PRESS RELEASE

Zanzibar                                                                                          8.6.2010

BENKI ya Maendeleo Afrika (ADB) imeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa hapa Zanzibar kwa ushirikiano baina ya Zanzibar na Benki hiyo na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo ili kuleta mafanikio zaidi.

Mwakilishi Mkaazi wa Benki ya Maendeleo Afrka (ADB), anaemaliza muda wake hapa nchini Dk. Sipho Moyo aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume, Ikulu mjini Zanzibar.

Katika maelezo yake Mwakilishi Mkaazi huyo, alimueleza Rais Karume kuwa ADB inafarajika kwa kiasi kikubwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopo hapa Zanzibar kutokana na kuweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Alisema kuwa hatua ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa mashirikiano na ADB hapa Zanzibar ni nzuri na ya kuungwa mkono katika suala zima la kuleta maendeleo na kuimarisha uchumi.

Dk. Moyo alisema kuwa kutokana na hatua hizo ADB itaendeleza kuunga mkono zaidi miradi iliyopo na kuiimarisha ile inayoanzishwa kutokana na kuwa na mwanga wa mafanikio.

“Kwa kweli Zanzibar imepiga hatua kubwa katika uimarishaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ninadiriki kusema kuwa hayo yote yanatokana na uongozi wako mzuri Mhe. Rais Karume”,alisema Mama Moyo.

Aidha, Dk. Moyo alieleza kuwa ADB imeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kufanya kazi zake hapa Zanzibar  kutokana na mashirikiano makubwa inayoyapata kutoka kwa viongozi wa serikali, taasisi na wananchi kwa jumla.

Sambamba na hayo, Mama Moyo alitoa pongezi na shukurani kubwa kwa viongozi na wananchi wa Zanzibar kutokana na ukarimu wao ambao ulimuwezesha yeye kufanya kazi zake  kwa ufanisi mkubwa katika muda wake wote aliofanya kazi hapa nchini.

Nae Rais Karume kwa upande wake, alimueleza Mwakilishi huyo kuwa mafanikio hayo yote ya uendelezaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo yaliyopatikana hapa Zanzibar ADB nayo imeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa.

Rais Karume alieleza kuwa ADB imeweza kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta za miundombinu ya barabara, elimu, maji,afya, sheria na uongozi wa fedha za umma na uchumi, utawala bora na nyenginezo.

Aidha, Rais Karume alisema kuwa ADB imekuwa na mashirikiano mazuri na Zanzibar hali ambayo imeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa utekelezaji na uendelezaji wa miradi ya maendeleo hapa Zanzibar.

Rais Karume alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inathamini kwa kiasi kikubwa hatua za ADB za kuendelea kuunga mkono miradi ya maendeleo hapa nchini na kuahidi kuendeleza ushirikiano na uhusiano wake uliopo.

“Nafurahishwa sana na juhudi za ADB za kushirikiana nasi katika kuimarisha miradi ya maendeleo kwani hatua hiyo imeweza kuleta manufaa makubwa sana katika kuimarisha uchumi na maendeleo yetu”.alisema Rais Karume.

Aidha, Rais Karume alimueleza Mwakilishi huyo wa ADB nchini Tanzania kuwa kwa upande wa uimarishaji wa miundombinu ya barabara kutaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya utalii, biashara na uwekezaji hapa nchini.

Alieleza kuwa juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar za kuimarisha sekta zake za maendeleo na huduma za kijamii imekuwa chachu kwa washiriki wa maendeleo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar kutokana na mafanikio yaliopatikana.

Sambamba na hayo, Rais Karume alitoa shukurani kwa ADB pamoja na Mwakilishi huyo kwa kuendeleza na kuimarisha ushirikiano ambao umeweza kuendeleza vyema miradi ya maendeleo na kumtakia heri na mafanikio katika shughuli zake nyengine atakazopangiwa baada ya kumaliza muda wake wa kazi hapa nchini.

Advertisements