapomaliza kusoma tahiyatu na Imamu bado hajamaliza na asome:

اللَّهُمَّ إِني أعُوذُ بِكَ مِنْ عَذَابِ جَهَنَّمَ، وَمنْ عَذَابِ القَبْرِ، وَمِنْ فِتْنَةِ المَحْيا

والمَماتِ، وَمِنْ شَرِّ فِتْنَة المَسِيحِ الدَّجَّالِ”

“Allahumma inni audhu bika min adhaabi jahannam, wamin adhaabi l qabri, wa min fitnatil mahyaa wa l mamaat, wamin sharri fitnatil masiyhi ddajaal”

Muslim

Na maana yake ni

“Mola wangu najikinga kwako kutokana na adhabu ya Jahannam na kutokana na adhabu ya kaburi na kutokana na mitihani ya uhai na ya kifo na (na najikinga kwako kutokana na) shari ya mitihani ya Masiyhi Dajjaal”

Na katika hadithi nyingine akasema:

“Mmoja wenu anapomaliza kusoma Tahiyatu na Imamu bado hajamaliza, basi na ajichagulie katika dua nzuri nzuri.”

Rudi juu

Kuunyosha mgongo
Katika hadithi iliyosimuliwa na Al Bara-a (Radhiya Llahu anhu) anasema:

“Alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) anaporukuu akiunyosha mgongo wake sawa sawa.”

Na katika riwaya nyingine:

“Alikuwa hainami sana kuelekea chini wala hainuki sana kuelekea juu.”

Al Baihaqi

Imepokelewa katika sifa za kurukuu kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa anaporukuu akiunyosha mgongo wake sawa sawa, hata kama mtu atamwaga maji juu ya mgongo wake basi maji hayo yangetulia.

(Kitabu cha Sifatu Salaatu Nnabiy- Sh. Al Albaniy na Sahih Al Jami-a al Saghiry – hadithi nambari 4732)

Rudi juu

Kusujudu
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:

“Nimeamrishwa kusujudu juu ya mifupa saba;

Mikono miwili (viganja). Magoti mawili. ‘Matumbo ya vidole vya miguu. Kipaji pamoja na pua.”

Na riwaya nyingine inasema; Alikuwa akigusisha kipaji chake na pua yake juu ya ardhi.

Na alikuwa akisema:

“Haifai Swala ya mtu ikiwa hajaimakinisha pua yake juu ya ardhi sawa sawa pamoja na kipaji chake”.

Addaraqutniy na Attabarani – Abu Daud na Imam Ahmad

Na alikuwa pia akiyamakinisha magoti yake juu ya ardhi pamoja na matumbo ya vidole vya miguu yake na akivielekeza vidole kibla.

Bukhari – Abu Daud – Al Baihaqi

Rudi juu

Vyakula vyenye harufu
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akikataza kula vyakula venye harufu ya kukirihisha kabla ya kwenda msikitini.

Alikuwa akisema:

“Aliyekula kitunguu thomu au kitunguu maji au ‘Kurratha’ (mfano wa vitunguu vidogo au majani yake), asiingie ndani ya misikiti yetu na (bora) akae nyumbani kwake mpaka itakapoondoka harufu. Kwa sababu Malaika wanaudhika kwa harufu yoyote inayowaudhi wanadamu.”

Muslim

Rudi juu

Kuvaa nguo nzuri
Mtu anapotaka kumkabili mfalme wa kidunia, au mkuu wake wa kazini basi hukakikisha kuwa amevaa vizuri na ananukia vizuri na utamuona kabla ya kuonana naye kila mara akijitizama penye kiyoo ili ahakikishe kuwa amependeza. Lakini anapokwenda kukabiliana na Mola wake, Mfalme wa wafalme, hayo hayamshughulishi hata kidogo.

Mwenyezi Mungu anasema:

يَا بَنِي آدَمَ خُذُواْ زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ

“Enyi wanadamu chukueni mapambo yenu wakati wa kila Sala.”

Al Aaraf – 31

Rudi juu

Sitra
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa anaposwali hujiwekea Sitra mbele yake. Na Sitra ni kitu chochote kisafi utakachoweka mbele yako wakati wa kuswali umbali wa mahali pa kusujudia kwa ajili ya kuwazuwia watu wasipite mbele yako.

Jambo hili si fardhi lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akilihimiza sana, na alikuwa akifanya hivyo na akausia.

Unaposwali na Imamu haina haja ya kuweka sitra, kwa sababu sitra ya Imamu ndiyo sitra yako, na hata kama mtu atapita mbele yako nawe unaswali, ikiwa Imamu keshaweka sitra huko mbele basi haidhuru.

Imepokelewa katika hadithi nyingi kuwa Masahaba wakubwa kama vile Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) walikuwa wakipita mbele ya safu za nyuma wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akiswalisha na hakuwakataza wala kuwaambia kitu. Hii ikimaanisha kuwa inajuzu mtu kupita mbele ya wanaoswali ikiwa huko mbele Imamu keshaweka sitra.

Kupita mbele ya mtu anayeswali peke yake (baina yake na sitra) ikiwa amejiwekea sitra, au hata kama hakujiwekea, hiyo ni haramu na haijuzu.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:

“Angelijuwa yule anayepita mbele ya mtu anayeswali atalipwa nini (kwa dhambi yake hiyo), basi angehiari asubiri arubaini kuliko kupita mbele yake.”

Aliyesimulia hadithi anasema:

‘Sielewi Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam)) alisema siku arubaini au miezi au miaka arubaini’.

Imepokelewa na Maiamu wote wa hadithi

Na katika hadithi ilipokelewa na Bukhari na Muslim, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alisema:

“Mmoja wenu anaposwali akiwa kieshajiwekea kitu kinachomsitiri, basi anapotaka mtu kupita baina yake na baina ya sitra yake, amsukume. Na kama atashikilia kutaka kupita, basi apigane naye, kwa sababu huyo ni shetani”.

Bukhari na Muslim

Rudi juu

Kuusimamisha msitari

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) anaposima mbele baada ya kuqimiwa Swala alikuwa akisema:

“Simamisheni msitari sawa, kwani kuusimamisha sawa ni katika ukamilifu wa Swala”.

Bukhari na Muslim

Na akisema:

“Wallahi mtasimamisha sawa msitari ama sivyo Mwenyezi Mungu atazifanya nyoyo zenu zikhitilafiane”.

Rudi juu

Sunna ya Alfajiri

Baadhi ya watu huchelewa kufika msikitini, kisha utawaona wakati watu washaanza kuswali wao ndio wanaswali Sunnah ya kabla ya Swala ya Alfajiri au hufanya hivyo wakati Swala inaqimiwa.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema juu ya Sunna hiyo ya kabla ya Swala ya Alfajiri:

“Ninaipenda kuliko dunia na kila kilichokuwemo ndani yake”.

Lakini wakati huo huo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amekataza mtu kuswali Swala za Sunnah wakati Swala ya fardhi inaqimiwa au ishaqimiwa.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:

“Inapoqimiwa Swala, basi hapana kuswali Swala nyingine isipokuwa (ile) iliyofaradhishwa.”

Bukhari – Muslim

Kwa hivyo tujaribu kuwasili mapema msikitini kwa ajili ya kuziwahi rakaa mbili hizo tusije tukakosa kheri nyingi zilizomo ndani yake, au tuziswali nyumbani kabla ya kwenda msikitini kwa ajili ya kuzipata kheri hizo pamoja na kuingiza nuru ndani ya nyumba zetu.

Rudi juu

Baada ya Swala

Kutojishughulisha na kumtaja Mwenyezi Mungu baada ya kumaliza Swala ni kujikosesha kheri nyingi sana.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:

“Anayemsabbihi Mwenyezi Mungu (Subhanallah) baada ya kila Swala ya Fardhi mara 33 Na kumhimidi mara 33 (Alhamdulillah) na kumkabbir mara 33 (Allahu Akbar), hizo ni tisini na tisa, kisha ili kuitimiza idadi ikawa mia moja akasema:

لاَ إِلَهَ إِلاّ الله وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ، لَهُ المُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ وَهُوَ عَلَى كلّ شَيْءٍ قَدِير

”Laa ilaaha illa Llahu wahdahu laa shariyka lahu, lahu l mulku walahu l hamdu wahuwa ala kulli shay in qadiyr,”, basi ataghufiriwa madhambi yake hata yakiwa mengi mfano wa povu la bahari”

Muslim – Abu Daud – Imam Ahmad

Rudi juu

Kuiwahi Rakaa

Unapomkuta Imamu amerukuu ukataka kujiunga na Swala ili uiwahi Raka-a ile, unatakiwa kupiga takbira mbili, moja ya kuingia katika Swala na ya pili ya kujiunga na Imamu katika kurukuu.

Unaporukuu lazima uhakikishe kuwa umemkuta Imamu akiwa bado amerukuu. Imamu akianza kuinua mgongo wake kwa ajili ya kusimama kabla wewe kurukuu, basi huhesabiwi kuwa umeiwahi raka-a ile.

Rudi juu

Kujizuwia kwenda haja

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amekataza mtu kuswali akiwa ameshikwa na haja kubwa au ndogo.

Katika hadithi sahihi, anasema Abu Umama (Radhiya Llahu anhu):

“Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akisema:

“Mmoja wenu asiswali akiwa ameshikwa na haja mpaka akajisaidie (kwanza), na asiingie mmoja wenu katika nyumba ya watu bila ya kuruhusiwa, na Imamu asije akaswalisha watu kisha akajihusisha peke yake kwa dua.”

Muslim – Ibni Majah – Abu Daud – Ahmad

Rudi juu

Kunyanyua macho

Mwenyezi Mungu Anasema:

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ. الَّذِينَ هُمْ فِي صَلاتِهِمْ خَاشِعُونَ

“Hakika wamefuzu Waislam. Ambao katika Sala zao huwa ni wanyenyekevu.”

Al Muuminun 1-2.

Katika kuifasiri aya hii, mfasiri maarufu wa Qurani Ibnu Kathiyr anasema:

“Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) amesema: “Khaashiuun, – maana yake, ‘Wanaoswali wakiwa na uoga pamoja na utulivu.”

Aliy (Radhiya Llahu anhu) amesema: “Khashiuun, – maana yake ni unyenyekevu wa moyo”.

Ibnu Kathiyr akaendelea kusema:

“Hapo mwanzo Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) walikuwa wanaposwali wakinyanyua macho yao juu. Lakini baada ya kuteremka aya hii (قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ. الَّذِينَ هُمْ فِي صَلاتِهِمْ خَاشِعُونَ), wakawa wanateremsha macho yao chini na kuangalia mahala wanaposujudu”.

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akasema:

“Waache (kufanya hivyo) wale watu wanaonyanyua macho yao kutizama juu ndani ya Swala. Yatapofolewa macho yao”

Bukhari – Muslim na wengineo.

Na katika kukataza huku, wanaingia pia wale wanaotizama huku na kule wakiwa ndani ya Swala.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenyezi Mungu anaendelea kumtizama mja wake (kwa rehma) anapokuwa akiswali mpaka pale anapoanza kugeuka na kutizama pengine. Anapougeuza uso wake, na Mwenyezi Mungu huacha kumtizama”.

Ahmad – Annasai – Abu Daud

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alipoulizwa juu ya kugeukageuka katika Swala akajibu:

“Huo ni wizi. Shetani anaiba kwa ujanja katika Swala ya mja”.

Bukhari – Imam Ahmad – Attirmidhiy na wengine

Rudi juu

Kutoa salam

Baadhi ya watu wanapotoa salam, huashiria upande wa kulia kwa kiganja cha mkono wa kulia na upande wa kushoto kwa kiganja cha mkono wa kushoto.

Kufanya hivyo ni makosa.

Kutoka kwa Jabir (Radhiya Llahu anhu) anasema: “Tulipokuwa tukiswali pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), tulikuwa pale tunaposema: ‘Assalaam aleikum wa Rahmatullahi’, tukiashiria mikono yetu pande mbili. Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akasema: ”Mbona nakuoneni mnanyanyua mikono yenu mfano wa wadudu wanaotembea bila kutulia?”

Watu wakaacha kuashiria.

Muslim

Kosa lingine linalofanywa katika kutoa salam, ni pale mtu anapokitingisha na kukipeleka kichwa chake juu na chini wakati anapougeuza uso wake upande wa kushoto baada ya kusalimia upande wa kulia.

Njia sahihi ya kutoa salam ni kugeuka kulia kisha kushoto bila kukinyanyua wala kukishuka kichwa.

Wallahu taala aalam

Wassalaam alaykum wa rahmatullahi wa Barakatuh

Rudi juu

Mapenzi ya Ahli Sunnah juu ya Ahlil Bayt

Mapenzi ya Ahli Sunnah juu ya Ahlil Bayt

(Watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam)

Mapenzi yetu Hadithi ya shuka Nani Ahlul Bayt? Al Mahdi na ‘‘Umar Utangulizi
Fadhila Makhsusi Fadhila za ujumla Fadhila za Ahlul Bayt Elimu ya Ghaibu Watu wa Ukoo
Ibni Abbas (Radhiyal llahu anhuma) Al Abbas (Radhiya Llahu anhu) Al Hassan na Al Hussayn Fatima (Radhiya Llahu anha) Aly (Radhiya Llahu anhu)
Aly bin Musa ‘Al Ridha Musa bin Jaafar ‘Al Kadhim Jaafar As Sadeq Al Baaqer Ali Zeiynul Aabidiyn
Tafsiri ya Al Iyashi Nani Mnafiki Nani Sahaba Wake zake Muhammad bin Musa ‘Al Jawaad
Hitimisho Wajibu wetu Kuoleana

Utangulizi

Mmoja katika wana falsafa wa zamani alisema:

“Haki yote haiwezi kumilikiwa na upande mmoja, wala makosa yote hayawezi kuwepo upande mwingine, bali kila upande husibu sehemu yake. Mfano wa kundi la vipofu waliopelekwa mbele ya tembo wakatakiwa wamguse mwili wake, kisha kila mmoja aelezee umbile lake.

Katika muda mfupi waliopewa, hapana aliyewahi kukamilisha kuushika mwili wote. Kila mmoja alifanikiwa kugusa sehemu tu.

Aliyeushika mkonga akidhani kuwa amemshika tembo wote akasema: “Mwili wa tembo ni mrefu mfano wa gogo la mti”,

Aliyeshika mgongo akasema:

“Hapana, bali mwili wa tembo ni mfano wa jabali dogo”,

Aliyeshika sikio akasema:

“Nilivyouona mimi mwili wa tembo ni mpana, duara na laini”.

Kila mmoja anahadithia juu ya ile sehemu aliyodiriki kuishika katika muda mfupi ule akidhani anatoa maelezo kamili. Wote wamesema kweli, lakini kila mmoja amehadithia sehemu tu ya ukweli anoujua yeye akidhani kuwa ndio ukweli wote.”

Hitilafu husababishwa na mambo mengi, yakiwemo upeo wa kufahamu, kupenda, matamanio ya nafsi, mielekeo ya elimu, ya kifikra, kuiga waliotangulia, kupenda umaarufu, kupenda ukubwa, hitilafu za ustaarabu. Wengine huiga waliyowakuta nayo wazee wao, na wengine wanafuata mafundisho ya walimu wao wanaowaamini n.k. Na wengine huiendeleza hitilafu kwa sababu ya ubishi au kiburi tu, hata kama wataiona haki mbele yao.

Si vibaya kuhitilafiana, kwa sababu Mwenyezi Mungu Ametuumba kila mmoja na akili yake pamoja uwezo wake wa kufahamu.

Mwenyezi Mungu Anasema:

وَلَوْ شَاء رَبُّكَ لَجَعَلَ النَّاسَ أُمَّةً وَاحِدَةً وَلاَ يَزَالُونَ مُخْتَلِفِينَ .إِلاَّ مَن رَّحِمَ رَبُّكَ وَلِذَلِكَ خَلَقَهُمْ.

«Na Mola wako Mlezi Angelipenda Angewafanya watu wote wakawa umma mmoja. Lakini hawaachi kukhitalifiana, Isipokuwa wale ambao Mola wako Mlezi Amewarehemu; na kwa hiyo ndio Mwenyezi Mungu Amewaumba.»

Huud-118-119

Anasema Al Hasan Al Basry: وَلِذَلِكَ خَلَقَهُمْ maana yake ni kuwa; Amewaumba ili wakhitalifiane.

Wenye kukhitilifiana wanaweza kusikilizana na kufahamiana ikiwa hapana chuki baina yao, lakini chuki inapoingia, hayapatikani tena masikilizano wala kufahamiana. Chuki inaondoa mapenzi na inavunja uhusiano mwema na inaendeleza bughudha na kuondoa uwezekano wowote wa masikilizano.

Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) usiku mmoja aliamka uso wake ukiwa mwekundu huku akisema:

لا إِلهَ إِلاّ الله، وَيْلٌ للعَرَبِ، مِنْ شَرَ قَدِ اقْتَرَب

Laa ilaaha illa Llah, Ole wao Waarabu kwa shari iliyo karibu

Alirudia maneno haya mara tatu.

Maulamaa wanasema kuwa;‘Hii ilikuwa ishara kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya hitilafu itakayotokea baada yake’.

Hitilafu iliyopo hivi sasa baina ya Shia na Sunni inakula kibichi na kikavu.

Mamia ya Waislamu wanauliwa kila siku huko Iraq, na wanaendelea kuuliwa, na mamilioni wengine wamejeruhiwa. Mamilioni wamekwishaihama nchi yao, na mamilioni hawana kazi wala bazi.

Lebanon, nchi iliyojaa neema, nchi ya elimu na ziraa. Nchi ya historia na sanaa, leo kila kitu kimesimama katika nchi hii kwa sababu ya fitna ya umadhehebu. Nchi haina serikali, ina majeshi mawili, kila moja linadai kuwa wao ndio wenye kuipenda nchi. Ina makundi mawili, kila moja linalituhumu jingine kuwa ni vibaraka. Watu hawaelewi wanapelekwa wapi, kila siku mapambano ya risasi na mabomu.

Huko Yemen, maelfu ya watu wamekwishapoteza maisha yao katika mapambano baina ya majeshi ya serikali na makundi ya watu wa kabila la Houthi wenye kufuata madhehebu ya Shia Ishnaashariyah.

