Archive for June, 2010

SHEIKH SIMBA AWATULIZA WAISLAM JUU YA MAHAKAMA YA KADHI

Sheikh Issa Shaban

Sheikh mkuu wa Tanzania Issa Shaaban amewataka waislamu nchini kudumisha amani na kuvuta subra wakati kamati iliyoteuliwa kusimamia undwaji wa mahakama ya kadhi ikifanya kazi zake ili kuweka mfumo wa utaratibu na utekelezaji wa suala hilo.

Shehe Shaaban ametoa tamko hilo aliopokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam juu ya namna ya suala hilo linavyoshughulikiwa.

Suala la mahakama ya kadhi limekuwa likizungumza na makundi mbali mbali kutokana na suala hilo kuingizwa katika ilani ya chama cha mapinduzi na kuibua misimamo tofauti juu ya suala hilo.

Advertisements

NDEGE YA JESHI LA JWTZ YAPATA AJALI TANGA

Ndege inayosadikiwa Mali ya jeshi la wananchi wa Tanzania JWTZ kikosi cha Ngerengere imeanguka na kuligonga Basi la watalii waliokuwa barabarani katika eneo la Manga Mkoani Tanga na kusababisha vifo vya marubani wawili waliokuwa katika ndege hiyo.

Kwa mujibu wa shuhuda wa ajali hiyo amesema ndege hiyo yenye nambari 919 ilikuwa katika mazoezi . …

Askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania pamoja na Jeshi la Polisi wamefika katika eneo la tukio kwa ajili ya kuondoa ndege hiyo ambayo imelala barabarani na kuzuwia mabasi yanayotoka Dar es salaam ,Tanga na Arusha kusimama kutokana na barabra hiyo kutopitika kutokana na ndege hiyo

SMZ YASHINDWA KULIENDELEZA ENEO LA UWEKEZAJI FUMBA

Moja ya eneo la uwekezaji Fumba

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema bado haijafanikiwa kuweka miundo mbinu katika eneo la uwekezaji la Fumba wilaya ya magharibi kutokana na gharama kubwa za fedha zinazohitajika.

Akijibu suala katika kikao cha baraza la wawakilishi waziri anaeshughulikia fedha na uchumi Dr. Mwinyihaji Makame amesema serikali inaendelea kuwakaribisha wawekezaji kuendeleza miundombinu hiyo.

Amesema eneo hilo limetangwa kwa ajili ya sekta ya viwanda ambapo wawekezaji wanaweza kudhalisha bidhaa na kuuzwa nje ya nchi.

Serikali ya mapinduzi Zanzibar imelitangaza eneo la Fumba kuwa la uwekezaji kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita, lakini uwekezaji uliofanywa katika eneo hilo bado ni mdogo kulinga na ukubwa wa eneo lenyewe.

SMZ USO KWA USO NA TANESCO

Serikali ya mapinduzi Zanzibar imesema kitendo cha shirika la umeme Tanzania TANESCO cha kutotekeleza agizo la waziri mkuu kuipinguzia bei ya umeme Zanzibar kinaweza kudhoofisha muungano wa nchi mbili hizo.

Waziri wa nchi afisi ya waziri kiongozi Hamza Hassan Juma amesema Zanzibar ilitaka ilipe bei ya umeme ya asilimia 21.7 kama wanavyolipa Tanzania bara badala ya asilimia 168.7 bei ya sasa.

Akijibu suala katika kikao cha baraza la wawakilishi amesema afisi ya waziri mkuu ilikubali ombi hilo na kuitaka wizara ya nishati Tanzania bara kutekeleza suala hilo, lakini agizo hilo halijatekelezwa.

Waziri Juma amesema bei ya huduma ya umeme inayotozwa na TANESCO ya asilimia 168.7 kwa Zanzibar ni kubwa  kutokana na miundo mbinu ya kusambaza umeme huo ni mali ya Zanzibar.

Hata hivyo waziri huyo amesema serikali bado ina imani na maelekezo waliopewa wizara ya nishati ya Tanzania bara juu ya malipo ya umeme kwa upande Zanzibar utatekelezwa na kuwaomba wananchi wa kuendelea kusubiri huku serikali ikichukua juhudi za kutatua kero hiyo.

