Na Juma Abdala-Zenji Fm

ZANZIBAR:

Katibu mkuu wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi Zanzibar Khamis Mwinyi Mohammed amesema bado wafanyakazi wa serikalini na sekta binafsi Zanzibar wanaendelea kukabiliwa na matatizo mbayo serikali inawajibika kuyashughulikia.

Akizungumza siku moja baada ya maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kufanyika hapo kesho amesema pamoja na mafanikio yaliopatikana kwa wafanyakazi katika kipindi hiki, lakini bado wanakabiliwa na matatizo ya mishahara midogo ya kima cha chini, pensheni ndogo kwa wafanyakazi wanaostaafu na marekebisho ya mishahara yasiozingatia hali ya maisha.

Aidha katibu mkuu huyo amewataka wafanyakazi kuwachagua viongozi watakaojali maslahi ya wafanyakazi katika uchaguzi mkuu ujao.

Amesema wafanyakazi wasifanye makosa kwa vichagua vyama au viongozi wasiojali maslahi yao.

Na huko Tanzania bara shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania TUCTA limesema kufanya au kutofanya mgomo wa wafanyakazi wa nchi nzima wa kudai maslahi yao utategemea mazungumzo yao yanaoendelea na serikali.

Shirikisho hilo linakusudia kuitisha mgomo wa wafanyakazi wa nchi nzima Mei tano mwaka huu endapo serikali haitayapatia ufumbuzi madai ya wafanyakazi ya kuongeza maslahi yao.

Siku ya wafanyakazi duniani hudhimisha kila ifikapo Mei Mosi ya kila mwaka na kutoa fursa kwa wafanyakazi kutathimini na kutafakari maslahi na matatizo wanayokabiliana nayo katika sehemu za kazi.

Advertisements