Hii ni fitna iliyopenyezwa katika mwili wa Waislamu kwa ajili ya kuwagawa. Inatumiliwa na kuchochewa na wale wasiopenda kuuona umma wao umetulia huku ukipiga hatua katika kuziendeleza nchi zao na kuwaelimisha watu wao.

Na katika kila pembe ya ulimwengu chuki hizi zinaanza kupasua njia kidogo kidogo na ni Mwenyezi Mungu peke Yake Anaelewa wapi yataishia.

Mambo yaliyotokea miaka elfu moja mia nne iliyopita yanaendelea kuwagawa na kuwafarikisha Waislamu hadi hivi sasa katika karne hii ya satellite na computer.

Umma huu ni Umma mmoja, Mungu wetu ni Mungu Mmoja, na Dini yetu ni moja na Mtume wetu ni mmoja, Lengo letu ni moja na adui yetu ni mmoja, kwa nini basi hatuungani tukawa kitu kimoja?

Ikiwa kuwapenda watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni Ushia, basi sisi sote ni Mashia, na ikiwa kuwapenda Masahaba (Radhiya Llaahu ‘‘anhum) ni Usunni, basi sote tuwe Masunni. Waislamu hawatakuwa na kheri yoyote ikiwa watawachukia watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ambao Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ametuamrisha tuwaswalie kila tunapomswalia.

Na Waislamu hawatakuwa na kheri yoyote ikiwa watawachukia Sahibu zake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) (Radhiya Llaahu ‘anhum), ambao baada ya kufariki dunia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), wao ndio walioibeba bendera na kuueneza Uislamu kila pembe ya ulimwengu.

Waislamu wanatakiwa waone fahari kubwa kila wanapotajwa Masahaba hawa watukufu (Radhiya Llaahu ‘‘anhum), kwa sababu wao ndio waliotuletea Uislamu. Wao ndio waliotufikishia Qur-aan tukufu ambayo ni Nuru itokayo kwa Mola wetu.

Mwenyezi Mungu Amewajaalia wao kuwa ndiyo sababu ya kutufikia dini hii kote huku tuliko. Kwa juhudi yao kubwa na kujitolea kwao mhanga kwa hali na mali waliuwezesha Uislamu kuingia na kuenea na kufuatwa na kupendwa Arabuni kote, Iran, Asia, Afrika hadi Ulaya na Marekani.

Wangelikuwa watu hawa ni makafiri basi wangelituletea ukafiri badala ya Uislamu. Wangelituletea misalaba na masanamu badala ya Qur-aan na Swalah na salamu (amani ?).

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) kuwa hitilafu baina ya madhehebu ya Kiislamu si katika kiini cha dini na asili ya mafundisho yake, kama vile kuabudiwa Mwenyezi Mungu Mmoja na kwamba Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni Mtume Wake. Hitilafu haikuwa juu ya Qur-aan tukufu, kwani AlhamduliLlaah Waislamu wote kwa pamoja wanaamini kuwa Qur-aan hii tuliyonayo hivi sasa ndiyo ile ile aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) miaka elfu moja mia nne iliyopita bila ya kubadilika.

Tunaelewa kuwa walikuwepo baadhi ya Maulamaa wachache wa madhehebu ya Kishia mfano wa Nuwriy At-Tubrusiy aliyeandika kitabu ‘Faslu l Khitwaab fiy ithbaat tahriyf kitaab Rabbil Arbaab’, akidai ndani ya kitabu hicho kuwa Qur-aan hii tuliyonayo ilibadilishwa na kupunguzwa na kuzidishwa, lakini AlhamduliLlaah katika wakati wetu huu hapana tena anayeziamini kauli hizo hata miongoni mwa wengi kati ya Mashia, ikiwa si wote, na kama watakuwepo basi watakuwa wachache sana.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) pia kuwa hitilafu hii haikuwa katika kuharamisha au kuhalalisha mambo yanayojulikana katika dini kuwa ni ya dharura kama vile uharamu wa Pombe, kula nyama ya nguruwe n.k.

Hapana shaka yoyote kuwa ipo hitilafu juu ya baadhi ya mambo yanayohusiana na Itikadi ‘Aqiydah’, kama vile kumuomba mwengine asiyekuwa Mwenyezi Mungu na kuyatukuzu makaburi ya watu wema.

Naelewa pia kuwa wapo wanaojinasibisha na Ahlus Sunnah wenye kuwaomba wengine wasiokuwa Mwenyezi Mungu na kuyatukuza makaburi ya watu wema, lakini tofauti iliyopo baina ya Sunnah na Shia ni kuwa Maulamaa wa Ahlus Sunnah wanayakemea na kuyakataza mambo haya, wakati maulamaa wa Shia wanayanyamazia na kuyapa kipaumbele.

Al Mahdi na ‘‘Umar
Anasema Dr. Ahmed Al Kaatib mwanachuoni wa Kishia kutoka Iraq ambaye ni mwalimu katika vyuo vikuu mbali mbali vya dini huko Iraq, Kuwait na Iran na ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Majadilianao ya Ustaarabu, ‘Al Hiwaar al Hadhwaariy’, ambayo makao yake makuu yapo London, alisema:

“Nimefanya utafiti ulionipa uhakika kuwa hitilafu iliyopo baina ya Sunnah na Shia hauna msingi wowote na imenithibitikia baada ya kuidurusu kadhia hii kuwa hitilafu zilizokuwepo ni za kisiasa tu na wala si za itikadi.

Baada ya kufanya utafiti wangu ulionichukua muda mrefu sana imenithibitikia kuwa hitilafu iliyokuwepo baina yetu (Shia na Sunnah) ni juu ya Imam Al Mahdi na pia yale madai kuwa ‘‘Umar (Radhiya Llaahu ‘‘anhu) alimpiga Bibi Faatwimah Az Zahraa (‘Alayhas Salaam) siku ile watu walipofungamana na Abu Bakr (Radhiya Llaahu ‘anhu).

Baada ya kumaliza utafiti wangu,” anaendelea kusema Ahmed Al Kaatib ambaye hadi hivi sasa ni mwalimu mkubwa wa madhehebu ya Shia Ithnaashariyah; “imenidhihirikia kuwa madai hayo kuwa ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alimpiga Bibi Faatwimah (Alayhas Salaam) hayana msingi wowote na kwamba ni uzushi ulioenezwa na kuandikwa katika vitabu mbali mbali vya historia kwa ajili ya kuipa nguvu nadharia ya Uimamu, nadharia ambayo inafutika ikithibiti kuwa ‘Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikubali kwa hiari yake kufungamana na Abu Bakr na ‘Umar na ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhum) walipochaguliwa kuwa Makhalifa, kwa sababu angelikuwa Imam ‘Aliy (‘Alayhis Salaam) amechaguliwa na Mwenyezi Mungu, basi asingekubali kufungamana nao kwa hiari yake.

Wazushi wa kisa hicho walidai kuwa Aliy (Alayhis Salaam) alikubali kufungamana na Abu Bakr baada ya Umar kuingia kwa nguvu nyumbani kwake na kumpiga mkewe ambaye ni Bibi Faatwimah (‘Alayhas Salaam) binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) mpaka mimba ikamtoka.”

Anasema Ahmed Al Kaatib:

“Nilikifanyia uchunguzi kisa hiki lakini sijakikuta katika kitabu chochote chenye kutambulika na kuaminika miongoni mwa vitabu vya Kishia kama vile Al Kafi na vyenginevyo.

Kinachokikanusha zaidi kisa hicho ni ule uhusiano mzuri uliokuwepo baina yao hadi kufikia kuwa ‘Aliy na Faatwimah (‘Alayhimas Salaam) walimuozesha binti yao Ummu Kulthum kwa ‘Umar.

Itawezekanaje basi, kwa mama akubali kumuozesha binti yake mtu aliyempiga mpaka mimba ikamtoka?”

“Ama kisa cha Uimamu,” anaendelea kusema Ahmed Al Kaatib: “Hata Ayatollah Sistani ametamka kuwa jambo hili si katika mambo ya msingi wa dini kwa Shia, na kwamba linaweza kujadiliwa.

Nilifuatilia vitabu vilivyoandikwa na waandishi wa Kishia katika karne ya tatu na ya nne na ya tano Hijri nikaona kuwa hapana ushahidi wowote unaothibitisha kuwa Imam huyu alizaliwa, na kwamba Sayed Murtadha na Al Umani na wengine wanasema: “Sisi tunaona kuwa haya ni mambo ya kukisia tu kwa dalili za kiakili na hatuna dalili za kielimu zisizopingika.

Kwa hivyo nadharia ya kuwepo kwa Imam wa kumi na mbili mwenye kusimamia, anayetokana na Imam Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyepewa jina na Muhammad bin Hasan Al Askary na nadharia ya kutoweka kwake, si katika itikadi za Ahlul Bayt, bali wamenasibishwa nazo na baadhi ya waandishi.

Na hivi sasa kwa vile serikali ya Iran imeamua kuipa nguvu nadharia ya Utawala wa mwanachuoni ‘Wilayat al Faqiyh’ na imeamua kufuata nidhamu ya kuchagua viongozi wa dini kwa njia ya kushauriana, ‘Shuura’ na kuchagua viongozi wa nchi kwa njia ya demokrasia (democracy), kwa hivyo haya yanafuta ile kauli ya kuwa kiongozi lazima awe aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu, na badala yake mtu yeyote anaweza kuwa kiongozi ikiwa watu wataridhka naye na kumchagua, (pia siyo lazima awe katika ‘Ahlul Bayt’)

Kwa ajili hiyo ile khitilafu iliyokuwepo baina ya Shia na Sunnah juu ya Uimamu sasa itakuwa ishaondoka pia kwa sababu Shia hawaamini tena juu ya ulazima wa kuwepo Imam aliyetoweka akaingia ndani ya pango na wala hawasubiri tena kutoka pangoni alipoingia miaka elfu moja iliyopita ili wapate kuisimamisha dola ya Kiislamu.

Na lile sharti ya kuwa Imam mwenye kuwaongoza Waislamu lazima awe Aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu na awe aliyekingwa asiyefanya makosa anayetokana na ukoo maalum, nayo pia imeondoka kwa sababu kiongozi hivi sasa anachaguliwa kwa njia ya uchaguzi au kwa kushauriana ‘Shuura’.”

Mwisho wa maneno ya Al Kaatib

(Website ya Al Arabiyah.net. Tarehe 27 May 2008)

Anasema mwanachuoni mwengine maarufu Dr. Musa al Musawiy katika kitabu chake ‘Ash Shi’ah wat Tas’hiyh’’:

«Baada ya utafiti mkubwa nilioufanya katika kulichambua tatizo hili la hitilafu kubwa iliyopo baina ya Shia Ithanaashariyah na Ahlus Sunnah, nimegundua kuwa yale yaliyotokea baada ya kufariki kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) siyo sababu ya hitilafu hii kubwa, wala si kwa sababu ya kuwa ‘Aliy (Alayhis Salaam) ndiye anayestahiki ukhalifa baada ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), kwa sababu nawaona wenye kufuata madhehebu ya Shia Zaydiyah wapo kwa mamilioni katika ulimwengu na wanaishi kwa wema na mapenzi na masikilizano baina yao na Masunni.

Kwa hivyo sababu ya hitilafu baina ya Shia Ithnaashariyah na Madhehebu mengine ya Kiislamu ni ule msimamo wao dhidi ya Makhalifa walioongoka na kuwatukana kwao na kuwalaani, jambo ambalo halipo upande wa Shia Zaydiyah na makundi mengine. Lau kama Shia Ithnaashariyah walingelifuata mwenendo wa Shia Zaydiyah basi hitilafu ingelipungua sana na tatizo lingekuwa dogo. Lakini Shia Ithnaashariyah wameingia katika shimo la kuwatukana Makhalifa walioongoka na kuwalani na kuwashambulia, jambo linalosababisha hitilafu hii izidi na kuongezeka.»

Ash Shi’ah wat Tashiyh’. Uk.4

Kutokana na maelezo haya ya Maulamaa wa Kishia, inatubainikia kuwa laiti kama wafuasi wa Shia wangeliacha mwenendo wa kuwatukana na kuwalaani Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na wake zake Mama wa Waislamu, na lau kama wataacha mwenendo wa kuwatukana na kuwalaani Waislamu wenzao katika siku za Muharram na kuwaapiza kwa kula viapo kuwa lazima watalipa visasi vya kuuliwa kwa Al Husayn, basi sehemu kubwa ya chuki baina ya makundi mawili haya yangeondoka.

Masunni wanawaheshimu sana na kuwatukuza watu wote wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na wanawaheshimu pia Masahaba wake (Radhiya Llaahu ‘anhum), na wanaamini kuwa wote hao ni watu bora ambao Mwenyezi Mungu Ameridhika nao, kama ilivyoandikwa katika Qur-aan tukufu.

Masunni wanajitenga na kila aliyeshiriki katika vile vita vilivyosababisha kuuliwa kwa Al Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu), na wanajitenga na wote waliomuua na waliosababisha kuuliwa kwa Al Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu) na aila yake, na wanaamini kuwa wameuliwa kwa dhulma na kwa uadui, na kwamba wote wamekufa Shahiyd.

Wakati huo huo Masunni wanashangazwa wanaposikia vilio na maneno ya kulipwa visasi katika vikao vya Al Husayniyah. Maneno kama vile:

يا لتارات الحسين

Maneno yanayohimiza kulipwa visasi kwa ajili ya kuuliwa Al Hussayn (Radhiya Llahu anhu).

Wanajiuliza; visasi hivyo watalipiwa nani wakati wote waliomuua Al Husayn (Radhiya Llaahu ‘anhu) wamekwishafariki dunia.

Al Hurr bin Yazid At-Tamimiy keshakufa, ‘Umar bin Dhil Jawshan keshakufa, Zara’a bin Shariyk keshakufa, ‘Umar bin Sa’ad keshakufa, Ubaydullah bin Ziyad naye pia keshakufa, na wote walioshiriki katika vita vile wamekwisharudi kwa Mola wao tokea miaka elfu moja mia nne iliyopita.

Maneno haya ya kuhimiza kulipa visasi yanatafsiriwa na Ahlus Sunnah kuwa wao ndio wanaokusudiwa, na haya ni katika chuki zilizopandikizwa na wasiopenda kuwaona Waislamu wa kila Madhehebu wakiishi pamoja kwa kupendana na kushirikiana katika kuziendeleza mbele dola zao.

Nani Ahlul Bayt?
Mojawapo ya hitilafu kubwa baina ya Sunnah na Shia ni juu ya tafsiri ya neno ‘Ahlul Bayt’. (Watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Wakati Shia wanasema kuwa Ahlul Bayt ni Aly bin Abu Talib na Fatima binti Muhammad na wanawe (Radhiya Llahu anhum) peke yao, Ahlus Sunnah wanaitakidi kuwa Ahlul Bayt ni wote hao waliotangulia kutajwa pamoja na wake wa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na binti zake waliobakia wasiotambuliwa na Shia, na pia wajukuu zake na baadhi ya waliohusiana naye katika ukoo wake.

Imeandikwa katika kamusi maarufu “Lisanul Arab” kuwa; mke na jamaa za mtu ni Ahli Bayti yake.

Na katika Qurani tukufu, Mwenyezi Mungu anawataja wake wa mtu kuwa ni Ahli yake.

Mwenyezi Mungu anasema:

قَالُواْ أَتَعْجَبِينَ مِنْ أَمْرِ اللّهِ رَحْمَتُ اللّهِ وَبَرَكَاتُهُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الْبَيْتِ إِنَّهُ حَمِيدٌ مَّجِيدٌ

“Wakasema: Je, unastaajabia amri ya Mwenyezi Mungu? Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake ziko juu yenu, enyi watu wa nyumba hii! Hakika Yeye ndiye Msifiwa wa kutukuzwa.”

Hud-73

Maulamaa wote wanasema kuwa neno (Watu wa nyumba), katika aya hii anakusudiwa Sarah mke wa Nabii Ibrahim (Alayhi ssalaam).

Na Akasema:

إِذْ رَأَى نَارًا فَقَالَ لِأَهْلِهِ امْكُثُوا إِنِّي آنَسْتُ نَارًا

“Alipo uona moto, akawaambia watu wake (Ahli yake): Ngojeni! Mimi nimeuona moto.”

Taha-10

Inajulikana hapa pia kuwa neno (Ahli yake) anakusudiwa mke wa Nabi Musa (Alayhi ssalaam) aliyekuwa amefuatana naye katika safari hiyo.

Na Mwenyezi Mungu akasema pia:

قَالَتْ مَا جَزَاء مَنْ أَرَادَ بِأَهْلِكَ سُوَءًا إِلاَّ أَن يُسْجَنَ أَوْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Hapana malipo ya mwenye kutaka kumfanyia maovu mkeo isipo kuwa kufungwa au kupewa adhabu chungu.”

Yusuf-25

Neno (Ahlika katika aya hii) na maana yake ni ‘mkeo’ aliyekusudiwa ni mke wa Al Aziz.

Kwa hivyo dalili zote zinaonyesha kuwa neno Ahlul Bayt au Ahl linatumika zaidi kwa maana ya mke.

Na katika Surat Al Ahzab kuanzia aya ya 28 hadi ya 33 Mwenyezi Mungu anasema:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ إِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا فَتَعَالَيْنَ أُمَتِّعْكُنَّ وَأُسَرِّحْكُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا، وَإِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَالدَّارَ الْآخِرَةَ فَإِنَّ اللَّهَ أَعَدَّ لِلْمُحْسِنَاتِ مِنكُنَّ أَجْرًا عَظِيمًا

“Ewe Nabii! Waambie wake zako: Ikiwa mnataka maisha ya dunia na pambo lake, basi njooni, nitakupeni kitoka nyumba, na kukuacheni mwachano mzuri.

Na ikiwa mnamtaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya Akhera, basi Mwenyezi Mungu amewaandalia wafanyao mema, miongoni mwenu, malipo makubwa.”

