Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dr. Amani Abeid Karume

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dr. Amani Abeid Karume amewataka wananchi kuzitumia fursa ziliopo kwa kuwekeza miradi ya kiuchumi ili kuondokana na umasikini.

Amesema serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kama vile ujenzi wa miundo mbinu ya barabara, umeme na huduma za bandari na uwanja wa ndege kama njia moja wapo ya kusogeza maendeleo.

Rais Karume amesema hayo alipokuwa akizundua mradi wa majenerata 32 ya umeme wa dharura huko kituo cha Umeme Mtoni wilaya ya Magharibi.

Majenerata hayo 32 yenye uwezo wa kuzalisha umeme mega 25 yamegharimu zaidi ya dola za Marekani milioni 13 ikiwa ni msaada kutoka nchi ya Norway, Uingereza na Sweeden na serikali ya Mapinduzi Zanzbiar imechangia dola milioni moja na nusu.

Kuwepo kwa majenerata hayo kutasaidia kupatikana huduma ya umeme wakati inapotokea hitlafu katika gridi ya taifa.

Matumizi ya huduma ya umeme Zanzibar yameongezeka kutoka megawati 25 mwaka 2000 hadi megawati 50 kwa Unguja na Pemba ambapo shirika la umeme Zanzibar linalipia zaidi ya shilingi milioni 500 na kuskusanya shilingi bilioni tatu kila mwezi.