moja ya meli za kigeni zinazovua katika bahari kuu ya Tanzania ambapo Zanzibar inataka kupatiwa mgao wa mapato ya asilimia 40

Na Salha Hamad-Zanzibar

ZANZIBAR:

Idara ya uvuvi na mazao ya baharini Zanzibar imesema mgao wa mapato ya rasilimali za bahari kuu bado haujafikiwa kufuatia serikali ya Tanzania kutiliana saina na meli za uvuvi za kigeni kuendesha shughuli za uvuvi wa bahari kuu.

Mkurugenzi wa idara hiyo Mussa Aboud Jumbe amesema Zanzibar haijajua hatma ya mafao yake baada serikali ya muungano kuingia mkataba na meli za uvuvi za Uhispania wenye thamani ya dola za Marekani laki sita kwa mwaka.

Hata hivyo amesema suala hilo bado linashughulikiwa na wizara ya kilimo, mifungo na mazingira ya Zanzibar kwa kuwasilisna na wizara ya maendeleo ya uvuvi na ufugaji Tanzia bara ili kujua mapata ya Zanzibar.

Bw. Jumbe ametoa ufuafanuzi huo alipokuwa akijibu maswali ya mwenyekiti wa kamati ya uchumi na fedha ya baraza la wawakilishi Salmini Awadh Salmini wakati wajumbe wa kamati hiyo walipofanya ziara ya kukagua majengo ya idara yanayojengwa kupitia mradi wa MACEMP.

Kauli hiyo ya mkurugenzi Jumbe imekuja baada ya Waziri wa maendeleo ya mifugo na uvuvi John Magufuli kutangaza Hispania imetoa zaidi ya dola laki sita kwa ajili ya kuendesha shughuli za uvuvi wa bahari kuu upande wa Tanzania.

Waziri Magufuli amefahamisha tayari meli 16 za Uhispania ziko nchini kwa ajili ya kuanza shughuli za uvuvi katika eneo hilo na meli nyingine za uvuvi kutoka nchi nyingine ikiwemo China zimeonesha nia ya kutaka kuvua eneo la bahari kuu la Tanzania.

Suala la uvuvi wa Bahari Kuu ni miongoni mwa mambo ya Muungano ambapo kwa mujibu wa sheria ya mamlaka ya uvuvi wa bahari kuu, Zanzibar inatakiwa kupata asilimia 40 ya mapato yanayotoka na uvuvi wa bahari kuu.

Advertisements