يَا نِسَاء النَّبِيِّ مَن يَأْتِ مِنكُنَّ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ يُضَاعَفْ لَهَا الْعَذَابُ ضِعْفَيْنِ وَكَانَ ذَلِكَ عَلَى اللَّهِ يَسِيرًا، وَمَن يَقْنُتْ مِنكُنَّ لِلَّهِ وَرَسُولِهِ وَتَعْمَلْ صَالِحًا نُّؤْتِهَا أَجْرَهَا مَرَّتَيْنِ وَأَعْتَدْنَا لَهَا رِزْقًا كَرِيمًا

“Enyi wake wa Nabii! Atakaye fanya uchafu dhaahiri miongoni mwenu, atazidishiwa adhabu mara mbili. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.

Na miongoni mwenu atakeye mt’ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akatenda mema, tutampa malipo yake mara mbili, na tutamwandalia riziki ya ukarimu.”

يَا نِسَاء النَّبِيِّ لَسْتُنَّ كَأَحَدٍ مِّنَ النِّسَاء إِنِ اتَّقَيْتُنَّ فَلَا تَخْضَعْنَ بِالْقَوْلِ فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ وَقُلْنَ قَوْلًا مَّعْرُوفًا

“Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha Mungu basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno mema.”

وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَى وَأَقِمْنَ الصَّلَاةَ وَآتِينَ الزَّكَاةَ وَأَطِعْنَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ

تَطْهِيراً

” Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijahilia ya kizamani. Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt’iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba (ya Mtume), na kukusafisheni baarabara.”

Ahlu Sunnah wanasema kuwa; kama vile katika aya zote zilizotangulia, kila anapotajwa Ahli ya mtu hukusudiwa mke, na katika aya hizi pia Mwenyezi Mungu anapotaja Ahli anawakusudia wake zake Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Ukizisoma kwa utulivu aya hizi utaona kuwa kuanzia aya ya 28 Mwenyezi Mungu anazungumza na wake wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam):

Mwenyezi Mungu anasema : “Ewe Nabii! Waambie wake zako….”, Akaendelea: “Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine.” Akaendelea kuwahutubia: «Kaeni majumbani mwenu» «Toeni Zaka». «Mt’iini Mwenyezi Mungu». Mpaka Aliposema: “Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba (ya Mtume), na kukusafisheni baarabara.” Yote haya wanaambiwa wake zake Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuanzia aya ya 28 hadi 33.

Hivi ndivyo ulivyo mfumo wote wa aya hizi zilizokamatana na haziwezi kutenganishwa isipokuwa kama mtu anataka kuvuka mipaka na kwenda kinyume na nassi.

Mtu anaweza kuuliza: ‘Kwa nini basi Mwenyezi Mungu Ametumia ‘sigha’ (mfumo wa maneno) ya wingi wa wanaume na wanawake kwa pamoja aliposema:

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ ‘Ankum’

Ikiwa Amewakusudia wake za Mtume (Swallah Llahu alyhi wa sallam) kwa nini asitumie sigha ya wanawake peke yao akasema:

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنكُن ‘Ankunnaُ

Kwa nini asitumie sigha ya wanawake kama alivyotumia katika aya nyingine zilizomo ndani ya mfumo huu?

Majibu ni kuwa; Aya za mwanzo Mwenyezi Mungu Alipozungumza juu ya hukmu za kisheria na makatazo na maamrisho yanayowahusu wake za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alitumia ‘Nuun’ ya wanawake عنكن lakini alipozungumza juu ya wema anaotaka kuuingiza ndani ya nyumba ile pamoja na kuwasafisha watu wa nyumba ile barabara, alimuingiza pia na mwenye nyumba ambaye ni mwanamume naye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ili kheri hiyo iwaenee wote. Na kawaida katika lugha ya kiarabu wanapotajwa wanawake na wanaume kwa pamoja hutumiwa wingi wa wanaume عنكم ‘Ankum’

Nani wanaostahiki zaidi kusafishwa na kutakaswa kuliko wake zake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), watu wa nyumba yake, mama wa Waislamu, na wanaostahiki pia ni jamaa zake, watu wa aila yake. Kwa sababu Mtume wetu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) anastahiki kuwa pamoja na kila kheri na kila jema na kila kilicho bora, na anastahiki zaidi kuwa pamoja na watu wema, naye haridhiki isipokuwa awe pamoja na watu wema, kwani wema lazima siku zote uwe katika mtiririko mmoja.

Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala alitaka kuwatakasa wake zake na jamaa zake, akamtunukia haya Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Ikiwa tumemkubali mke wa Nabi Musa (Alayhissalaam) katika aya tuliyotangulia kuitaja kuwa ni Ahli yake na tukamkubali mke wa Al Aziz kama ilivyokuja katika aya kuwa ni Ahli yake na tukamuingiza Sarah mke wa Nabi Ibrahim (Alayhissalaam) kuwa ni Ahli yake, juu ya kuwa katika aya ile Mwenyezi Mungu alitumia mfumo ule ule wa wingi wa wanaume na wanawake kwa pamoja Aliposema:

رحمة الله وبركاته عليكم أهل البيت

Alitumia neno (عليكمAlaykum)

Kama alivyotumia (عنكم Ankum) katika Suratul Ahzab aliposema:

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ

Ikiwa tumewakubali wake wa Mitume wote hao kuwa ni watu wa nyumba, tunalazimika pia kuwakubali wake wa Mtume wetu Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwa ni watu wa nyumba yake.

Hadithi ya shuka na dalili katika Hadithi
Kutokana na haya inafahamika zaidi tafsiri ya ile hadithi maarufu inayoitwa Hadiyth al Kisaa na maana yake ni hadithi ya nguo au hadithi ya shuka, wakati Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipowaingiza ndani ya shuka ile Aly na Bibi Fatima na Al Hassan na Al Hussayn (Radhiya Llahu anhum), kwa ajili ya kuwaingiza na wao katika zile baraka zilizoteremshwa ndani ya aya ile ya Surat al Ahzab.

Hadithi inasimulia kuwa baada ya kuwaingiza wote hao ndani ya shuka, akasema:

“أللهمَّ هؤلاء أهل بيتي فاذهب عنهم الرجس وطهرهم تطهيراً

“Mola wangu hawa ni watu wa nyumba yangu, waondolee uchafu na uwasafishe baarabara.”

Na Ummu Salama (Radhiya Llahu anha) mke wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipoingiza kichwa chake ndani ya shuka hiyo akasema:

“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu na mimi ni katika watu wa nyumba yako.»

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamuambia:

تنحي فإنك على خير

“Wewe umo katika kheri wewe umo katika kheri.”

Na maana yake ni kuwa Ummu Salama na wake wenzake wote wamekwisha tajwa na Mwenyezi Mungu katika aya hiyo na kwamba wao wamo katika kheri hiyo ya kusafishwa na kutakaswa.

Ndiyo maana akaambiwa:

“Wewe umo katika kheri wewe umo katika kheri.”

Dalili nyingine inayothibitisha kuwa wake wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ni katika watu wa nyumba yake imo katika Bukhari na Muslim na Attirmidhy na Annasaiy na wengine kama ilivyopokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipoulizwa na Masahaba:

“Vipi tukuswalie?

Akasema:

“Semeni:

اللهم صل على محمد وأزواجه وذريته، كما صليت على إبراهيم، وبارك على محمد وأزواجه وذريته، كما باركت على آل إبراهيم إنك حميد مجيد

“Mola wangu mswalie Muhammad na wake zake na vizazi vyake, kama ulivyomswalie Ibrahim, na umbariki Muhammad na wake zake na vizazi vyake kama ulivyowabariki watu wa nyumba ya Ibrahim hakika Wewe ni Mwenye kuhimidiwa uliye Mtukufu.”

Ikajulisha kuwa mke wa mtu na vizazi vyake ni watu wa nyumba yake.

Ikiwa mtu hajatoshelezwa na dalili zote tulizozinukuu kutoka katika kitabu cha Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam), basi ipo dalili nyingine katika Sahih al Bukhari itakayoondoa shaka yoyote iliyobaki kwa mwenye kuutafuta ukweli bila ya chuki moyoni mwake.

Inajulikana kuwa Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha) mke wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alisingiziwa uwongo katika kisa mashuhuri kinachojulikana kwa jina la Haadithatul If’k , uwongo ambao Mwenyezi Mungu aliteremsha aya katika Qurani tukufu kuukanusha, na wakati huo huo aya hizo ziliwaonya Waislamu kutorudia tena kueneza uvumi huo, na zikawatahadharisha juu ya adhabu kali itakayomfikia mwenye kurudia tena.

Wakati ule Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipanda juu ya membari yake kuhutubia, akasema:

“يا معشر المسلمين من يعذرني من رجل قد بلغني أذاه في أهلي، فواللّه ما علمت على أهلي إلا خيراً، ولقد ذكروا رجلاً ما علمت عليه إلا خيراً، وما كان يدخل على أهلي إلا معي”

“Enyi Waislamu! Nani atakayenipumzisha na mtu aliyeniudhi katika Ahli yangu, kwani Wallahi sijaona kwa Ahli yangu isipokuwa kheri tupu, na hakuwa akiingia kwa Ahli yangu isipokuwa akiwa pamoja nami.”

Bukhari

Atakayechunguza, ataona kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amelitaja neno Ahly (watu wa nyumba yangu) katika hotuba hii fupi mara tatu, zote zikimaanisha mkewe Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha), ikituthibitishia kuwa neno Ahly lina maana ya mke.

Sisi tunawakubali na tunawapenda na tunawapa heshima kubwa na tunawatambua watu wote wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah LLahu alayhi wa sallam), wale wanaokubaliwa na Shia na pia wasiokubaliwa na Shia kuwa ni katika Ahlul Bayt kama vile ami zake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah LLahu alayhi wa sallam), watoto wa ami zake pamoja na watoto wao (Radhiya Llahu anhum), hawa ambao Shia hawawatambui kuwa ni watu wa nyumba yake (Swallah LLahu alayhi wa sallam), kama walivyotajwa katika hadithi iliyotangulia, nao ni kama ifuatavyo:-

1. Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)

2. Wake zake

3. Binti zake wote

4. Watu wa nyumba ya Al Abbas bin Abdulmuttalib

5. Watu wa nyumba ya Aqiyl bin Abu Talib

6. Watu wa nyumba ya Aly bin Abu Talib

7. Watu wa nyumba ya Jaafar bin Abu Talib

Hawa wote wametajwa katika hadithi iliyotolewa na Muslim wakati Zeid bin Al Arqam (Radhiya Llahuanhu) alipoulizwa:

‘Wake zake si katika watu wa nyumba yake?’

Akasema:

‘Wake zake ni watu wa nyumba yake. Lakini watu wa nyumba yake (waliokusudiwa hapa) ni wale walioharimishwa kupokea sadaka.’

Akaulizwa:

‘Nani hao.

Akasema:

‘Hao ni watu wa nyumba ya Aly na watu wa nyumba ya Aqiyl na watu wa nyumba ya Jaafar na watu wa nyumba ya Abbas (Radhiya Llahu anhum).’

Kwa hiyvo watu wa nyumba hizo juu ya kuwa wengine hawakuwemo ndani ya ile shuka lakini wametajwa kuwa ni watu wa nyumba yake (Swallah LLahu alayhi wa sallam).

Wake zake bila shaka wanaingia katika watu wa nyumba yake kwa sababu ya kutajwa katika Suratul Ahzab kama ilivyotangulia, na ndiyo maana katika kuikamilisha aya hiyo Mwenyezi Mungu akasema :

{ وَاذْكُرْنَ مَا يُتْلَى فِي بُيُوتِكُنَّ مِنْ آيَاتِ اللَّهِ وَالْحِكْمَةِ إِنَّ اللَّهَ كَانَ لَطِيفاً خَبِير}

‘Na watajieni (watu) yasomwayo majumbani mwenu katka Aya za Mwenyezi Mungu na hikima (ya Mtume), kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo ya siri na Mjuzi wa mambo ya dhahiri.’

Al Ahzab-34

Na maana yake ni kuwa zifanyieni kazi zile aya zilizoteremshwa ndani ya nyumba zenu, kwa sababu Mwenyezi Mungu amezihusisha nyumba zenu kwa kuteremsha aya Zake, tofauti na nyumba nyingine. Na Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha) ndiye anayehusika zaidi kwa sababu hazikupata kuteremshwa aya juu ya kitanda cha yeyote miongoni mwa wake wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) isipokuwa kwake.

Na watoto na wajukuu wa Al Hassan bin Aly na Al Hussayn bin Aly na Abdillahi bin Abbas na Muhammad bin Al Hanafiyah (mtoto wa Sayiduna Aly kwa mke mwengine), na Al Abbas bin Aly na wajukuu zao na wajukuu wa wajukuu zao, wote hao pia ni miongoni watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na hii ni kwa wale waliokuwa Waislamu.

Abu Lahab juu ya kuwa ni ami yake Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam), lakini yeye hayumo katika Ahli yake kwa sababu hakuwa Muislamu.

Nabi Nuh (Alayhissalaam) allipomuona mwanawe amekimbilia jabalini na maji yanaanza kumfikia alimuomba Mwenyezi Mungu amuokowe.

Mwenyezi Mungu anasema :

وَنَادَى نُوحٌ رَّبَّهُ فَقَالَ رَبِّ إِنَّ ابُنِي مِنْ أَهْلِي وَإِنَّ وَعْدَكَ الْحَقُّ وَأَنتَ أَحْكَمُ الْحَاكِمِينَ {45}‏ قَالَ يَا نُوحُ إِنَّهُ لَيْسَ مِنْ أَهْلِكَ إِنَّهُ عَمَلٌ غَيْرُ صَالِحٍ فَلاَ تَسْأَلْنِ

مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ إِنِّي أَعِظُكَ أَن تَكُونَ مِنَ الْجَاهِلِينَ {46)

“Na Nuhu alimuomba Mola wake akasema: ‘Ewe Mola wangu! Mwanangu ni katika watu wa nyumbani kwangu. Na hakika ahadi yako ni haki. Nawe ni Mwenye haki kuliko mahakimu (wote).

Akasema (Mwenyezi Mungu), “Ewe Nuhu! Huyu si miongoni mwa watu wako. Yeye ni (mwenye) mwendo usiokuwa mzuri. Basi usiniombe ambayo huyajui . mimi nakunasihi usiwe miongoni mwa wajinga.”

Hud-45-46

Mwenyezi Mungu alimkatalia na kumuambia kuwa huyo si mwanawe, wala si katika watu wa nyumba yake kwa sababu ya kuukanusha ujumbe aliokuja nao Nabi Nuh (Alayhissalaam).

Shia hawakubali kuwaingiza wengine isipokuwa wale tu waliotajwa katika hadithi ya shuka pamoja na maimamu kumi na mbili waliofuata wa madhehebu ya Ithnaasheri kwa sababu wanaamini kuwa hao ndio viongozi wa Waislamu waliotakaswa wasiotenda makosa watakaowaongoza Waislamu baada ya kufa kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) mpaka Siku ya Kiama.

Mapenzi yetu kwa Ahlul Bayt
1- Watu wa Ukoo
Ahlus Sunnah wanawapenda na kuwaheshimu watu wa ukoo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na wamewaweka katika daraja ya juu wanayoistahiki.

Hawa ni binti zake wote, pamoja na Bibi Fatima Al Zahraa na wanawe Al Hassan na Al Hussayn na watu wa ukoo wake tuliotangulia kuwataja kuwa ni katika Ahlul Bayt wakiwemo Aly bin Abi Talib na watu wa nyumba yake, na Al Abbas bin Abdulmuttalib na watu wa nyumba yake, na Aqiyl bin Abi Talib na watu wa nyumba yake na Jaafar bin Abi Talib na watu wa nyumba yake (Radhiya Llahu anhum).

Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na kuwasafisha barabara watu hawa na akatuamrisha katika kitabu chake kitukufu kuwapenda, na pia Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ametuamrisha tuwapende.

Katika Sahih Muslim imeelezwa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipowahutubia watu mahali panapoitwa Ghadiyr aliwaambia:

{ وأهل بيتي، أذكركم الله في أهل بيتي، أذكركم الله في أهل بيتي }.

«Na watu wa nyumba yangu. Nakukumbusheni Mwenyezi Mungu juu ya watu wa nyumba yangu, Nakukumbusheni Mwenyezi Mungu juu ya watu wa nyumba yangu.»

Muslim

Mwenyezi Mungu anasema:

((إِنَّ اللَّهَ وَمَلائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا))

«Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamsalia Nabii. Enyi mlio amini! Msalieni na mumsalimu kwa salamu»

Al Ah’zaab -56

Ilipoteremshwa aya hii Masahaba (Radhya Llahu anhum) walimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam):

«Vipi tukuswalie?»

Akawaambia:

«Semeni:

{اللهم صل على محمد وعلى آل محمد، كما صليت على إبراهيم وعلى آل إبراهيم إنك حميد مجيد، وبارك على محمد وعلى محمد، كما باركت على إبراهيم وعلى آل إبراهيم إنك حميد مجيد}.

“Mola wangu Mswalie Muhammad na Aali ya Muhammad, kama ulivyomswalia Ibrahim na aali ya Ibrahim hakika Wewe ni Msifiwa na Mwenye kutukuzwa. Na umbariki Muhammad kama ulivyombariki Ibrahim na aali ya Ibrahim hakika Wewe ni Msifiwa na Mwenyeye kutukuzwa.”

Anasema Ibnul Qayyim katika kuisherehesha hadithi hii:

Kuwaswalia Aali zake ni katika kukamilisha kumswalia Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kwa sababu kufanya hivyo ni katika kumfurahisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na Mwenyezi Mungu anamuongezea daraja na heshima (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Imepokelewa kuwa Abubakar Al Siddiq (Radhiya Llahu anhu) alisema:

[[ارقبوا محمداً في آل بيته]].

“Mpeni heshima Muhammad kwa (kuwaheshimu) watu wa nyumba yake.”

Na alisema pia:

[[والله لأن أَصِلَ قرابة رسول الله صلى الله عليه وسلم أحب إلي من أصل قرابتي]]

“Wallahi, kuwasiliana na jamaa zake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ni bora kwangu kuliko kuwasiliana na jamaa zangu.”

