Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Amani Abeid Karume,akitumbukiza kura yake,katika kituo cha kupigia kura ya Maoni, ya kuwezesha Uundwaji Serikali ya Kitaifa ya Zanzibar,katika Skuli ya Msingi ya Kiembesamaki Wilaya Magharibi jana,Uundwaji wa Serikali hiyo ya Kitaifa ni baada ya Uchaguzi Mkuu ujao wa mwezi Octoba mwaka 2010.

Zanzibar imepiga kura ya maoni kwa amani na utulivu, huku kukiwa na idadi kubwa ya watu walijitokeza kupiga kura hiyo itakayotoa ridhaa ya kukubali au kupinga undwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi mkuu Octoba mwaka huu.

Upigaji kura huo umeanza mapema leo asubuhi na kumalizika saa 10.00 jioni hii ambapo wananchi waliopiga kura wameelezea kuridhishwa na upigaji wa kura hiyo.

Mwandishi wetu alietembelea katika vituo vya manispaa ya mji wa Zanzibar amesema upigaji wa kura hiyo haukuwa na usumbufu mkubwa kama zilivyokuwa chaguzi zilizopita.

Jumla ya vituo vya kupigia kura elfu moja na 400 Unguja na Pemba vimetumika kupigia kura hiyo, huku baadhi ya vituo vimeripotiwa kutokea matatizo ya majina ya wapiga kura kujitokeza mara mbili, hata hivyo wananchi hao walipiga kura.

Hata hivyo mkurugenzi wa tume ya uchaguzi Zanzibar Salum Kassim amesema bado hajapokea taarifa yoyote ya matatizo katika vituo vya kupigia kura.

Amesema idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza kupiga kura hiyo na kufikia zaidi ya asilimia 90 ambapo matokeo yatatangazwa ndani ya saa 26

Nae mwandishi  wetu alioko Kisiwani Pemba amesema kazi za upigaji kura katika kisiwa hicho zilifanyika kwa amani na utulivu, licha kuwepo kwa baadhi ya watu ya kuendesha kampeni za siri wakati wa upigaji kura.

Hata hivyo msimamizi wa kura ya maoni katika skuli ya Madungu Ali Mussa Said amesema……CLIPS….(SAVED-PEMBA)

Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume alipiga kura katika kituo cha Kiembe samaki na kueleza kuwa amefarijika kuona zoezi hilo linakwenda kwa amani na utulivu na kuwataka wananchi kudumisha utulivu wakati wote wa upigaji kura na baada ya kupiga kura na baada ya matokeo.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya kuweka kura ya maoni kura zote zitahesabiwa katika vituo na kutangazwa kabla ya kufanyika majumuisho ya mwisho.

Naye katibu mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad alipiga kura yake katika kituo cha Mtoni wakati mgombea mwenza wa urais wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal alipiga kura katika kituo cha Kiembe samaki.

Maalim Seif alisema kwamba kura hiyo ya maoni imefanyika katika mazingira ya amani na utulivu kutokana na maridhiano yaliofikiwa kati yake na rais Karume huku huku akisisitiza kudumishwa amani iliyopo.

Alisema ni jambo la faraja kuona wananchi wanatekeleza haki yao ya kikatiba bila ya kusukumana tofauti na miaka ya nyuma na kuwataka wananchi kuendelea kudumisha hali ya maelewano hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi huu mkuu.

Jumla ya wapiga kura laki nne, elfu saba 950 wameandikishwa kupiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Iwapo kura za ndio zitafika asilimia 51 baraza la wawakilishi litakutana kwa mara ya mwisho Agost tisa mwaka huu kabla ya kumaliza muda wake wa miaka mitano ili kufanya marekebisho ya katiba ya Zanzibar.