ZANZIBAR:

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dr. Amani Abeid Karume leo anatarajiwa kushuhudia utiaji saini wa utengenezaji wa waya mpya wa umeme wa chini ya bahari wa megawati 100 kutoka Tanzania bara hadi Zanzibar.

Mkataba wa utekelezaji wa mradi huo utatiwa saini ikulu mjini hapa kati ya kampuni ya VISCAS ya Japan iliyoshinda tenda ya utengenezaji na uwekaji wa waya huo na afisi ya Changamoto za Milenia Tanzania inayofadhili mradi huo.

Taarifa iliyotolewa na afisi ya Chamoto za Milenia kwa vyombo vya habari imesema balozi wa Marekani nchini Tanzania pia atahudhuria utiaji wa saini huo na viongozi wengine wa serikali ya mapinduzi Zanzibar na taasi ya Changamoto.

Kukamilika kwa mradi huo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya dola za Marekani milioni 28 kutakiwezesha kisiwa cha Unguja kupata umeme wa uhakika ambao utachangia shughuli za uwekezaji.

Hivi karibuni waziri wa maji, ujenzi, nishati na ardhi Mansour Yussuf Himid amesema kisiwa cha Unguja bado kinakabiliwa na tatizo la umeme licha ya matengenezo makubwa yalifanywa kwenye waya wa sasa unaoleta umeme kutoka Tanzania bara.

Amesema waya huo wa megawati 45 licha ya kumalizika muda wake, umezidiwa na matumizi na kuwataka wananchi kujiepusha na matumizi yasiokuwa ya lazima.

Advertisements