Bukhari

Na ile hadithi isemayo: « Fatima ni Bibi wa wanawake wa Peponi.»

Imepokelewa kutoka kwa Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha).

Imepokelewa pia kuwa siku ile Abu Sufyan alipokuja kusilimu mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), Umar bin Khataab (Radhiya Llahu anhu) alimuambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam):

«Huyu hapa Abu Sufyan amekuja mwenyewe kwa miguu yake, niruhusu nimkate kichwa chake».

Al Abbas (Radhiya Llahu anhu) ami yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema:

«Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mimi namuingiza Abu Sufiyan katika himaya yangu.»

Al Abbas akakaa karibu na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na alipomuona Umar (Radhiya Llahu anhu) anashikilia kutaka kumkata kichwa Abu Sufyan, Al Abbas akamuambia:

«Taratibu ewe Umar angelikuwa huyu ni katika watu wa kabila lako la Bani Uday bin Kaab usingelishikilia namna hii, lakini kwa vile huyu ni mtu (wa kabila langu) anayetokana na ukoo wa Abdu Manaf.»

Umar akasema kumuambia Al Abbas (Radhiya Llahu anhum):

«Taratibu ewe Abbas, kwani Wallahi naapa kuwa siku uliyosilimu wewe ilikuwa bora kwangu kuliko angelisimu baba yangu Al Khattab, kwa sababu naelewa kuwa kusilimu kwako kulimfurahisha sana Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).»

Attabarani, Al Bidaya wal Nihayah- Ibni Kathiyr na Siyrat Ibn Hisham

Hadithi hizi na nyingi nyingine zinatufundisha namna gani watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) walivyokuwa wakiwapenda Masahaba, na pia Masahaba walivyokuwa wakiwapenda watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na zinatufundisha pia namna gani Ahlu Sunnah walivyojishughulisha kuzitafuta na kuziandika hadithi zinazowahusu watu wa \nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Masahaba na pia ‘Tabi’iyna’ (waliokuja baada yao) walijishughulisha sana kutafuta na kuziandika fadhila za watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ili watakaokuja baada yao wazijuwe na kuzichunga na kuzifuata. Na hii ndiyo sababu utakaposoma kitabu chochote katika vitabu vya Ahli Ssunnah hukosi kuona ndani yake mlango maalum uliohusishwa kwa ajili ya sifa za Ahlul Bayt. Utayakuta haya katika vitabu vya Hadiyth na vitabu vya Aqida na hata katika vitabu vya Tariykh ‘historia’.

Imam Bukhari kwa mfano, amehusisha mlango maalum juu ya fadhila za Imam Aly (Radhiya Llahu anhu), na amehusisha mlango wa fadhila za Bibi Fatima (Radhiya Llahu anha) nk.

Imam Muslim katika mlango wa Fadhila za Masahaba ameandika juu ya fadhila za Maimam Al Hassan na Al Hussayn (Radhiya Llahu anhum).

Imam Attirmidhy na Ibni Maajah na Imam Ahmad bin Hanbal na Ibni Kathiyr na Attabariy na Ibni Taymiyah na Adh’dhahabiy na wengine, wote hawa katika vitabu vyao wameandika kwa mapana na marefu juu ya fadhila za Maimam hawa wawili ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amewaita ‘Mabwana wa vijana wa Peponi.’

Hizi zote ni dalili wazi juu ya heshima tunayowapa watu wa nyumba hii tukufu (Radhiya Llahu anhum).

Elimu ya Ghaibu na Kukingwa
Anasema Ayidh Al Qar’niy katika kitabu ‘Mawaddat Ahlil Bayt inda Ahlis Sunnah:

«Sisi tunawaheshimu na tunawaenzi watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), lakini hatuamini kama wanavyoamini Shia kuwa wao wanajua elimu ya Ghaibu na wamekingwa hawafanyi makosa nk. Tunaamini kuwa mwenye kujuwa ghaibu ni Mwenyezi Mungu peke yake.

Mwenyezi Mungu anasema:

قل لا يعلم من في السموات والأرض الغيب إلا الله” [النمل: 65]

Sema: “Hakuna aliyeko katika mbingu na ardhi ajuaye Ghayb (yasiyotokea) ila Mwenyezi Mungu.”

An Naml-65

Na akasema:

قل لا أملك لنفسي نفعا ولا ضرا إلا ما شاء الله ولو كنت أعلم الغيب لاستكثرت من الخير وما مسني السوء إن أنا إلا نذير وبشير لقوم يؤمنون

Sema: “Sina mamlaka ya kujipa nafuu wala ya kujindolea madhara ila apendavyo Mwenyezi Mungu; na lau kama ningelijua ghaibu ningejizidishia mema mengi; wala isingalinigusa dhara. Mimi si chochote ila ni muonyaji na mtoaji wa habari njema kwa watu wanaoamini.”

Al Aaraf-188

«Na tunaamini kuwa aliyekingwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) peke yake.

Mwenyezi Mungu anasema:

وَاللّهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّاسِ

“Na Mwenyezi Mungu amekukinga“

Al Maidah-67

Sisi tunaamini kuwa hapana yeyote aliyekingwa (Maaswum معصوم), si katika watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) wala katika Masahaba wake, kwa sababu zifuatazo:-

1. Hapana nassi iliyo wazi isiyopingika inayoeleza juu ya kukingwa kwao. Lau kama ingekuwepo basi tungelifuata bila matatizo wala kipingamizi.

2. Hapana hata mmoja katika watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliyedai kuwa yeye amekingwa, akawataka watu waamini hivyo, isipokuwa katika vitabu ambavyo maulamaa wote kama vile Ibni Kathiyr na Ibni Hajar na Adhahaby na wengineo wamesema kuwa hadithi hizo si dhaifu tu, bali maudhui. (zimepachikwa).

3. Hapana hata mwanachuoni mmoja katika maulamaa wetu aliyesema hivyo, juu ya kukhitalifiana kwao katika mambo mengi, lakini juu ya jambo hili hapana hitilafu baina yao.

4. Lau kama wangelikuwa wamekingwa, basi wasingelikubali kukosolewa na mtu yeyote katika Ijtihadi zao. Kwa mfano kama Aly (Radhiya Llahu anhu) angelikuwa amekingwa, basi asingelikubali kukosolewa na Abubakar au Umar au Uthman (Radhiya Llahu anhum), na anapokosolewa angelisema kwa mfano; ‘Vipi mnanikosoa wakati mimi nimekingwa?’

Lakini Aly alikuwa akiwakosoa na wao walikuwa wakimkosoa, akiwaheshimu na wao wakimuheshimu, akiwapenda na wao wakimpenda.

5. Maulamaa wanasema kuwa التطهير ‘kusafishwa’ kama ilivyokuja katika aya, maana yake si kukingwa, bali ni kusafishwa na kutakaswa. Na si kila aliyetakaswa amekingwa akawa hafanyi makosa, ama sivyo basi kila aliyesifiwa kuwa ametakaswa au amesafishwa atakuwa amekingwa. Kama ilivyokuja katika hadithi:

واجعلني من التوابين واجعلني من المتطهرين

Na unijaalie niwe miongoni mwa waliotubu na unijaalie niwe miongoni mwa wenye kujitakasa.

Na Mwenyezi Mungu anawapenda wenye kutubu na anawapenda wenye kujitakasa, lakini haimaanishi kuwa hao wamekingwa hawafanyi makosa.

6. Kama Muislamu atachukua elimu yake kutoka katika Qurani na Mafundisho ya Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) peke yake bila ya kuchukua kutoka kwa watu wa Ahlul Bayt, huyo Uislamu wake unakuwa sahihi na hauna dosari yoyote. Wangelikuwa Ahlul Bayt wamekingwa ‘Maasumiyn’, basi ingelimuwajikia kila Muislamu kuchukua elimu kutoka kwao.

7. Kwetu Ahlus Sunnah, Abubakar na Umar ni viumbe bora kupita wote baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam). Na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) mara zote alikuwa akiwatanguliza mbele ya Aly. Alikuwa akimuacha Abubakar aswalishe na Aly akiswali nyuma yake, na hapana hata mmoja katika Ahlis Sunnah aliyewahi kusema kuwa Abubakar amekingwa (Maaswum معصوم). Itakuwaje basi awe mwengine asiyekuwa yeye?

8. Imepokelewa kuwa Aly (Radhiya Llahu anhu) aliwasifia waliojitenga katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, na alijuta kwa yaliyotokea katika vita vya ngamia na vita vya Swiffiyn. Angelikuwa amekingwa asingetenda matendo kisha akajuta.

9. Imepokelewa kuwa Aly (Radhiya Llahu anhu) alipanda juu ya membari katika mji wa Al Kufa akasema:

«Namshitakia Allah dhiki zangu na matatizo yangu.» Kisha akasema:

«Wana daraja zao kwa Mwenyezi Mungu Muhammad bin Maslamah na Usama bin Zeyd na Saada bin Abi Waqaas. Kama ni shari basi ndogo, na kama ni kheri basi ni nyingi (kwa kujitenga kwao na fitna).»

Naye ni mkweli (Radhiya Llahu anhu), lakini angelikuwa Maasuwm basi asingetamka haya. Asingewasifia waliojitenga na fitna ile wakati yeye mwenyewe alikuwemo ndani yake.

10. Siku ya Saqiyfah, siku ile baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kufariki dunia, wakati Waislamu walipojumuika na kumchagua Abubakar kuwa Khalifa wao, hapana hata mmoja aliyejitokeza akasema : «Jamani tunaye aliyekingwa hapa, kwa hivyo yeye ndiye anayestahiki kuchaguliwa.» Hilo halijatokea, na siku ile walikuwepo waliopigana vita vya Badar na pia walikuwepo wale ambao Mwenyezi Mungu alitangaza kuridhika nao chini ya mti. Inaingia akilini kweli kuwa watu wote hao waliosifiwa na Mwenyezi Mungu ndani ya Qurani tukufu, na wakasifiwa na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) wafanye njama dhidi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wasallam)?

(Mwisho wa maneno ya Ayidh Al Qar’niy)

Mawaddat Ahlil Bayt inda Ahlis Sunnah Uk.317-322

Fadhila za Ahlul Bayt
Tunaweza kugawa fadhila za Ahlul Bayt katika mafungu mawili:-

1. Fadhila za ujumla

2. Fadhila makhsusi

Kwanza Fadhila za ujumla
Fadhila za ujumla mfano wa hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliposema:

{ وأهل بيتي، أذكركم الله في أهل بيتي، أذكركم الله في أهل بيتي }.

«Na watu wa nyumba yangu. Nakukumbusheni Mwenyezi Mungu juu ya watu wa nyumba yangu, Nakukumbusheni Mwenyezi Mungu juu ya watu wa nyumba yangu.»

Muslim

Na fadhila zilizotajwa katika Surat al Ahzab:

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيراً

“Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba (ya Mtume), na kukusafisheni baarabara.”

Ndani yake fadhila hizi wanaingia wake wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kwa sababu wao ndio waliokusudiwa, na pia wanaingia Sayiduna Aly na Bibi Fatima na Al Hassan na Al Hussayn (Radhiya Llahu anhum) kupitia hadithi ya Al Kisaa.

Fadhila za ujumla zinapatikana pia katika kutoa shahada ndani ya Swala wakati wa kusoma Tahiyatu, tunaposema:

اللهم صل على محمد وعلى آل محمد

“Mola wangu mswalie Muhammad na Aali yake Muhammad”

Na yote haya yanatokana na fadhila zao na daraja yao mbele ya Mwenyezi Mungu.

Fadhila Makhsusi
Wafuatao ni baadhi ya watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na hawa ni maimamu kumi na mbili wa Shia:-

1. Aly bin Abu Talib

2. Al Hassan

3. Al Hussayn

4. Aly bin Al Hussayn (Zeinul Abedeen)

5. Muhammad bin Aly bin Al Hussayn (Al Baqer)

6. Jaafar Al Sadeq

7. Musa Al Kadhim

8. Aly Ridha

9. Muhammad Al Jawaad

10. Aly Al Haadi

11. Al Hassan Al Askary

12. Muhammad (Imam wa kumi na mbili wanayemsubiri)

Hawa tunaweza kuwagawa makundi manne.

1- Kundi la mwanzo ni Masahaba (waliomuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam)), nao ni Aly na Al Hassan na Al Hussayn (Radhiya Llahu anhum).

2- Kundi la pili ni maulamaa wacha Mungu miongoni mwa maulamaa wa Ahlis Sunnah wal Jama’a nao ni:

1-Aly bin al Hussayn
2-Muhammad Al Baqer

3-Jaafar al Sadeq
4-Musa Al Kadhem

5-Ali Ridha
6-Muhammad Al Jawaad

3- Kundi la tatu; hawa ni wacha Mungu lakini si katika maulamaa na inawatosha fahari ya kuwa wanatoka katika nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na wanayo haki ya kwenda penye kaburi la Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na kusema:

‘Assalaam alayka ewe baba yangu.’

Na hawa ni: Aly Al Haadi na Al Hassan Al Askary.

4- Sehemu ya nne ni mtu asiyezaliwa wanayemsubiri, naye ni Muhammad bin Al Hassan.

Aly bin Abu Talib (Radhiya Llahu anhu)
Wa mwanzo wao ni Aly bin Abu Talib (Radhiya Llahu anhu) ambaye ni mtoto wa ami yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na mume wa Bibi wa mabibi wa Peponi Fatima (Radhiya Llahu anha) binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam). Na Aly (Radhiya Llahu anhu) ni Khalifa wa nne muongofu, na ni katika wale kumi waliobashiriwa kuingia Peponi.

Ndani ya Bukhari na Muslim ipo hadithi kutoka kwa Abul Abbas Sahal bin Saad Al Saidiy (Radhiya Llahu anhu), aliyesema kuwa siku ya vita vya Khaibar, Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alisema:

(لأعطين هذه الراية غدا رجلا يفتح الله على يديه، يحب الله ورسوله ويحبه الله ورسوله)

“Nitampa bendera hii kesho, mtu ambaye atatupa ushindi Mwenyezi Mungu kwa mikono yake. (Mtu huyo) Anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake na anapendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake”.

Anaendelea kusema Sahal (Radhiya Llahu anhu):

“Usiku kucha watu walikuwa wakiwaza wakitaka kujua ni nani huyo mwenye kupendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake atakayepewa bendera hiyo. Asubuhi yake watu wote wakaamkia kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), kila mmoja akitamani apewe yeye bendera siku hiyo”.

Baada ya watu kujikusanya mbele yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akauliza:

“Yuwapi Aly bin Abi Talib?….”

Bukhari na Muslim

Na akasema pia (Swallah Llahu alayhi wa sallam) juu ya Aly (Radhiya Llahu anhu):

لا يحبك إلا مؤمن، ولا يبغضك إلا منافق

«Hakupendi isipokuwa muumini na hakuchukii isipokuwa mnafiki »

Na sisi Wallahi tunampenda na kumuenzi na kumheshimu yeye na mkewe na watoto wake wote (Radhiya Llahu anhum). Hadithi zake zimejaa ndani ya vitabu vyetu. Hekima yake tunaitumia na tunawafunza watoto wetu. Mashairi yake yaliyojaa mafunzo ya kheri na busara tunayasoma na kuyarudia na tunamfunza kila mmoja wetu.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema pia:

{أما ترضى أن تكون مني بمنزلة هارون من موسى} وزاد مسلم: { إلا أنه لا نبي بعدي}

Bukhari

«Hutoridhika ukiwa wewe kwangu upo katika daraja ya Harun kwa Musa» na Muslim akaongeza: «Isipokuwa hapana Mtume baada yangu».

Hadithi zote hizi na nyingi nyingine zimo ndani ya vitabu vya Ahlis Sunnah zikituhakikishia kuwa hatuna uzito wowote kwetu katika kuzitaja au kuziandika ndani ya vitabu vyetu na hata kuzisema hadharani, bali ni fahari kwetu kufanya hivyo, kwa sababu hawa ni watu wa nyumba ya Mtume wetu Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Fatima (Radhiya Llahu anha)
Bibi Fatima (Radhiya Llahu anha) binti yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam). Kipenzi chake (Swallah Llahu alayhi wa sallam). Manukato yake mazuri aliyesema juu yake :

{إن فاطمة بضعة مني يؤذيني ما آذاها}

«Hakika Fatima ni sehemu inayotokana na mimi kinaniudhi kinachomuudhi»

Muslim

Na akasema kumuambia Fatima:

{أما ترضي أن تكوني سيدة نساء المؤمنين، أو سيدة نساء هذه الأمة}

«Huridhiki ukiwa wewe ni Bibi wa wanawake waumini, au Bibi wa wanawake wa umma huu»

Na katika Bukhari :

فاطمة سيدة نساء أهل الجنة

« Fatima ni Bibi wa wanawake wa Peponi»

Al Hassan na Al Hussayn
Tunawaheshimu na kuwapenda pia Al Hassan na Al Hussayn (Radhiya Llahu anhum), na ndani ya vitabu vya Ahlus Sunnah utakuta maelezo mengi juu ya wajukuu hawa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliyokuwa akitamka mbele ya Masahaba (Radhiya Llahu anhum). Alikuwa akisema:

اللهم إني أحبهما فأحبهما

‘Mola wangu kwa hakika mimi ninawapenda na Wewe wapende’

Attirmidhiy

Na akasema:

الحسن والحسين سيدا شباب أهل الجنة

‘Al Hassan na Al Hussayn ni mabwana wa vijana wa Peponi’

Attirmidhy na Ahmad na Al Hakim na wengine

Al Abbas bin Abdul Muttalib (Radhiya Llahu anhu)
Huyu ni ami yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah llahu alayhi wa sallam) aliyesema juu yake:

عم الرجل صنو أبيه

‘Ami yake mtu ni sawa na baba yake

Attirmidhy

Abdillahi bin Abbas (Radhiya Llahu anhuma)
Huyu ni mtoto wa ami yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliyemuombea dua nzuri aliposema:

{اللهم علمه التأويل وفقهه في الدين}

“Mola wangu mpe elimu ya kujuwa uhakika wa mambo na mjaalie awe na fiq-hi katika dini.”

