Watoto yatima wanaolelewa katika kijiji cha SOS kilioko Mombasa mjini Zanzibar

Kijiji cha SOS Zanzibar kimetoa wito kwa wananchi na wahisani nchini kuchangia maendeleo ya kijiji hicho ili kuona watoto yatima wanaolelewa katika kijiji hicho wanapata huduma nzuri.

Mkurugenzi wa kijiji hicho Suleiman Mahamoud Jabir anesena bado kijiji hicho kinahitaji ufadhili kwa mtoto mmoja mmoja, familia, nyumba na mradi au hata kufadhili kijiji kizima.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa mwanzilishi wa jumuiya ya SOS duniani Dr. Herman Gmeiner yaliofanyika kijijini hapo Mombasa amesema licha ya kijiji hicho kupata ufadhili nje ya nchi lakini bado kinahitaji ufadhili wa ndani.

Amesema ingawa wafadhili wa kijiji hicho hawajalalamika ambao wengi wao ni wanafunzi kutoka nchi za Scandanavia, lakini jamii inapaswa kufahamu mzozo wa kiuchumi uliozikumba nchi za magharibi ambao umeathiri maendeleo ya kijiji cha SOS Zanzibar.

Hivyo mkurugenzi huyo amewataka wananchi na wahisani wa ndani kujitokeza kwa wingi kuchangia maendeleo ya watoto yatima wanaolelewa katika kijiji hicho pamoja na watoto wengine wanaoishi na familia zao.

Mwanzilishi wa kijiji cha SOS duniani Dr. Herman raia wa Australia alizaliwa June 23 mwaka 1919, inasemekana alianzisha kijiji hicho kwa fedha ndogo kutokana moyo wake wa huruma wa kuwasaidia watoto yatima ambao familia zao hazina uwezo.

Advertisements