Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Amani Abeid Karume,akisisitiza jambo baada ya mazungumzo yao na Mwenyekiti wa kamati maalun Usimamizi wa miradi ya maendeleo ya shirika la kimataifa la UNDP,Helen Clark alipofika Ikulu Mjini Zanzibar

Zanzibar                                                                                            6.5. 2010

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo Duniani (UNDP) limeeleza kufarajika na hatua za maendeleo zilizofikiwa hapa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuziweka pamoja afisi zote za Umoja wa  Mataifa (ONE UN) katika jengo moja, hali ambayo  imeweza kurahisisha utendaji wa kazi.

Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo Duniani (UNDP)  Bi Helen Clarke aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume,Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Bi Clarke alimueleza Rais Karume kuwa mafanikio yaliopatikana Zanzibar ni makubwa na kuna kila sababu ya Shirika lake kuendelea kuyaunga mkono ili mafanikio hayo yaimerike zaidi.

Bi Clarke alipongeza kwa mafanikio ya  miradi inayoendeshwa na  UNDP hapa Zanzibar.

Akieleza juu ya kuvutiwa kwake na mipango maalum iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kuziweka katika jengo moja afisi zote za Mashirika ya Umoja wa Mataifa (ONE UN) zilizopo Zanzibar hapo katika jengo la kitega Uchumi la ZSTC liliopo Gulioni mjini Zanzibar, Bi Clarke alieleza kuwa hiyo ni hatua kubwa ya mafanikio.

Alieleza kuwa hatua hiyo iliyowekwa na serikali ni nzuri na inaleta ufanisi zaidi katika utendaji wa kazi na pia inaonesha ni kwa jinsi gani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikiyajali Mashirika ya UN hapa nchini.

“Nimefarajika sana na hatua za maendeleo pia kuona afisi zote za UN zipo sehemu moja, nilijona kama nipo New York, naipongeza sana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar nakupongeza Rais Karume…),alisema Bi Clarke.

Aidha, Bi Clarke alimueleza Rais Karume kuwa UNDP itaendelea kutoa ushirikiano wake katika kuimarisha sekta za maedeleo hapa Zanzibar.

Pamoja na hayo, Bi Clarke alipongeza uendelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Shirila lake hapa nchini na kupongeza hatua za miradi hiyo ilivyofikiwa hapa Zanzibar.

Pia, Mwenyekiti huyo  alipongeza hatua za uimarishaji wa demokrasia hapa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha maelewano na maridhiano ndani ya jamii ya Wazanzibari hatua ambayo itaifanya Zanzibar izidi kuimarika katika sekta zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Sambamba na hayo Bi Clarkealieleza kuvutiwa kwake na ushirikishwaji wa wanawake katika Baraza la Wawakilishi hapa Zanzibar sanjari na kupongeza mikakati ya kuongezeka kwa wanawake katika Baraza hilo la kutunga sheria.

Bi Clarke yupo Zanzibar kwa ziara ya siku moja ambapo katika ziara hiyo mbali ya kukutana na viongozi pamoja na kufanya nao mazungumzo pia atatembelea sehemu mbali mbaali zikiwemo za kihistoria.

Nae Rais Karume kwa upande wake alimueleza Bi Clarke kuwa UNDP imekuwa mstari wa mbele katika kuiunga mkono miradi mbali mbali inayoendeshwa hapa Zanzibar hali ambayo imeweza kuleta mafanikio zaidi.

Rais wa Karume alieleza kuwa miongoni mwa juhudi zilizochukuliwa na Shirika hilo ni pamoja na kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Mkakati mzima wa Kukuza Uchumi na Kupambana na Umasikini (MKUZA).

Akieleza juu ya mafanikio ya kuziweka afisi za Umoja wa Mataifa katika jengo moja Raius Karume alisema kuwa hiyo ni changamoto kubwa kwa serikali kwani hatua hiyo imefikiwa kutokana na umuhimu wake mkubwa.

Rais Karume pia,a lieleza kuwa mbali ya juhudi za serikali katika kuendeleza miradi ya maendeleo sekta ya nishati nayo imepewa kipaumbe ambapo tayari saini juu ya mradi mkubwa wa umeme kutoka Da-r-es-Salaam hadi Zanzibar imeshatiwa kwa msaada wa serikali ya Marekani kupotia MCC.

Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia zaidi katika uimarishaji sekta za maedeleo sanjari an ukuzaji wa uchumi kwa kuimarisha sekta ya viwanda na utalii hapa Zanzibar.

Rais Karume pia, alimpongeza Bi Clarke kwa kushika wadhifa huo, kwani kabla ya hapo aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa New Zealand  kwa muda wa miaka tisa pamoja na kushika nyadhifa nyengine.

Rajab Mkasaba

Advertisements