Ahmad

Ali Zeiynul Aabidiyn (Radhiyal Llahu anhu)
Huyu ni Aly bin Al Hussayn bin Aly bin Abi Talib (Radhiya Llahu anhum) ambaye amesema Imam Al Zuhry juu yake:

‘Sijapata kumuona mtu kutoka kabila la Quraysh aliye bora kupita yeye.’

Na alisema Said bin Musayib:

‘Sijapata kumuona mcha Mungu kupita huyu.’

Muhammad bin Aly bin Al Hussayn ‘Al Baaqer’ (Radhiyal Llahu anhu)
Amesema juu yake Abu Naeem:

‘Alikuwa mtu wa kuaminika, mwingi wa elimu na hadithi.’

Jaafar bin Muhammad (Radhiyal Llahu anhu)
Huyu ndiye Jaafar As Sadeq bin Muhammad Al Baqer ambaye Imam Abu Hanifa alisema juu yake :

‘Sijapata kuona mtu mwenye elimu ya fiq’hi kupita Jaafar bin Muhammad.’

Amesema pia juu yake Ibni Hibban :

‘Mwenye kuaminika asiye na mfano.’

Amesema Imam Adhahaby :

« Imam As Sadeq ni Shekhe katika Mashekhe wa Kikureshi anayetokana na ukoo wa Bani Hashim na ni miongoni mwa maulamaa wao.»

Musa bin Jaafar ‘Al Kadhim’ (Radhiyal Llahu anhu)
Huyu ni mtoto wa Jaafar As Sadeq (Radhiya Llahu anhu)

Amesema juu yake Ibni Tayimiyah:

« Mashuhuri kwa kufanya ibada na kuhiji.»

Akasema Abu Hatim Al Razi:

« Ni mwenye kutegemewa msemakweli, Imam katika maimamu wa Kiislamu.»

Amesema juu yake Ibni Kathiyr:

« Alikuwa mwingi wa kufanya ibada na mwenye kuheshimika.»

Anasema Adhahaby katika ‘Siyar’ kuwa siku moja Harun Al Rashiyd alipokuwa katika Hija alikwenda mbele ya kaburi la Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na alikuwa pamoja naye katika safari hiyo Musa bin Jaafar Al Kadhim (Radhiya Llahu anhu). Harun Al Rashiyd alipofika penye kaburi la Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema kwa ufahari mbele ya watu: “Assalaam alayka ewe mtoto wa ami yangu.” Harun Al Rashiyd anatokana na ukoo wa Al Abbas bin Abdul Muttalib (Radhiya Llahu anhu). Musa bin Jaafar naye akasogea mbele ya kaburi hilo kisha akasema: “Assalaam alayka ewe baba yangu.”

Uso wa Harun Al Rashiyd ulibadilika. Akamtizama kisha akamuambia: “Hili Wallahi ni la kujionea fahari.”

Aly bin Musa ‘Al Ridha’
Amesema juu yake Ibni Hibban:

« Huyu ni miongoni mwa mabwana wa Ahlul Bayt na katika wenye hekima.»

Na Adhahaby amesema juu yake :

« Alikuwa mwenye shani kubwa mwenye kustahiki ukhalifa.»

Muhammad bin Aly bin Musa ‘Al Jawaad’
Amesema juu yake Ibni Taymiyah:

«Alikuwa miongoni mwa watu wema na mkarimu sana, na kwa ajili hii alipewa jina la Al Jawaad. Na alikuwa mwenye kuheshimika sana.»

Yote haya yanabatilisha zile kauli kuwa Masunni hawawapendi watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Alipotuhumiwa Abdullah mwana wa Imam Muhammad bin Abdul Wahaab kwamba alisema kuwa watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hawana haki yoyote” akajibu:

“Subhana Llah huu ni uongo mkubwa. Waliotuzulia haya au kutunasibisha nayo wamesema uongo mtupu juu yetu.”

Na hivi ndivyo ilivyo kwa wote wanaotokana na ukoo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na pia wajukuu wote wa Sayiduna Aly (Radhiya Llahu anhu), wote tunawapenda bila kuwafarikisha na wote wamepewa sifa wanazozistahiki ndani ya vitabu vya Sunni ikiwa ni dalili wazi kuwa watu hawa tunawaenzi na kuwaheshimu.

Shia juu ya kudai kwao kuwa wanawapenda na kufuata mwenenendo wa watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), lakini ukweli ni kuwa wao wanawafarikisha na kuwatenga wengine. Kwa sababu watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kwao ni Aly na Fatima na Al Hassan na Al Hussayn na watoto wao na wajukuu zao peke yao, na wengine wasiokuwa hao wamewatoa katika sifa hii.

Aly (Radhiya Llahu anhu) alioa wake wengine akazaa nao watoto wengi, lakini Mashia hawahesabu watoto hao kuwa ni Ahlul Bayt.

Watoto wengine wa Aly (Radhiya Llahu anhu) kama vile Muhammad bin Al Hanafiyah, Abubakar bin Aly, Umar bin Aly na Uthman bin Aly na Abbas, wote hawa ni watoto wa Sayiduna Aly (Radhiya Llahu anhu).

Wamewatoa pia mabinti wengine wa Aly kama walivyowatoa mabinti wengine wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), nao ni Zeinab na Ruqayah na Ummu Kulthum, kama walivyowatoa wake wa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hapo mwanzo.

2- Wake zake
Sisi tunaamini kuwa wake wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ni katika watu wa nyumba yake, na kwamba wao ni mama zetu.

Mwenyezi Mungu anasema:

(( النَّبِيُّ أَوْلَى بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنْفُسِهِمْ وَأَزْوَاجُهُ أُمَّهَاتُهُمْ ))[الأحزاب:6]

«Nabii ana haki zaidi kwa Waislamu kuliko nafsi zao.na wakeze ni mama zao.»

Al Ahzab -6

Na akaharamisha kuwaoa baada ya kufariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Mwenyezi Mungu anasema:

(( وَمَا كَانَ لَكُمْ أَنْ تُؤْذُوا رَسُولَ اللَّهِ وَلا أَنْ تَنْكِحُوا أَزْوَاجَهُ مِنْ بَعْدِهِ أَبَدًا))

«Wala haikupasieni kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu. Wala kuwaoa wake zake baada yake kabisa. Hakika jambo hilo ni dhambi kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.»

Al Ahzab-53

Tunawapa heshima kubwa mama zetu hawa, na wa mwanzo wao ni Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha. Wa mwanzo kuamini, aliyemsaidia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kwa hali na mali huku akimpa moyo na kumliwaza kila anapopatwa na masaibu au shida. Bibi Khadija ndiye aliyeambiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam):

“إن اللّه أمرني أن أبشر خديجة ببيت في الجنة لا صخب فيه ولا نصب”

“Mwenyezi Mungu ameniamrisha nimpe bishara njema Khadija juu ya nyumba yake Peponi ya Lulu, hamna zogo ndani yake wala tabu (yoyote).”

Bukhari na Muslim

Na kutoka kwa Aly bin Abi Talib (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:

خير نسائها مريم بنت عمران، وخير نسائها خديجة بنت خويلد

«Mwanamke bora (katika zama zake) ni Maryam binti Imran, na mwanamke bora (katika zama zake) ni Khadija binti Khuwaylid»

Bukhari na Muslim

Kisha anafuatia Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha), binti wa Abubakar Al Siddique (Radhiya Llahu anhu), Bibi aliyetakaswa kutoka mbingu ya saba baada ya mnafiki yule aliyejitwika sehemu yake kubwa katika uzushi wake ambaye ni Abdullahi bin Ubay bin Saluul kueneza uvumi mbaya juu ya mama huyu wa Waislamu kipenzi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Maulamaa wote wamekubaliana kuwa kumsingizia uwongo bibi Aisha (Radhiya Llahu anha) katika kile kisa cha uwongo alichozuliwa (hadithi ya “Al-Ifki”) wakati MwenyeziMungu kishamtakasa, basi anakuwa si Muislamu tena.

MwenyeziMungu anasema:-

إِنَّ الَّذِينَ جَاؤُوا بِالْإِفْكِ عُصْبَةٌ مِّنكُمْ لَا تَحْسَبُوهُ شَرّاً لَّكُم بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُم مَّا اكْتَسَبَ مِنَ الْإِثْمِ وَالَّذِي تَوَلَّى كِبْرَهُ مِنْهُمْ لَهُ عَذَابٌ عَظِيمٌ {11} لَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْراً وَقَالُوا هَذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ {12} لَوْلَا

جَاؤُوا عَلَيْهِ بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاء فَإِذْ لَمْ يَأْتُوا بِالشُّهَدَاء فَأُوْلَئِكَ عِندَ اللَّهِ هُمُ الْكَاذِبُونَ {13} وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ لَمَسَّكُمْ فِي مَا أَفَضْتُمْ فِيهِ عَذَابٌ عَظِيمٌ {14} إِذْ تَلَقَّوْنَهُ بِأَلْسِنَتِكُمْ وَتَقُولُونَ بِأَفْوَاهِكُم مَّا لَيْسَ لَكُم بِهِ عِلْمٌ وَتَحْسَبُونَهُ هَيِّناً وَهُوَ عِندَ اللَّهِ عَظِيمٌ {15} وَلَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَذَا سُبْحَانَكَ هَذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ {16} يَعِظُكُمُ اللَّهُ أَن تَعُودُوا لِمِثْلِهِ أَبَداً إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ {17} وَيُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمُ الْآيَاتِ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ {18} إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَاللَّهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ {19} وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ وَأَنَّ اللَّه رَؤُوفٌ رَحِيمٌ {20}‏

“Hakika wale walioleta uwongo huo (wa kumsingizia bibi AishaRadhiya Llahu anha) mkewe Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwa amezini)) Ni kundi miongoni mwenu (ni jamaa zenu) msifikiri ni shari kwenu bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata aloyachuma katika madhambi yao na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao atapata adhabu kubwa (zaidi).

Kwa nini mlipo sikia khabari hii, wanaume Waumini na wanawake Waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhaahiri?

Kwa nini hawakuleta mashahidi wane? Na ilivyo kuwa hawakuleta mashahidi wane basi hao mbele ya Mwenyezi Mungu ni waongo.

Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake katika dunia na

Akhera, bila ya shaka ingeli kupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyo jiingiza. Mlipoupokea (uwongo huo mkawa mnautangaza) kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyo yajua, na mlifikiri ni jambo dogo, kumbe mbele ya Mwenyezi Mungu ni kubwa.

Na kwa nini mlipo yasikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya. Subhaanaka (Mola wetu) Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa!?

Mwenyezi Mungu anakuonyeni msirudi kabisa (msirejee tena) kufanya kama haya, ikiwa nyinyi ni Waumini! (Waislamu) kweli.”

An Nur– 11-17

Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala katika aya hizi ametumia neno; ‘Subhaanaka’ katika kumtakasa Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha) kutokana na uwongo aliozuliwa, na neno hili ‘Subhanaka’ Mwenyezi Mungu analitumia katika kukanusha uongo mkubwa tu, Anaponasibishwa na mwana au mshirika.

Mwenyezi Mungu amesema:

سُبْحَانَكَ هَذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ

(Mola wetu) Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa!?’

Anasema Az Zamakhshary:

“Alipokanusha kuwa hana mwana wala mshirka alisema:

وَقَالُواْ اتَّخَذَ اللّهُ وَلَداً سُبْحَانَهُ بَل لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ كُلٌّ لَّهُ قَانِتُونَ

“Na wanasema:”Mwenyezi Mungu amejifanyia mtoto” ‘Subhaanahu’ Ameepukana na hilo bali ni vyake hivyo vilivyomo mbinguni na ardhini . Vyote vinamtii Yeye.”

Al Baqarah-116

Na akasema:

مَا كَانَ لِلَّهِ أَن يَتَّخِذَ مِن وَلَدٍ سُبْحَانَهُ

“Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kufanya mtoto; ‘Subhanahu’ Ametakasika.”

Maryam-35

Amelitumia neno ‘Subhanahu’ kwa ajili ya kujitakasa na kukanusha kuwa anaye mwana, na amelitumia neno hilo hilo ‘Subhanahu’ katika kuukanusha uwongo aliozuliwa Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha).

Miongoni mwa wake wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) pia ni Ummu Salamah (Radhiya Llahu anha), mama yetu mtulivu wa tabia, mwenye akili yenye uwezo wa kupima mambo, mwingi wa hekima ambaye Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) mara nyingi alikuwa akichukuwa ushauri wake katika baadhi ya mambo. Alimshauri siku ile ya Sulhu ya Hudaibiya na akapata ushauri mwema kutoka kwake.

Hawa na wake zake wengine wote ni mama zetu. Ni watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kama ilivyokuja katika aya za Surat al Ahzab, na kama tulivyoona katika dalili mbali mbali kutoka katika Qurani tukufu na katika Mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Inatuwajibikia kuwapenda na kuwaenzi na kuwaheshimu mama zetu hawa.

Baada ya kumalizika vita vya Ngamia (Waqaat al Jamal), Aly (Radhiya Llahu anhu) aliamua kumuacha huru Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha). Wafuasi wake wakamuuliza:

«Inakuwaje halali kumwaga damu zao na haiwi halali kwetu mali zao na mateka wao?»

Aly (Radhiya Llahu anhu) akasema:

«Yupi kati yenu atakayefurahi Mama wa Waislamu awe mateka wake?»

Wote wakanyamaza.

Ikiwa ni haramu kumsema vibaya Muislamu yeyote, basi inakuwa vibaya zaidi kuwasema vibaya watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) wakiwemo wake zake na watu wa ukoo wake pamoja na wajukuu wake na wajukuu wa wajukuu wakiwemo Al Hassan na Al Hussayn na Abdullah bin Al Hassan na Aly bin Al Hassan na Muhammad bin Alyn a Jaafar bin Muhammad na Musa bin Jaafar na Aly bin Musa Al Ridha na waliobaki, na pia Sahaba zake (Radhiya Llahu anhum) wote kwa pamoja wa Makkah na wa Madina, na wale ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amewabashiria Pepo, na pia viongozi wetu wa dini.

Haiwezekani ukapatikana umoja wa Waislamu ikiwa kundi lolote litakuwa shughuli yao kubwa ni kuweka vikao vya kila mwaka kuwalani na kuwatukana Watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) wakiwemo wake zake, au Sahaba zake (Radhiya Llahu anhum), kwa sababu hawa ni viongozi wetu waliokuwa naye tokea siku ile ya mwanzo. Hawa ni mifano mema kwetu, walioisimamia dini hii na kuieneza ulimwenguni kote, na hawa ndio waliotufikishia dini hii baada ya kujitolea mhanga roho zao na mali zao.

Wakati huo huo sisi tunaamini kuwa watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) wanatoka katika nyumba bora kupita zote, lakini pia tunaamini kuwa hapana ajuaye Ghaybu isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake.

Mwenyezi Mungu anasema:

(( قُلْ لا يَعْلَمُ مَنْ فِي السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّهُ ))[النمل:65].

“Sema: ‘Hakuna aliyoko katika mbingu na ardhi ajuaye Ghayb ila Mwenyezi Mungu.”

An Naml-65

Na anasema:

(( وَعِنْدَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ))[الأنعام:59]

“Na ziko Kwake (Mwenyezi Mungu tu) funguo za siri (Ghayb) hakuna azijuaye ila Yeye tu.”

Al An-Am-59

Nani Sahaba – kilugha na kidini
Katika kamusi la lugha ya Kiarabu, neno ‘Sahaba’, maana yake ni Rafiki, Mwenzi wake, Sahibu nk.

Katika dini, neno ‘Sahaba’ maana yake ni Mwislamu aliyemuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), akamfuata na kumuamini na akafariki katika imani hiyo.

Na hii ina maana kuwa, yeyote aliyewahi kumouna Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) na asimuamini, basi hawezi kuingia katika maana ya neno ‘Sahaba’.

Nani Mnafiki – kilugha na kidini
Katika kamusi la lugha ya kiarabu, neno ‘Mnafiki’ maana yake ni mtu mwenye kigeugeu au mwenye kuwa na sura mbali mbali: Leo hivi kesho vile.

Katika dini, neno ‘Mnafiki’ maana yake ni yule anayejidhihirisha kuwa ni Muislam na kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), wakati undani wake ni kafiri na adui wa Mwenyezi Mungu na adui wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam).

Baada ya tafsiri hii fupi ya nani Sahaba na nani Mnafiki, tutakubaliana kuwa maneno hayo mawili hayawezi kuwa na maana moja, (hayawezi kwenda sambamba) Kilugha wala Kidini.

Kwa sababu Sahaba ni yule aliyemuamini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akafariki dunia akiwa Muislam, wakati Mnafiki ni mwenye kujidhihirisha kama ni Mwislam wakati ndani ya nafsi yake ni kafiri.

Kwa hivyo haiwezekani Sahaba akawa Mnafiki na wala Mnafiki hawezi akawa Sahaba.

Sasa Mtu anaweza kuuliza:

‘Vipi tutaweza kutofautisha baina ya Sahaba na Mnafiki?’

Majibu:

Mnafiki ana sifa na alama maalum tulizojulishwa katika Qurani na katika Mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), na kwa ajili hiyo tunaweza kutofautisha baina yake na Sahaba.

Wanafiki ni watu;

‘Wanaoeneza ufisadi ardhini, kuifanyia istihzai dini, kuwafanyia istihzai wacha Mungu, ni wavukaji mipaka katika kufanya maasi wenye kuununua upotofu (upotevu) kwa uongofu, wavivu katika kufanya ibada, hugeuka geuka, mara Waislamu mara makafiri, kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

مُّذَبْذَبِينَ بَيْنَ ذَلِكَ لاَ إِلَى هَـؤُلاء وَلاَ إِلَى هَـؤُلاء

“Wanayumba yumba baina ya huku (kwa Waislam) na huko (kwa makafiri). Huku hawako wala huko hawako)”.

Annisaa-143

Na katika sifa za wanafiki pia ni;

‘Kuwa hawamwamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Akhera na kwamba Waislam wanapopata kheri yoyote au mafanikio, wao wanahuzunika, na hufurahi pale Waislamu wanapopata tabu au wanapokumbwa na masaibu au mitihani.

