July 11, 2010

Chama cha Mapinduzi(CCM) leo kimemchagua rasmi Jakaya Mrisho Kikwete kuwa mgombea wake katika Uchaguzi Mkuu mwezi Octoba mwaka huu.

Baada ya mashauriano na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Rais Kikwete amemteua Dr.Mohammed Gharib Bilal, kuwa mgombea mwenza.Kwa maana hiyo tiketi ya CCM itabebwa na Jakaya Mrisho Kikwete na Dr.Mohammed Gharib Bilal.

Dr.Gharib Bilal alizaliwa tarehe 6 Februari,1945 huko Unguja. Dr.Bilal ni mwanasayansi aliyepata stashahada ya kwanza katika sayansi ya nuklia kutoka Chuo Kikuu cha Howard nchini Marekani mwaka 1967. Alipata Masters Degree katika masuala hayo hayo ya sayansi ya nuklia kutoka Chuo Kikuu Cha California mwaka 1969 kabla ya kupata PhD katika fizikia kutoka chuo hicho hicho cha California mwaka 1976. Kuanzia mwaka 1976 mpaka mwaka 1990 alikuwa Lecturer(mkufunzi) katika Chuo Kikuu Cha Dar-es-salaam-Idara ya Fizikia

Kati ya mwaka 1990 na 1995 alikuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Sayansi,Tekinolojia na Elimu ya Juu katika serikali ya Muungano.Mwaka 1982 alikuwa Mkuu wa Kitivo Cha Sayansi,Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, aliteuliwa na Rais Salmin Amour kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar. Mwaka 2000 aligombea Urais wa Zanzibar bila mafanikio. Mwaka huu alikuwemo miongoni mwa waliojitokeza kuomba ridhaa ya CCM kusimama kama mgombea Urais Zanzibar lakini bahati hiyo ikamuangukia Dr.Ali Mohammed Shein.Badala yake na kwa maana hii,atasimama na Kikwete kama mgombea mwenza na hivyo,endapo watashinda,atakuwa Makamu wa Rais wa serikali ya Muungano.

Advertisements