Hivi karibuni TANESCO ilitangaza ongezeko la malipo ya umeme kwa asilimia 168% upande wa Zanzibar kiwango kinachodaiwa kikubwa ikilinganishwa na Tanzania bara cha asilimia 21.7.

WAZIRI MEMBE AIONYA BURUNDI

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Benerd Membe

Baadhi ya wakimbizi wa Burundi walioko nchini Tanzania

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Benerd Membe amesema wakati Burundi ikielekea kufanya uchaguzi wa urais, hali bado mbaya nchini humo, licha ya ushirikiano wa kikanda kunusuru hali hiyo.

Amesema Tanzania inaweza kuelemewa na mzigo wa wakimbizi iwapo nchi hiyo itaingia tena katika machafuko.

Kwa mujibi wa Membe mawaziri wa mambo ya nje wa Afrika ya Mashariki waliamuwa kukutana na viongozi wa kisiasa nchini Burundi na kubaini kiongozi wa upinzani Agathon Rwasa hayupo nchini humo.

Burundi inatarajia kufanya uchaguzi mkuu siku ya Jumatatu.

SOS ZANZIBAR WAOMBA MSAADA

Watoto yatima wanaolelewa katika kijiji cha SOS kilioko Mombasa mjini Zanzibar

Kijiji cha SOS Zanzibar kimetoa wito kwa wananchi na wahisani nchini kuchangia maendeleo ya kijiji hicho ili kuona watoto yatima wanaolelewa katika kijiji hicho wanapata huduma nzuri.

Mkurugenzi wa kijiji hicho Suleiman Mahamoud Jabir anesena bado kijiji hicho kinahitaji ufadhili kwa mtoto mmoja mmoja, familia, nyumba na mradi au hata kufadhili kijiji kizima.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa mwanzilishi wa jumuiya ya SOS duniani Dr. Herman Gmeiner yaliofanyika kijijini hapo Mombasa amesema licha ya kijiji hicho kupata ufadhili nje ya nchi lakini bado kinahitaji ufadhili wa ndani.

Amesema ingawa wafadhili wa kijiji hicho hawajalalamika ambao wengi wao ni wanafunzi kutoka nchi za Scandanavia, lakini jamii inapaswa kufahamu mzozo wa kiuchumi uliozikumba nchi za magharibi ambao umeathiri maendeleo ya kijiji cha SOS Zanzibar.

Hivyo mkurugenzi huyo amewataka wananchi na wahisani wa ndani kujitokeza kwa wingi kuchangia maendeleo ya watoto yatima wanaolelewa katika kijiji hicho pamoja na watoto wengine wanaoishi na familia zao.

Mwanzilishi wa kijiji cha SOS duniani Dr. Herman raia wa Australia alizaliwa June 23 mwaka 1919, inasemekana alianzisha kijiji hicho kwa fedha ndogo kutokana moyo wake wa huruma wa kuwasaidia watoto yatima ambao familia zao hazina uwezo.

ZANZIBAR KUANZA UTAFITI WA UCHIMBAJI MAFUTA NA GESI

Waziri wa maji,ujenzi,nishati na ardhi Zanzibar Mansour Yussuf Himid

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatarajia kufanya utafiti wa kimazingira kuhusiana na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kwa kushirikiana na serikali ya Norway.

Akiwasilisha hutuba ya bajeti waziri wa wizara ya mawasiliano na uchukuzi Zanzibar  Mansour Yussuf Himid amesema mipango ya utafiti huo umefikia katika hatua nzuri na unaweza kuanza muda mfupi ujao.

Amesema serikali ya Norway inafanya mazungumzo na mshauri mwelekezi kwa ajili ya kazi hiyo ili kujua gharama za utekelezaji wa utafiti huo.

Kuhusu suala la mafuta na gesi asilia kuondolewa kisheria kwenye orodha ya mambo ya muungano Himid amesema baraza la mapinduzi limemuagiza waziri kiongozi kumuandikia barua waziri mkuu kulitoa suala.

Amesema wizara yake inasubiri maelekezo kutoka afisi ya waziri kiongozi juu ya suala hilo ili kuanza hatua nyingine za uchimbaji na utafutaji wa nishati hiyo.

Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na wizara hiyo katika uchimbaji wa mafuta na gesi ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake na kuwapeleka masomoni vijana kumi nje ya nchi kupata taaluma