Huchukizwa na kutoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu na hufurahi wanaporudi nyuma na kumuacha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) peke yake vitani.

Wameingia katika dini kwa ajili ya kujikinga wasiambiwe kuwa wao ni makafiri, na wanapenda kuwadhuru Waislam na kuwafarikisha. Na katika sifa za unafiki ni kuwa; wanaiahirisha swala mpaka nyakati zake za mwisho na hawahudhurii Swala za jamaa na kwamba wanaionea uzito kabisa Swala ya Alfajiri na ya Ishaa’.

Hizi ni baadhi tu ya sifa za Wanafiki alizozitaja Mwenyezi Mungu katika Qurani tukufu, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) katika mafundisho yake.

Bila shaka Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ni watu walio mbali kabisa na sifa hizi. Hawa ambao Mwenyezi Mungu Amewaambia:

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللّهِ

“Nyinyi ndio umma bora kuliko umma zote zilizodhihirishiwa watu (ulimwenguni) mnaamrisha yaliyo mema na mnakataza yaliyo maovu, na mnamwamini Mwenyezi Mungu”.

Aali Imran- 110

Na Akasema juu yao:

يا أيها النبي حسبك الله ومن اتبعك من المؤمنين

“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mwenyezi Mungu anakutoshelezea wewe na wale walokufuata katika hao walioamini”.

Al Anfal-64

Na Akasema juu yao:

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّهِ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاء عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاء بَيْنَهُمْ تَرَاهُمْ رُكَّعاً سُجَّداً يَبْتَغُونَ فَضْلاً مِّنَ اللَّهِ وَرِضْوَاناً

“Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye ni wenye nyoyo thabiti mbele ya makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama kwa kurukuu na kusujudu (pamoja), wakitafuta fadhila za Mwenyezi Mungu na radhi (yake).”

Al Fat-h- 29

Na Akasema:

وَالَّذِينَ آمَنُواْ وَهَاجَرُواْ وَجَاهَدُواْ فِي سَبِيلِ اللّهِ وَالَّذِينَ آوَواْ وَّنَصَرُواْ أُولَـئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقّاً لَّهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ

“Na wale walioamini wakahama (kuja Madina) na wakaipigania dini ya Mwenyezi Mungu (Nao ni Muhajir); na wale waliowapa (Muhajir) mahala pa kukaa na wakainusuru dini (ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake).(nao ni Ansar) Hao ndio Waislam wa kweli. Watapata msamaha (wa Mwenyezi Mungu) na kuruzukiwa kuzuri (kabisa huko Akhera)”.

Al Anfal – 74.

Masahaba wa Makka (Radhiya Llahu anhum) ndio walioamini, wakahama, na wakapigana jihadi. Na Masahaba wa Madina (Radhiya Llahu anhum) ndio waliowapa mahala pa kukaa na wakainusuru dini.

Baada ya maelezo haya kutoka kwa Muumba wa mbingu na ardhi, asije mtu akatuambia kuwa Masahaba na wanafiki ni kitu kimoja. Hakika haya ni matusi makubwa kabisa!

Hawawezi kuwa wanafiki watu ambao Mwenyezi Mungu Amesema juu yao; “Nyinyi ndio umma bora kuliko umma zote zilizodhihirishiwa watu (ulimwenguni).”

Hawawezi kuwa wanafiki watu ambao Mwenyezi Mungu Ameshuhudia kuwa ni “Wenye nyoyo thabiti mbele ya makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama kwa kurukuu na kusujudu (pamoja), wakitafuta fadhila za Mwenyezi Mungu na radhi (yake).”

Hawawezi kuwa wanafiki watu ambao Mwenyezi Mungu Mwenyewe Anashuhudia kuwa “Hao ndio Waislam wa kweli.”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alisema:

“لا تَسُبّوا أَصْحَابِي، فَوَالّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَوْ أَنّ أَحَدَكُمْ أَنْفَقَ مِثْلَ أُحِدٍ ذَهَباً مَا أَدْرَكَ مُدّ أَحَدِهِمْ وَلاَ نَصِيفَهُ”.

“Msiwatukane Sahaba wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, hata mmoja wenu atajitolea katika njia ya MwenyeziMungu kugawa dhahabu ukubwa wake mfano wa jabali Uhud, basi hatofikia gao lao wala hata nusu ya gao lao”.

Bukhari na Muslim

Na akasema:

من سب أصحابي فعليه لعنة الله والملائكة والناس أجمعين

“Atakayewatukana Masahaba wangu, basi itampata laana ya Mwenyezi Mungu na (laana ya) Malaika na (laana ya) watu wote”.

((Attabariy, katika ‘Al Kabeer’, Abi Naeem katika ‘Al Hiliya’ na Abi Asim, na hadithi hii pia inapatikana katika ‘Silsila za hadithi sahihi kilichoandikwa na Sheikh Al Albani)).

Na akasema (Swallah Llahu alayhi wa sallam):

“Nihifadhieni Masahaba wangu, kisha wale waliowafuatilia kisha wale waliofuatilia”.

Imam Ahmad, Ibni Majah, na Al Haakim.

Ikiwa Masahaba waliokuwa wengi wanatuhumiwa kuwa ni watu wenye kigeugeu na unafiki, hii italeta maana kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) hakuweza kuwalea na kuwafundishsa vizuri Masahaba wake (Radhiya Llahu anhum) wakaijuwa haki, na kwamba yeye ni mlezi asiyefanikiwa, aliyeshindwa kuifanya kazi yake ya kuwalea Masahaba (Radhiya Llahu anhum).

Haikubaliki akilini abadan kuwa baada ya kuishi nao muda mrefu wote huo alifanikiwa kuwalea na kuwafundisha Masahaba watatu tu au wasiozidi saba?

Kila anayesoma na kuidurusu sira (historia) ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), anaelewa kwamba wakati Waislam walipokuwa Makka hapakuwa na unafiki, na hii ni kwa ajili ya adhabu kali walizokuwa wakipata waliosilimu wakati ule. Na inajulikana pia kwamba unafiki ulianza kujitokeza baada ya Waislam kuhamia Madina, na baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kupata nguvu, na dini ya Mwenyezi Mungu kuanza kutambulika kila mahala.

Na inaeleweka pia kwa kila mwenye kuidurusu sira ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kuwa Abubakar, Umar na Uthman na wengineo ni miongoni mwa Masahaba walioingia katika dini ya Mwenyezi Mungu tokea siku za mwanzo, wakapata tabu na shida kama walivyopata wenzao, na hii ni dalili wazi kuwa walikuwa mbali na sifa ya unafiki.

Mwenyezi Mungu amewafedhehesha wanafiki kwa kuwateremshia Suratul Munafiqun na At Tawba; akaelezea ndani ya sura hizo juu ya hali zao na vitimbi vyao; na akatuelezea yale yaliyofichika nyoyoni mwao katika kuwachukia Waislam, na ndiyo maana Surat at Tawba ikaitwa ‘Sura ya Kufedhehesha’. Katika sura hiyo Mwenyezi Mungu alitaja pia sifa za Masahaba (Radhiya Llahu anhum) na akatujulisha kuridhika kwake nao. Na huu ni ushahidi utokao Kwake Subhanahu wa Taala.

Ama Suratul Munafiqun, hii imeteremshwa kwa ajili ya kutujulisha juu ya mkubwa wa wanafiki na kiongozi wao aitwae Abdillahi bin Ubay bin Salool na wenzake.

Anasema Zayd bin Al Arqam (Radhiya Llahu anhu):

“Nilikuwa vitani, nikamsikia Abdillahi bin Ubay akisema:

“Msitoe mali kuwasaidia waliokuwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu mpaka watakapomwondokea pale alipo, na tutakaporudi Madina yule mtukufu (akimaanisha yeye Abdillahi bin Ubay ‘mkuu wa wanafiki’kuwa ni mtukufu) atamtoa (katika mji wa Madina) yule aliyedhalilika (akimaanisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam kuwa eti ndiye aliyedhalilika)”.

Nikamhadithia ami yangu hayo niliyoyasikia (au Umar) naye akamhadithia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam): Akaniita na mimi nikamhadithia. Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamtuma mtu amuite Abdillahi bin Ubay pamoja na wenzake, wakaapa na kukanusha yale waliyosema, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) hakunisadiki na akamsadiki yeye. Nikaona dhiki sijapata kuona mfano wake. Nikakaa nyumbani kwangu, lakini haujapita muda Mwenyezi Mungu akateremsha Suratul Munafiqun, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamtuma mtu aniite, akanisomea (Sura hiyo) kisha akaniambia:

“Mwenyezi Mungu amesadikisha maneno yako ewe Zeyd”.

Bukhari.

Tafsiri hii pia inapatikana katika kitabu cha tafsiri cha Mashia kiitwacho ‘Maj maa l bayan fiy tafsiyri l Quran’, kilichoandikwa na Imam Al Tubrusy ambaye ni miongoni mwa maulamaa wakubwa wa Kishia. Na katika kitabu hicho, ameelezea sababu ya kuteremshwa Suratul Munafiqun kuwa ni juu ya Abdillahi bin Ubay ‘mnafiki’ na wenzake …..

(Maj maa l bayan fiy tafsiyr l Qur an ukurasa 85)

Kisha Mwanachuoni huyu wa Kishia akazitaja riwaya zile zile alizozielezea Imam Bukhari zinazothibitisha hoja hiyo.

Inajulikana wazi kuwa Abdillahi bin Ubay pamoja na wafuasi wake walikuwa wakijulikana na Masahaba wote (Radhiya Llahu anhum) kuwa ni wanafiki, na mtu yeyote anaposoma Surat at Tawba ataona kuwa sura hiyo imeelezea juu ya vituko mbali mbali walivyokuwa wakivifanya wanafiki hao kiasi ambapo ilikuwa ikijulikana wazi mbele ya kila mtu kuwa wao ndio waliokusudiwa.

Kwa mfano kuanzia aya ya 44 hadi 49 ya sura hiyo Mwenyezi Mungu anasema:

لاَ يَسْتَأْذِنُكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ أَن يُجَاهِدُواْ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ وَاللّهُ عَلِيمٌ بِالْمُتَّقِينَ {44} إِنَّمَا يَسْتَأْذِنُكَ الَّذِينَ لاَ يُؤْمِنُونَ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ وَارْتَابَتْ قُلُوبُهُمْ فَهُمْ فِي رَيْبِهِمْ يَتَرَدَّدُونَ {45} وَلَوْ أَرَادُواْ الْخُرُوجَ لأَعَدُّواْ لَهُ عُدَّةً وَلَـكِن كَرِهَ اللّهُ انبِعَاثَهُمْ فَثَبَّطَهُمْ وَقِيلَ اقْعُدُواْ مَعَ الْقَاعِدِينَ {46} لَوْ خَرَجُواْ فِيكُم مَّا زَادُوكُمْ إِلاَّ خَبَالاً ولأَوْضَعُواْ خِلاَلَكُمْ يَبْغُونَكُمُ الْفِتْنَةَ وَفِيكُمْ سَمَّاعُونَ لَهُمْ وَاللّهُ عَلِيمٌ بِالظَّالِمِينَ {47}‏ لَقَدِ ابْتَغَوُاْ الْفِتْنَةَ مِن قَبْلُ وَقَلَّبُواْ لَكَ الأُمُورَ حَتَّى جَاء الْحَقُّ وَظَهَرَ أَمْرُ اللّهِ وَهُمْ كَارِهُونَ {48} وَمِنْهُم مَّن يَقُولُ ائْذَن لِّي وَلاَ تَفْتِنِّي أَلاَ فِي الْفِتْنَةِ

سَقَطُواْ وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمُحِيطَةٌ بِالْكَافِرِينَ {49}

“Hawatakuomba ruhusa wale wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, wasende kupigana Jihadi kwa mali yao na nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwajua wachaMungu.

Wasio muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na nyoyo zao zikatia shaka, hao tu ndio wanao kutaka ruhusa. Basi hao wanataradadi katika shaka zao.

Na ingeli kuwa kweli walitaka kutoka bila ya shaka wangeli jiandalia maandalio, lakini Mwenyezi Mungu kachukia kutoka kwao, na kwa hivyo akawazuia na ikasemwa: Kaeni pamoja na wanao kaa!

Lau wangeli toka nanyi wasingeli kuzidishieni ila mchafuko, na wange tanga tanga kati yenu kukutilieni fitna. Na miongoni mwenu wapo wanao wasikiliza. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhaalimu.

Tangu zamani walitaka kukutilieni fitna, na wakakupindulia mambo juu chini, mpaka ikaja Haki na ikadhihirika amri ya Mwenyezi Mungu, na wao wamechukia”.

Na miongoni mwao wapo wanao sema: ‘Niruhusu wala usinitie katika fitina’. Kwa yakini wao hivyo wamekwisha tumbukia katika fitina. Na hakika Jahannamu imewazunguka.”

At Tawba – 44-49

Inaeleweka na kila mtu kuwa Masahaba wote walitoka kwenda vitani siku hiyo ya vita vya Tabuk (vita ambavyo aya hizo zinazungumzia juu yake), na waliobaki nyuma ni Aba Dhar na Aba Khaythamah (Radhiya Llahu anhum), kisha nao pia wakenda kujiunga na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) pamoja na wenzao, na walikutana nao njiani kabla ya kuwasili uwanja wa vita.

Na ineleweka pia kuwa miongoni mwa waliobaki nyuma ni Kaab bin Malik, Hilal bin Umayyah na Mirara bin Rabia (Radhiya Llahu anhum), nao ni katika watu wa Madina na inajulikana na kila mtu kuwa Mwenyezi Mungu aliwasamehe Masahaba hao kama ilivyoelezwa katika kisa cha ‘Wale watatu waliongojeshwa’.

Ama wengine waliobaki Madina wasiende vitani walikuwa wakijulikana kuwa ni katika wale wanafiki waliomuendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kuomba udhuru wa uongo, au wale waliokuwa na udhuru wa kutopigana Jihad kwa ajili ya ugonjwa au udhuru mwingine unaokubalika.

Na haya tulieleza hapo mwanzo katika kisa cha Kaab (Radhiya Llahu anhu) kuwa katika waliobaki pale Madina wasende vitani hakuwa akimuona aliye kufu yake isipokuwa wenye udhuru au wale waliokuwa wakijulikana kuwa ni Wanafiki.

Na hii ni dalili kuwa wanafiki walikuwa wakijulikana na Masahaba.

Na katika sura hiyo hiyo ya At Tawba, Mwenyezi Mungu Anatujulisha kuridhika kwake na Masahaba waliotangulia kuingia katika Uislamu miongoni mwa Wahajir (watu wa Makka waliohamia Madina) na Ansaar (Watu wa Madina waliowapokea Wahajir wa Makka) na akawatayarishia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele.

Mwenyezi Mungu anasema:

وَالسَّابِقُونَ الأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللّهُ عَنْهُمْ وَرَضُواْ عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَداً ذَلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Na wale walio tangulia, wa kwanza, katika Wahajiri na Ansari, na walio wafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao wameridhika naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”

At Tawba 100

Sasa tizameni ndugu zangu, vipi Mwenyezi Mungu anatuelezea juu ya kuridhika kwake na Masahaba katika Muhajir na Ansar kinyume na wanavyotuhumiwa unafiki, na kwamba walirudi nyuma na kukufuru, akiwemo mbora wa Masahaba wote Abubakar Al Siddique (Radhiya Llahu anhu).

Sisi tunaridhika na wote alioridhika nao Mwenyezi Mungu, na tunawafanyia uadui maadui wote wa Mwenyezi Mungu, na tunafuata yale tuliyofundishwa na Mwenyezi Mungu pamoja na mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu wake (Swalla Llahu alayhi wa sallam).

Mwenyezi Mungu anasema:

لَقَد تَّابَ الله عَلَى النَّبِيِّ وَالْمُهَاجِرِينَ وَالأَنصَارِ الَّذِينَ اتَّبَعُوهُ فِي سَاعَةِ الْعُسْرَةِ مِن بَعْدِ مَا كَادَ يَزِيغُ قُلُوبُ فَرِيقٍ مِّنْهُمْ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ إِنَّهُ بِهِمْ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ {117}‏

“Mwenyezi Mungu amekwisha pokea toba ya Nabii na Wahajiri na Ansari walio mfuata katika saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia nyoyo za baadhi yao kugeuka. Basi akapokea toba yao, kwani hakika Yeye kwao wao ni Mpole na ni Mwenye kuwarehemu.”

Attawba 117

Mwenyezi Mungu ni mpole kwao na anawarehemu na ameridhika nao na anawasifia namna walivyosimama pamoja na Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) katika saa ile ya dhiki (vita vya Tabuk), na huu ni ushahidi utokao kwa Mwenyezi Mungu Asiye mshirika.

Utayakuta haya pia katika vitabu vya wanavyuoni wakubwa wa Kishia (Ithnaasheri) waliotamka ukweli ndani ya baadhi ya vitabu vyao vinavyotambulika.

Tafsiri ya Al Iyashi
Anasema Abu Nasr Muhammad bin Masaud, anayejulikana kwa jina la ‘Al Iyashi’ katika tafsiri yake juu ya kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

إِنَّ اللّهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِين

“Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubu na huwapenda wanaojitakasa.’

Al Baqarah – 222

Alisema:

“Kutoka kwa Salaam anasema: ‘Nilikuwa kwa Abu Jaafar (Muhammad Al Baqer Alayhi ssalaam- Imam wa tano kwa Shia) akaingia Hamran bin Ayun na kumuuliza baadhi ya mambo, na alipotaka kuondoka, Ayun akamuuliza Abu Jaafar:

‘Tuelezee Mwenyezi Mungu akupe umri mrefu, sisi tunapokuwa nawe nyoyo zetu hulainika na nafsi zetu zinakuwa mbali na dunia, tunadharau kila kilichomo mikononi mwa watu katika mali, lakini tunapotoka na kuchanganyika na watu na kufanya biashara, tunaanza kuipenda tena dunia.’

Abu Jaafar akasema:

“Nyoyo zinashindwa na mambo baadhi ya wakati, na wakati mwengine mambo yanakuwa mepesi.’ Kisha Abu Jaafar (Alayhi ssalaam) akaendelea kusema: ‘Kwa hakika Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu walisema:

‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, tunajiogopea unafiki’ akasema: “Kwa nini mnaogopa?”

