Serikali ya mapinduzi Zanzibar imesema kitendo cha shirika la umeme Tanzania TANESCO cha kutotekeleza agizo la waziri mkuu kuipinguzia bei ya umeme Zanzibar kinaweza kudhoofisha muungano wa nchi mbili hizo.

Waziri wa nchi afisi ya waziri kiongozi Hamza Hassan Juma amesema Zanzibar ilitaka ilipe bei ya umeme ya asilimia 21.7 kama wanavyolipa Tanzania bara badala ya asilimia 168.7 bei ya sasa.

Akijibu suala katika kikao cha baraza la wawakilishi amesema afisi ya waziri mkuu ilikubali ombi hilo na kuitaka wizara ya nishati Tanzania bara kutekeleza suala hilo, lakini agizo hilo halijatekelezwa.

Waziri Juma amesema bei ya huduma ya umeme inayotozwa na TANESCO ya asilimia 168.7 kwa Zanzibar ni kubwa  kutokana na miundo mbinu ya kusambaza umeme huo ni mali ya Zanzibar.

Hata hivyo waziri huyo amesema serikali bado ina imani na maelekezo waliopewa wizara ya nishati ya Tanzania bara juu ya malipo ya umeme kwa upande Zanzibar utatekelezwa na kuwaomba wananchi wa kuendelea kusubiri huku serikali ikichukua juhudi za kutatua kero hiyo.

Hivi karibuni TANESCO ilitangaza ongezeko la malipo ya umeme kwa asilimia 168% upande wa Zanzibar kiwango kinachodaiwa kikubwa ikilinganishwa na Tanzania bara cha asilimia 21.7.

Advertisements