Wakasema:

“Sisi tunapokuwa nawe ukatukumbusha, huwa na uoga, na nyoyo zetu zinalainika tukaisahau dunia, hatuitamani, hata hufikia kuwa tunaiona akhera Pepo na Moto mbele yetu. Lakini mara tunapotoka kwako na kuingia majumbani mwetu na kuanza kuwabusu watoto wetu na kuonana na wake zetu na mali zetu, tunaanza kubadilika hali zetu kinyume na pale tunapokuwa nawe, kama kwamba hatukuwa na kitu. Je! Hutuogopei unafiki?”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akawaambia:

“Kabisa sikuogopeeni hilo, kwani hizi ni katika hatua za shetani akijaribu kukupendezesheni dunia, Wallahi lau kama mungebaki katika hali ile mliyokuwa nayo pale mlipokuwa nami, basi Malaika wangekusalimieni majiani na mungekuwa mnatembea juu ya maji, na kama mungelikuwa hamtendi madhambi na kumuomba Maghfira Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu angeliumba viumbe vingine ili wafanye madhambi kisha wamuombe maghfira ili apate kuwaghufiria, kwani Muislam siku zote yupo katika mtihani, hukuisikia kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

إِنَّ اللّهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ

‘Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubu?’

na isemayo:

وَأَنِ اسْتَغْفِرُواْ رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُواْ إِلَيْهِ

“Na ili muombe msamaha kwa Mola wenu kisha mtubie (mrejee)?”

Hud 3

(Tafsir Al Iyashi Juz1 uk.128)

Katika riwaya hii, anatubainishia Al Iyashi katika tafsiri yake kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ameshuhudia kuwa hawaogopei Sahaba zake unafiki. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hasemi kwa matamanio ya nafsi yake.

Kwa hivyo mwenye kumuita Sahaba yeyote kuwa ni mnafiki, mtu huyo atakuwa ana moja katika mawili:-

1- Ama anakwenda kinyume na mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

2- Au anajua zaidi kupita Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Ikiwa tunautaka umoja wa Waislamu kikweli na kuiondoa chuki iliyopo, basi nawaomba ndugu zetu Mashia waache kuwakufurisha Masahaba au kuwaita wanafiki na kuwaapiza, na badala yake tumfanye Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwa ni ruwaza njema kwetu, kuwa ni mfano mwema kwetu wa kuigwa, na tuwapende kama alivyokuwa akiwapenda Swallah Llahu alayhi wa sallam.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akiwapenda Swahaba zake (Radhiya Llahu anhum). Na watu wa nyumba yake ‘Ahlul Bayt’ (Radhiya Llahu anhum) nao pia walikuwa wakiwapenda Maswahaba (Radhiya Llahu anhum), na Maswahaba nao walikuwa wakiwapenda Ahlul Bayt.

Huyu hapa Imam Al Hassan Al Askari, ambaye ni Imam wa kumi na moja wa Shia alipokuwa akiwafahamisha watu daraja ya Masahaba (Radhiya Llahu anhum) mbele ya Mwenyezi Mungu alisema:

‘Miongoni wa masuala aliyouliza Musa (Alayhi Ssalaam) kumuuliza Mwenyezi Mungu alisema:

‘Wapo Masahaba wa Mtume yeyote wa Mwenyezi Mungu walio bora kuliko Masahaba wangu?’

Mwenyezi Mungu akamjibu:

“Ewe Musa kwani hujui kuwa ubora wa Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad juu ya Masahaba wa Mitume yote ni sawa na ubora wa watu wa nyumba ya Muhammad juu ya watu wa nyumba za Mitume yote, na mfano wa ubora wa Muhammad juu ya Mitume yote?”

Tafsiri ya Al Hassan Al Askary uk.11(Tafsiri ya Surat Al Baqarah

Ndani ya kitabu kitukufu kwa Shia kiitwacho ‘Nahaj al Balaghah’, Sharhi ya Muhammad Abdo Uk. 225, imeandikwa kua Imam Aly alisema:

“Nimewaona Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam), na sioni yeyote kati yenu aliyeshabihiana nao. Walikuwa wakati wa asubuhi utawaona nywele zimetimka kwa sababu ya kusimama kwao usiku kucha wakisujudu na kusimama (kwa kuswali), wanaomba huku wakisujudu, na wanapolala, na wanapokumbuka akhera yao utawaona wanasimama kama kwamba wamesimamia makaa ya moto. Na anapotajwa Allah basi macho yao yanatoa machozi mpaka nyuso zao zinaroa, na wanainamisha vichwa vyao chini mfano wa miti iliyopinda kwa upepo mkali wa kimbunga kwa kuhofia adhabu na kutarajia thawabu”.

Ama Ibarahim Al Thaqafi ambaye ni katika maulamaa wakubwa wa Shia, katika kitabu chake kiitwacho ‘Al Ghaaraat’ Juzuu ya 1 Uk.177 akimnukuu Aly (Radhiya Llahu anhu):

“Aliulizwa Aly: ‘Ewe Amiri wa Waislam, tuelezee juu ya Sahibu zako.’

Akauliza:

“Juu ya sahibu zangu wepi?”

Wakamwambia:

“Juu ya Sahaba wa Muhammad (Swalla Llahu alayhi wa sallam).”

Akasema:

“Masahaba wa Muhammad wote ni sahibu zangu”.

Tunamuomba msomaji arudie marejeo yote tuliyonukuu kutoka katika Qurani tukufu na kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na kutoka kwa maulamaa wa pande zote mbili ili imbainikie heshima ya Masahaba hawa wakiwemo Makhalifa watatu wa mwanzo wa Waislam mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na mbele ya maulamaa waliotangulia wa pande zote mble, kisha ajiulize; ni kwa maslahi ya nani mtu anaweza kuthubutu kuwatukana au kuwazulia uongo na kuwawekea vikao vya kila mwaka kuwalani na kuapa juu ya kulipa visasi.

Bali hata Sayiduna Al-Husayn (Radhiya Llahu anhu) alikuwa katika nchi ya Constantinople akipigana jihadi, na wakati huo Mu’awiyah (Radhiya Llahu anhu) ndiye aliyekuwa Khalifa wa Waislamu. Kwa hivyo Masahaba na Watu wa Nyumba ya Mtume (Radhiya Llahu anhum) walikuwa wakishirikiana na kupendana na kunasibiana na walikuwa pamoja katika jihadi yao dhidi ya maadui wa Uislamu.

Siku moja kundi la watu lilikwenda kwa Imam Aly Zeinul Abideen (Radhiya Llahu anhu) na walikuwa wakiwasema vibaya Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam); Abubakar, Umar na Uthman (Radhiya Llahu anhum).

Aly Zeinul Abideen (Radhiya Llahu anhu) akawauliza:

“Kwanza nielezeni ni nani nyinyi? Nyinyi ni katika wale Wahajir (Watu wa Makka) waliohama mwanzo waliotolewa majumbani mwao na katika mali zao wakitaka fadhila za Mwenyezi Mungu na radhi zake na wakamnusuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake?”

الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيارِهِمْ وَأَمْوَالِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلاً مِّنَ اللَّهِ وَرِضْوَاناً وَيَنصُرُونَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ

Al Hashr -8

Wote kwa pamoja wakasema: “La, sisi si katika hao”

Akawauliza tena:

“Basi nyinyi ni katika watu waliofanya maskani yao hapa (Madina) na wakautakasa Uislamu (wao barabara) kabla ya (kuja ) hao (Muhajirin) na wakawapenda hao waliohamia kwao”.

وَالَّذِينَ تَبَوَّؤُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ

Al Hashr -9

Wakajibu:

“La! Sisi si katika hao”

Kisha Imam Aly Zeinul Abideen (Radhiya Llahu anhu) akawaambia:

“Nyinyi wenyewe mumeshuhudia kuwa si katika hawa wala si katika wale. Basi na mimi ninashuhudia pia kuwa nyinyi si katika kundi lile la tatu ambalo Mwenyezi Mungu Amesema juu yao:

وَالَّذِينَ جَاؤُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلّاً لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na Waliokuja baada yao (wakawa wanapendana na Waislamu waliotangulia wanawaombea dua) wanasema; ‘”Mola wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu waliotutangulia (kufa) katika Uislamu. Wala usijaaliye katika nyoyo zetu undani kuwafanyia Waislamu (wenzetu). Mola wetu! Hakika Wewe ni Mpole sana, Mwenye Rehema mno”.

Al Hashr – 10

Katika aya hizi Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa watu wa Makka waliacha majumba yao na mali zao na watu wao kwa ajili ya kutaka fadhila za Mwenyezi Mungu na radhi zake, na kwa ajili ya kumnusuru Mwenyezi Mungu na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na akashuhudia kuwa ni wakweli.

Na Mwenyezi Mungu anashuhudia pia watu wa Madina waliutakasa Uislamu baraabara, juu ya kuwa walifikiwa na wageni wazito na hawakuwa na mali ya kutosha, waliwapokea wageni hao kwa moyo mkunjufu, wakahiari kujinyima wao kwa ajili ya kuwakirimu wageni.

Kisha Mwenyezi Mungu Akatuamrisha tuliokuja baada yao kuwaombea maghfira na akatutaka tusijaaliye ndani ya nyoyo zet undani wowote juu yao.

Imepokelewa kutoka kwa Yahya bin Kathiyr kutoka kwa Jaafar bin Muhammad bin Aly bin Al Hussayn kutoka kwa baba yake ((Radhiya Llahu anhum) kuwa amesema:

« Alikuja mtu kwa baba yangu akamuambia : ‘Nihadithie juu ya Abubakar.’ Akasema: ‘Unauliza juu ya Al Siddique.’ Akasema yule mtu : ‘Mwenyezi Mungu akurehemu, na wewe pia unamuita Al Siddique ?’ Akamuambia : ‘Akukose mama yako wewe. Ameitwa As Siddique na aliye bora kupita mimi na wewe, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na Watu wa Makkah na watu wa Madina. Asiyemuita kwa jina la Al Siddique basi Mwenyezi Mungu hatosadiki kauli yake duniani wala akhera. Nenda, tena umpende Abubakar na Umar.»

Imeandikwa katika Nahj Al Balaghah pia kuwa Aly (Radhiya Llahu anhu) alimuandikia Muawiyah bin Abi Sufiyan (Radhiya Llahu anhu) akimuambia:

Kwa Muawiyah:

“Bisimillahi Rahmaani Rahiym,

Amma baad, kwa vile watu wote wamefungamana nami katika mji wa Madina, basi nawe pia uliyeko huko Sham (Syria) unalazimika kufungamana nami. Na hii ni kwa sababu watu waliofungamana nami ni wale wale waliofungamana na Abubakar na Umar na Uthmaan. Kwa hivyo aliyehudhuria hana haki ya kulikataa na asiyehudhuria hana haki ya kulipinga. Kwa hakika ushauri ni wa Muhaajirin na Answaar (Watu wa Makkah na wa Madina). Wanapokubaliana wote juu ya mtu na kumchagua kuwa Imam wao, na Mwenyezi Mungu Anaridhika na uchaguzi wao.

Nimemtuma kwako Jariyr, naye ni katika watu wa Imani na watu waliohajir, kwa hivyo fungamana nami – Walaa quwwata illa billaah!!”.

Nahjul-Balaaghah- uk. 427 mlango wa 6

Subhanallah! Huyu hapa Aly (Radhiya Llahu anhu) anakiri mwenyewe kuwa hapana mwenye haki ya kupinga uchaguzi wa watu wa Makka na wa Madina na kwamba Mwenyezi Mungu ameridhika na kuchaguliwa kwa Abubakar na Umar na Aly (Radhiya Llahu anhum) kwa sababu wote wamechaguliwa kwa njia hiyo.

Kuoleana
Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ameoa mabinti wa Abubakar na Umar. Na Uthman alioa mabinti wawili wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), Mabibi Ruqayya na Ummu Kulthum, na alijulikana kwa jina la ‘Dhiy Nnurayn’, na maana yake ni Mwenye Nuru mbili kwa sababu ya mabinti hao wawili (Radhiya Llahu anhum).

Alihuzunika sana alipofariki mkewe wa pili Bibi Ummu Kulthum (Radhiya Llahu anha) na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipomuona katika hali ile akamuuliza:

“Kipi kinachokuliza ewe Uthman?”

Uthman akajibu:

“Ninalia ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa sababu kumekatika kunasibiana kwangu na wewe.”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:

“Usilie ewe Uthman, naapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, lau kama nina mabinti mia wanakufa mmoja baada ya mwengine, basi ningekuozesha mpaka wasibaki katika mia hao hata mmoja.”

Attabarani na wengine

Hii ni katika dalili za mapenzi makubwa yaliyokuwepo baina ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) pamoja na watu wa nyumba yake juu ya Masahaba (Radhiya Llahu anhum).

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alimuoa Bibi Aisha binti wa Abubakar Al Siddiquqe na alimuoa Hafsa binti wa Umar bin Khatab na alimuoa pia Ummu Habiybah Ramlah binti Abu Sufyan (Radhiya Llahu anhum).

Aly (Radhiya Llahu anhu) alimuozesha binti yake Ummu Kulthum kwa Umar bin Khatab.

(Al Kafi/346/5)

Alipouliwa Jaafar bin Abi Talib (Radhiya Llahu anhu), mkewe Asmaa binti Umays (Radhiya Llahu anha) aliolewa na Abubakar Al Siddique na alipofariki Abubakar (Radhiya Llahu anhu), Bibi Asmaa aliolewa na Aly bin Abu Talib (Radhiya Llahu anhu).

Jaafar Assadiq ni mjukuu wa Abubakar As Siddique, kwa sababu Muhammad Al Baqer mjukuu wa Al Hussain alimuoa Um Farwah mjukuu wa Muhammad bin Abubakar, na kutokana na ndoa hiyo akapatikana Jaafar As Sadiq. Kwa hivyo Jaafar ni mjukuu wa Abubakar na mwanawe Musa Al Kadhim anakuwa pia mtoto wa mjukuu wa Abubakar na kwa njia hii Maimam wote waliofuata wa Shia ni wajukuu wa Abubakar Al Siddique (Radhiya Llahu anhum jamiy’an)

Imepokelewa kuwa Jaafar Al Sadeq alikuwa akisema:

“Amenizaa Abubakar mara mbili.”

Siyar aalam al Nubalaa

Abaad bin Uthman bin Affan alimuoa Ummu Kulthum binti yake Abdullah bin Jaafar bin Abi Talib.

Shia wa Ahlul Bayt/141

Sakina binti Al Hussayn bin Aly bin Abi Talib aliolewa na Masaab bin Al Zubair bin Al Awaam.

Tabaqaat ibn Saad183/5

(Mwenyezi Mungu awe radhi nao wote)

Majina ya watoto

Aly bin Abi Talib aliwapa wanawe majina ya Abubakar na Umar na Uthman.

Kashf al Ghumah 2/67

Al Hassan bin Aly alimpa mmoja wa watoto wake jina la Abubakar.

Kashf al Ghumah 2/198

Musa bin Jaafar alikuwa na watoto aliowapa majina ya Aisha na Umar.

Kashf al Ghumah 3/29

Wajibu wetu
Itakuwa siku ya furaha kubwa tutakapowaona wafuasi wa Sunni wakipeana mikono na wafuasi wa Shia kwa furaha bila kinyongo wala undani. Lakini hatuwezi kulifikia lengo hilo ikiwa Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) wataendelea kutukanwa na kukashifiwa na kulaaniwa.

Hatuwezi kulifikia ikiwa watu wataendelea kulizuru kaburi la Majusi Abu Lulua aliyemuua Khalifa wa Waislamu na Sahibu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) Umar bin Khataab (Radhiya Llahu anhu) na kuliita kaburi la Majusi huyo ‘Babu Shujaa ddiyn’ ‘Mlango wa shujaa wa dini.’

Dini gani wakati mtu huyu hakuwa Muislamu? Kwa nini wanakubali kuisherehekea siku ambayo Mmajusi aliyekuwa akiabudu moto alimuuwa Khalifa wa Wasilamu?

Narudia mwito wa Sheikh Al Qaradhawi aliposema : «Enyi viongozi wa Shia wenye akili na hekima, upigeni vita mnasaba huu kwa ajili ya umoja wa Waislamu. Inatosha jamani kueneza chuki kwa mambo yaliyotokea miama 1500 iliyopita.»

Msisahau kuwa Umar huyu ni ami yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amemuowa bini yake Hafsa (Radhiya Llahu anha), na Umar huyu huyu ni mume wa Ummu Kulthum binti Aly bin Abi Talib (Radhiya Llahu anhu).

Nilifurahi sana nilipomskia Dr. Sabah Al Khuzaiy katika channel Al Mustaqillah, na huyu ni mtaalamu anayesomesha katika mojawapo ya Vyuo vikuu huko Uingereza, na ni mfuasi wa madhehebu ya Shia.

Anasema Dr. Khuzaiy:

«Sielewi kwa nini viongozi wetu wa Shia wanashadidia sana jambo hili la kufanya matanga kila mwaka wakidai kuwa hiyo ni siku aliyouliwa Bibi Fatima (Alayhas Salaam) binti wa Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na ndani ya matanga hayo wanalaaniwa Masahaba wakubwa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hasa Makhalifa wawili wa mwanzo, Abubakar na Umar (Radhiya Llahu anhum).

Mimi siamini kuwa Umar wala Abubakar walimshambulia Bibi Fatima! Haya yote ni uzushi mtupu uliotungwa na watu wasioitakia kheri dini yetu, na baadhi ya watu wakausadiki uongo huo na kuueneza.

Inaingia akilini jamani kwa watu hawa waliosifiwa ndani ya Qurani tukufu na katika hadithi mbali mbali za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na huyu Abubakar aliyeruhusiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kusalisha wiki nzima ya mwisho kabla ya kufariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akimtizama huku akitabasamu, na hii ni dalili ya kuridhika naye.

Na Umar ambaye Aly (Alayhis Salaam) alikubali kumuozesha binti yake Ummu Kulthum. Kama kweli Umar ndiyo sababu ya kufariki kwa Bibi Fatima (Alayhas Salaam) wangelikubali kumuozesha binti yao mtu katili ?

Hadithi sahihi kwa pande zote mbili Shia na Sunni inasema:

« Atakapokujieni mtakayeridhika na dini yake na khulka zake muozesheni. »

Bila shaka Aly na Fatima (Alyhimussalaam) waliridhika na dini ya Umar ndiyo maana wakakubali kumuozesha binti yao.

Hivyo Aly huyu aliyepigana vita vya Khaybar kwa ushujaa mkubwa akapambana na Amr ibni Abdi Wudd wakati Masahaba wengine walihofia kupambana naye, leo Aly huyu avunjiwe heshima ya mke wake kisha anyamaze kimya ? Isitoshe ampe tunza muovu huyo ya kukubali kumuozesha binti yake?

Mimi, » aliendelea kusema Dr. Al Khuzaiy : «Ni Shia wa Aly yule shujaa aliyeuvunja mlango wa Khaybar, nilikuwa pamoja naye siku ile, na nilikuwa pamoja na Aly siku ile alipokubali kuswali nyuma ya Abubakar wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipokuwa akiumwa maradhi yake ya mwisho. Nilikuwa na Aly siku ile alipochaguliwa Abubakar kuwa Khalifa wa Waislamu na Aly akamkubali na akaswali nyuma yake, na nilikuwa pamoja na Aly siku ile alipokubali kuswali nyuma ya Umar bin Khattab baada ya kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Waislamu. Na nilikuwa pamoja na Aly siku ile Abdul Rahman bin Auf alipowashauri Waislamu juu ya nani awaongoze, nusu yao walimchagua Uthman na nusu nyingine walimchagua Aly. Mimi siku ile nilikuwa pamoja na Aly.

Na nilikuwa pamoja na Aly pia siku ile alipokubali kuswali nyuma ya Uthman baada ya kuchaguliwa Khalifa wa Waislamu, na maisha yangu yote nitakuwa pamoja na Aly mpaka siku ya Kiama. Lakini siwakufurishi Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) wala wake zake wala sikubali mtu yeyote awaseme vibaya watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Mimi naamini kuwa Bibi Fatima (Alayhassalaam) alikwenda kweli kwa Abubakar (Radhiya Llahu anhu) akidai ardhi ya Fadak na baada ya kufahamishwa hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwa Mitume hawarithiwi akaridhika, juu ya kukasirika kwake kidogo.

Na Abubakar (Radhiya Llahu anhu) alipomuendea nyumbani kumuomba radhi Fatima (Alayhassalaam) alikubali bila kinyongo. »

Mwisho wa maneno ya Al Khuzaiy

Hadithi hii ya Mitume kutorithiwa ni sahihi na imo ndani ya vitabu vinavayotegemewa vya Shia na Sunni.

Imesimuliwa na Al Kulayni katika kitabu chake maarufu ‘Al Kafi’ kuwa:

“Abu Abdillah (Imam Jaafar as Sadiq) amesema:

“Na hakika maulamaa ni warithi wa Mitume. Na hakika Mitume hawarithiwi Dinari wala Dirham, bali wao wanarithiwa elimu, kwa hivyo atakayeipata elimu hiyo amepata bahati kubwa”

Al Kafi 1/42.

Imam Muhammed Baqer al Majlisi katika kitabu chake kiitwacho Mir’at al – Uqul 1/111 amesema kuwa hadithi hii ni sahihi.

Imam Khomeni ameiandika hadithi hii katika kitabu chake kiitwacho ‘Al Hukumah al Islamia’ (Serikali ya Kiislamu), na akaitumia kama ni ushahidi wa Wilayat al Faqih chini ya kichwa cha maneno; (Sahihat al Qaddah) aliposema:

“Amesema Ali bin Ibrahim kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Hammad bin Issa kutoka kwa Abdullah bin Maymun al Qaddah kuwa Abu Abdullah (Jaafar as Sadiq (Alayhi Ssalaam) amesema:

“Atakayefuata njia ya kutafuta elimu, basi Mwenyezi Mungu atamsahilishia njia ya Peponi. Na maulamaa ni warithi wa Mitume. Na Mitume hawarithiwi Dinari wala Dirham, bali wao wanarithiwa elimu, kwa hivyo atakayeipata elimu hiyo amepata bahati kubwa.”

Al Kafi, kitab fadhl Al Ilm, mlango wa Sifat al Ilm wa Fadhlihi, hadithi nambari 2

Na katika kitabu hicho hicho cha ‘Al Hukumah al Islamia’ ukurasa wa 133 Imam Khomeni ameiandika hadithi nyingine iliyopokelewa kwa njia ya Muhammad Yahya kutoka kwa Ahmad bin Muhammad bin Iysa kutoka kwa Muhammad bin Khalid kutoka kwa Abu Abdullah (Imam Jaafar as Sadiq (Alayhi Ssalaam) kuwa amesema:

“Hakika maulamaa ni warithi wa Mitume, na hii ni kwa sababu Mitume hawaachi Dirham wala Dinari kwa ajili ya kurithiwa, bali wao wanaacha maneno yao”.

Al Hukumat al Islamiyah uk. 133

Kutokana na yaliyotangulia tunamaliza kwa kusema kuwa;

Si haki kutoikubali hadithi hii ya Kutorithiwa kwa Mitume katika kadhia ya Fadak, na kuikubali katika kadhia ya Wilayat al Faqih, kama alivyoandika Imam Khomeni na kabla yake Majlisi.

Kwa nini tuzikubali kauli za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) pale tunapotaka na tuzikatae tusipotaka juu ya kujuwa kwetu kuwa kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) haiwezi kubadilishwa na kiumbe chochote kile.

Na hadithi hii imo pia katika vitabu vifuatavyo :-

Katika At Tahdhiyb ameandika At Tuwsi na katika Bihar al Anwaar ameandika Al Majlisi:

“Nilimuuliza Abu Abdullah (Alayhi Ssalaam) juu ya wanawake na haki zao katika urithi akasema:

“Wana haki zao katika thamani ya udongo na ujenzi na mbao na miti tu, ama ardhi na nyumba, wao hawana haki ya urithi (wowote ndani yake).”

Na kutoka kwa Muhammad bin Muslim kutoka kwa Abu Jaafar (Alayhi Ssalaam) kuwa amesema:

“Wanawake hawana haki ya kurithi ardhi wala nyumba”.

Na kutoka kwa Abdul Malik bin Aayun kuwa mmoja wa ma Imam alimwambia:

“Wanawake hawana haki ya urithi katika ardhi wala nyumba”.

Hitimisho
Kwa kumaliza, hatusemi kuwa Maswahaba (Radhiya Llahu ‘anhum) wamekingwa na kufanya makosa ‘Maasuwmiyn’ au ‘hawakosei’. Bali wao ni viumbe wanaokosea kama viumbe wengine. Tunachotaka na kusisitiza ni kuwanasihi ndugu zetu; ikiwa kweli wanautaka umoja wa Kiislamu, na wanapenda Waislamu waungane wawe kitu kimoja bila kujali madhehebu, basi waache kuwatukana na kuwalani na kuwadhalilisha na kuwafanyia chuki Maswahaba hawa waliotukuzwa na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala. Masawahaba walioibeba Qur-aan hii tukufu tuliyonayo majumbani mwetu na misikitini na kila mahali wakaifikisha kwetu na kuieneza kila pembe ya ulimwengu. Bila ya juhudi zao kubwa na kujitolea kwao mhanga kwa hali na mali, wakapigana jihadi dhidi ya maadui wa Mwenyezi Mungu, dini isingeweza kutufikia, na tungelibaki hadi leo tukisujudia moto na masanamu na mizimu.

Walipotawala, dola kubwa kubwa zilisalimu amri mbele ya majeshi yao, na ulimwengu wote ulikuwa chini ya amri yao.

Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala Anasema juu yao:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُواْ وَهَاجَرُواْ وَجَاهَدُواْ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللّهِ وَالَّذِينَ آوَواْ وَّنَصَرُواْ أُوْلَئِكَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاء بَعْضٍ وَالَّذِينَ آمَنُواْ وَلَمْ يُهَاجِرُواْ مَا لَكُم مِّن وَلاَيَتِهِم مِّن شَيْءٍ حَتَّى يُهَاجِرُواْ وَإِنِ اسْتَنصَرُوكُمْ فِي الدِّينِ فَعَلَيْكُمُ النَّصْرُ إِلاَّ عَلَى قَوْمٍ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُم مِّيثَاقٌ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿72﴾ وَالَّذينَ كَفَرُواْ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاء بَعْضٍ إِلاَّ تَفْعَلُوهُ تَكُن فِتْنَةٌ فِي الأَرْضِ وَفَسَادٌ كَبِيرٌ ﴿73﴾ وَالَّذِينَ آمَنُواْ وَهَاجَرُواْ وَجَاهَدُواْ فِي سَبِيلِ اللّهِ وَالَّذِينَ آوَواْ وَّنَصَرُواْ أُولَئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا لَّهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ

Hakika wale walio amini na wakahama na wakapigania Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao, na wale walio toa mahala pa kukaa, na wakanusuru, hao ni marafiki na walinzi wao kwa wao. Na wale walio amini lakini hawakuhama, nyinyi hamna waajibu wa ulinzi kwao hata kidogo mpaka wahame. Lakini wakiomba msaada kwenu katika Dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipo kuwa juu ya watu ambao yapo mapatano baina yenu na wao. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.

Na wale walio kufuru ni marafiki wenyewe kwa wenyewe. Msipo fanya hivi itakuwako fitna katika nchi na fisadi kubwa.

Na walio amini wakahama na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na walio toa mahala pa kukaa na wakanusuru, hao ndio Waumini wa kweli. Watapata msamaha wa Mwenyezi Mungu na kuruzukiwa kwema.

Al Anfal -72-74

Ndugu zangu Waislamu, aya hizi tukufu zinazungumza juu ya Masahaba hawa (Radhiya Llahu anhum) walioamini wakahama (Watu wa Makka) na walioamini wakatoa mahala pa kukaa (Watu wa Madina), kisha wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu wakiwemo Abubakar na Umar na Uthman na Aly na wenzao (Radhiya Llahu anhum jamiy’an).

Mwenyezi Mungu Mwenye kujuwa yaliyodhihirika na yaliyojificha aliangalia ndani ya nyoyo zao akawapa sifa hizo wanazostahiki.

Mwenyezi Mungu Anasema :

ألا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ {14)

Oh! Asijue Aliyeumba! Naye ndiye avijuaye visivyojulikana na vinavyojulikana?

Al Mulk-14

Ndugu zangu Waislamu, zile kauli zisemazo kuwa ulikuwepo uadui baina ya Masahaba na Watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) si sahihi. Hizi ni kauli zilizoingizwa ndani ya baadhi ya vitabu kwa ajili ya kujenga chuki baina yetu Waislamu na kututenganisha na kutudhoofisha. Msighururike nazo.

Na hapa tunakuleteeni mtiririko wa kauli mbali mbali kutoka kwa Maulamaa wa Kishia wenye kuonyesha mapenzi ya hali ya juu yaliyokuweo baina ya Maswahaba na baina ya Watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam):-

Imam Hassan Al Askary ambaye ni Imamu wa kumi na moja katika madhehebu ya Shia Ithnaasheri akihadithia juu ya siku ya Hijra allisema : « Baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kumtaka Aly Alayhissalaam alale juu ya tandiko lake, alimuambia Abubakar Al Siddique Radhiya Llahu anhu: «Utakuwa radhi uwe pamoja nami ewe Abubakar ukitafutwa kama ninavyotafutwa na ukijulikana kuwa wewe ndiye mwenye kunisaidia katika haya ninayowalingania watu ndani yake, na utabebeshwa kwa ajili yangu kila aina ya adhabu?» Abubakar akasema: «Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ama mimi hata kama nitaishi duniani nikaidhibishwa maisha yangu yote adhabu kali kali, bila ya kufa kifo cha uhakika na bila ya furaha, na yote haya yawe kwa ajili ya kukupenda wewe, basi hayo ni bora kwangu kuliko kuneemeka duniani nikiwamiliki wafalme wote dhidi yako. Kwani mimi na mali yangu na watoto wangu ni kitu gani isipokuwa ni kwa ajili yako.»

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasema: «Bila shaka Mwenyezi Mungu ameangalia ndani ya moyo wako akaona kuwa unakubaliana na yanayotamka ulimi wako. Akujaalie uwe mfano wa masikio yangu na macho yangu katika mwili, na roho katika nafsi.»

Tafsiri ya Al Hassan Al Askariy na Bihar Al Anwaar

Imepokelewa pia kuwa Aly bin Abi Talib alimuambia Uthman (Radhya Llahu anhum: «Na Wallahi sijui nikuambie nini. Hapana ninachokijua mimi usichokijua wewe, na hapana ninachoweza kukufundisha usichokifahamu, hatukukutangulia katika jambo lolote hata tuweze kukupa habari zake, wala hapana kilichofichika kwao tukakujulisha nacho. Umeona tuliyoyaona, na umeyasikia tuliyosikia, na umekuwa pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kama tulivyokuwa pamoja naye, na wala si mwana wa Quhafa, (Abubakar Al Siddique) wala si mwana wa Al Khattab, (Umar bin Khataab) waliokutangulia katika haki. Na wewe umehusiana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) zaidi kuliko wao, kwa sababu umeoa kwake zaidi kupita walivyofanya wao. Kwa hivyo Allah Allah katika nafsi yako…»

Nahaj Al Balaghah

Anasema Al Majlisiy kutoka kwa Attusy kuwa Imam Aly (Radhiya Llahu anhu) aliwaambia sahibu zake : «Nakuusieni juu ya sahibu zake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), msiwatukane kwani hawa ni sahibu zake Mtume wenu, na ni sahibu zake ambao hawajaongeza uzushi wowote katika dini, wala hawamuogopa mwenye kuleta uzushi. Ndiyo! Ameniusia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) juu yao hawa.»

Hayaat al Qulub kilichoandikwa na Al Majlisi- uk.122

Na kutoka kwa Jaafar Al Sadeq kutoka kwa wazee wake kutoka kwa Aly Alayhissalaam amesema: «Nakuusieni juu ya Sahibu zake Mtume wenu. Msiwatukane. Hawa hawajaongeza uzushi wowote, wala hawajampa ulinzi mwenye uzushi. Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ameusia juu yao kila la kheri. »

Bihar al Anwaar – 305 na Al Shia al Imamiyah, kilichoandikwa na Dr. Al Qifary-uk.935

Na siku ile Ibni Muljam (mwenye kustahiki kutoka kwa Mwenyezi Mungu kile anachostahiki) alipompiga upanga Aly bin Abi Talib – Alayhissalaam- na Aly alipohisi kuwa anafariki dunia, alimuusia mwanawe Al Hassan –Alayhissalaam- akimuambia ; ‘Allah Allah (nakuusia) juu ya wake wa Mtume wenu, wasidhulumiwe wakati mpo hai. Na Allah Allah (nakuusieni) juu ya Sahibu zake Mtume wenu, kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ameusia (mema) juu yao.’

Kash’f al Ghummah-2/59 na Muqatil al Talibin kilichoandikwa na Al Asfahani uk.39

Kutoka kwa Urwa bin Abdillah alisema :

Nilimuuliza Aba Jaafar Muhammad bin Aly –Alayhimassalaam- juu ya kuzipamba panga, akasema ; ‘Hapana ubaya, hata Abubakar Al Siddique alikuwa akiupamba upanga wake –Radhiya Llahu anhu.’ Nikamuambia : ‘Na unamuita ‘ Al Siddique ?’ anasema : ‘Aliinuka kwa haraka sana akaelekea kibla, kisha akasema ; ‘Naam (namuita) Al Siddique Naam (namuita) Al Siddique Naam (namuita) Al Siddique, na asiyemuita kwa sifa hii basi hana ukweli wowote duniani wala akhera.’

Kashf al Ghummah -2/360

Anasema Aly (Radhiya Llahu anhu):

« Nilipokwenda kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kumposa Fatima aliniambia: ‘Uza ngao yako kisha niletee thamani yake ili nipate kukutayarishia wewe na binti yangu Fatima kitakachoweza kukufaeni.» Anasema Aly : «Nikaichukua ngao yangu nikaenda nayo moja kwa moja mpaka sokoni nikamuuzia Uthman kwa Dirham mia nne. Na baada ya kupokea pesa zangu na baada ya Uthman kuipokea ngao yangu, akasema: Ewe Baba yake Hassan, ngao hii si imekuwa yangu na Dirham zimekuwa zako ?» Nikamuambia : «Ndiyo.» Akaniambia: «Basi ngao hii ni zawadi yako kutoka kwangu. » Nikaichukua ngao na Dirham nikaenda kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) nikaiweka ngao pamoja na pesa mbele yake, nikamhadithia aliyonitendea Uthman, akamuombea dua ya kheri. »

Al Manaqib/Al Khawarizmi uk.252 na Kashf al Ghummah 1/359 na Bihar al Anwar/Al Majlisi uk.39-40

Tunamuomba msomaji arudie marejeo yote upate kumbainikia ukweli na ili apate kufikiri na kutanabahi juu ya msimamo wa wenye kuwalani Masahaba wakiwemo Makhalifa watatu wa mwanzo wa Waislam.

Baada ya kuzisoma kauli hizi za Maimamu wa Ahlul Bayt – Alayhimussalaam- zinazowapa Maswahaba (Radhiya Llahu anhum) sifa zao wanazozistahi, kilichobaki hivi sasa ni kwa kila mwenye kudai kuwa anawapenda watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) nao pia wazitambue haki za Masahaba hawa (Radhiya Llahu anhum) kama zilivyotambuliwa na Maimam wao.

Hili ni tumaini letu kwa kila mwenye kuitafuta haki na mwenye kujinasibisha na Ahlul Bayt.

Na baada ya kuujua ukweli huu asije mtu akaanguka tena ndani ya shimo la kuwalani na kuwatukana Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na kuwatuhumu kwa ukafiri na unafiki.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuepushe na shari ya ukafir na unafik wabillahi tawfiyq

Wassalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh