Archive for August, 2010

RAIA WA AFRIKA YA KUSINI AJINYONGA KISIWANI PEMBA

Ufukwe mwanana wa kitalii Pemba

Raia mmoja wa Afrika ya kusini amekutwa amekufa baada ya kujinyonga chumbani kwake katika hoteli ya Manta Riff iliyopo Micheweni Kisiwani Pemba.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kaskazini Pemba Rashid Yahya Bugi amesema raia huyo alitambuliwa kwa jina la James Ignatus White mwenye umri wa miaka 21 ni mfanyakazi wa hotel ya Manta Riff.

Amesema jeshi la polisi mara baada ya kupokea taarifa za tukio hilo lilikwenda katika eneo hilo na kuukuta mwili wa White ukiwa ananinginia katika kamba aliyojitundika.

Hata hivyo amesema chanzo cha kujiua kwa raia huyo wa kigeni bado hakijafahamika kwa vile hajawacha ujumbe wowote

Mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa uongozi wa hoteli ya Manta Riff kwa ajili ya kuusafirisha nchini kwao Afrika ya Kusini.

Advertisements

MAELFU YA WAUMINI WA KISLAMU WAMZIKA MUFTI MKUU WA ZANZIBAR

Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Shaaban Bin Simba akiongoza Du'aa kumuombea Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Harith bin Khelef wakati mwili wake ulipowasili katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere. Kulia kwa Mufti ni Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi na anaefuatia ni Kaimu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji Khamis. Kushoto kwa Mufti ni Sheikh Mkuu wa Dar Al Had Musa Salum (Picha na Othaman Maulid)

Maelfu ya waumini wa dini ya kislamu na wananchi wengine leo wamehudhuria maziko ya mufti mkuu wa Zanzibar sheikh Harith bin Helf aliefariki nchini India Alhamis iliyopita.

Maziko hayo yaliofanyika kijijini kwao Muyuni Wilaya ya Kusini yameongozwa na makamo wa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr. Ali Mohammed Shein.

Viongozi wengine waliohudhuria maziko hayo ni rais mstaafu wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi, waziri kiongozi wa Zanzibar Shamsi Vuai Nahodha na mufti mkuu wa Tanzania bara Sheikh Shaaban bin Simba na viongozi wengine wa serikali na kidini.

Marehemu Harith amezaliwa mwaka 1927 katika kijiji cha Muyuni alipata elimu ya msingi mwaka 1937 na elimu ya chuo kikuu cha Alzhar nchini Misri na kuchaguliwa mufti mkuu wa Zanzibar mwaka 1992.

Marehemu alifariki dunia nchini India katika hospitali ya Miyot alikukuwa akitibiwa ugonjwa wa moyo na uti wa mgongo. Mungu ailaze roho ya marehemu peponi amina.

CHADEMA YATAKA RAIS KIKWETE AWEKEWE PINGAMIZI

Chama cha Demokraisa na maendeleo CHADEMA kimewasilisha malalamiko kwa msajili wa vyama vya siasa kikitaka mgombea wa urais wa Tanzania kupitia chama cha Mapinduzi CCM rais Jakaya Kikwete awekewe pingamizi katika kinyanganyiro cha uchaguzi wa urais.

Hoja kuu ya CHADEMA kuweka pingamizi ni kwa serikali kupandisha mishahara ya wafanyakazi waliokusudia kugoma wakati wa mkutano wa uchumi wa dunia, lakini rais Kikwete wakati huo alisema hawezikupandisha mishahara.

Kaimu katibu mkuu wa CHADEMA John Mnyika amesema hatua ya sasa ya serikali kupandisha mishahara ya watumishi wa umma inahesabiwa kama yenye kutaka ungwaji mkono na wafanyakazi.

Mnyika amedai suala la nyongeza wa mishahara kwa wafanyakazi halikuongezwa na bunge kama vile ilivyopendekezwa hivyo suala hilo linatumiwa kama kampeni za mgombea huyo na kwenda kinyume na sherria ya gharama za uchaguzi

MGOMBEA URAIS KUPITIA SAU ASHINDWA KUREJESHA FOMU

Ikiwa leo ni siku ya mwisho kurejesha fomu za kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar, mgombea wa nafasi hiyo kupitia Chama Cha Sauti ya Umma (SAU) Haji Mussa Kitole ameshindwa kurejesha fomu za kuwania nafasi hiyo kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Kitole awali alikataliwa kupewa fomu ya kuwania nafasi hiyo na ZEC kutokana na kuwa chama hicho kimetoa wagombea urais wawili wenye kutaka kuwania urais wa Zanzibar wakati sheria za ZEC zinaeleza chama kitowe mgombea mmoja wa nafasi hiyo.

Vyama ambavyo vimerejesha fomu leo katika afisi hiyo ni NCCR-MAGEUZI, TADEA, AFP, NRA, Jahazi Asilia huku chama cha SAU kikiwa bado hakijarejesha fomu hiyo.

Akizungumza na Zenji fm radio afisa wa habari wa tume ya uchaguzi Zanzibar Idriss Haji Jecha amesema hadi kufikia saa 9.45 cha cha SAU bado hakijarejesha fomu ambapo muda wa mwisho ulikuwa saa 10.00 jioni.

Amesema katika urejeshaji wa fomu hizo hakukuwa na kasoro zozote na fomu zilizorejeshwa zilikuwa safi.

SAU ndio chama pekee kilichoshindwa kuwasilisha fomu zake kwa tume ya uchaguzi ambapo vyama vyengine vilivyorejesha fomu zake jana ni pamoja Juma Ali Khatib (46) -TADEA, saa 4:13 asubuhi, Said Soud Said (62) AFP,saa 5:00, Haji Ambar Khamis (44) NCCR–Mageuzi, saa 5:30, Kassim Bakari Ali (43) Jahazi Asilia, saa 7.06, na Haji Khamis Haji (60) NRA saa 8:20 mchana.

Wengine waliorejesha fomu zao kwa ZEC wa mwanzo ni ni Mgombea wa chama cha wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ((67) alirejesha Agosti 16 majira ya saa 9:00 mchana wakati mgombea wa chama cha mapinduzi (CCM) Dk Ali Mohammed Shein (62) alijesha fomu yake Agosti 18 majira ya saa 8:30 mchana.

Akizungumza katika kikao hicho baada ya kupokea fomu hizo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Khatib Mwinchande alisema kwao wao kujitokeza kwa wagombea wengi ni kupanuka kwa demokrasia nchini.

Mwenyekiti huyo aliwaomba wagombea wote ambao watateuliwa na tume kuingia katika mchakato wa kutaka urais baada ya kuhakikiwa fomu zao kuingia katika kampeni za kistaarabu zisizo na matusi ili kuepusha Zanzibar kuingia katika sura mbaya ya kukosekana amani.

Iwapo wagombea urais kutoka vyama hivyo hawatawekewa pingamizi uchaguzi mkuu kwa nafasi ya urais unatarajiwa kufanyika Octoba 31 mwaka huu utakuwa na wagombea saba.

TATIZO LA SOMALIA NI UINGILIAJI KATI WA MATAIFA YA KIGENI-HIZB UT-TAHARIR

Baadhi ya majeshi ya kigeni yakilinda amani nchini Somalia

Jumuiya ya kislamu ya kimataifa ya Hiz Ut-Tahrir imepinga ungiliaji kati unaofanywa na mataifa ya kigeni katika mzozo unaoendelea nchini Somalia kati ya wanamgambo wa Al-shabab na serikali ya mpito ya nchi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa naibu mwakilishi wa wa vyombo vya habari vya Jumuiya hiyo Afrika Mashariki Massoud Mselem amesema mzozo wa Somalia hauhitaji nguvu za kijeshi bali ni kuangalia kiini cha tatizo lenyewe.

Amesema suluhisho la amani ya Somalia sio kupambana na wanamgambo wa Al-Shabab bali ni kupinga uingiliaji kati wa masuala ya nchi hiyo dhidi ya mataifa ya kigeni

Akizungumzia mateso na vitendo viovu wanavyofanyiwa waislamu wa Tajikistan Masoud ameitahadharisha dola hiyo na kusema iwapo hasara itatokea itarejea upande wa taifa hilo na kusema chama hicho kitajitolea kulingania utukufu wa mwezi mungu.

Amesema serikali ya Tajikistan inafanya makosa hayo huku ikiungwa mkono na madola ya magharibi na taasisi zinazodai kutetea haki za binadamu zikiwa zimekaa kimya.

Masoud amefahamisha zaidi ya waislamu 300 wa Tajikistan wanaendelea kusulubiwa kwa mateso, uonevu na vifungo vya muda mrefu.

Amesema Hiz ut-Tahrir Afrika Mashariki inalaani mateso na uharamia wanaofanyiwa waislamu wasiokuwa na hatia na utawala wa nchi hiyo  unaongozwa na rais Rahmanov.

Jumuiya ya Hiz ut-Tahrir ni chama cha kislamu cha kimataifa chenye malengo ya kurejesha tena uislamu kupitia dola ya Helaf iliyoangushwa mwaka 1924.

RAIS KARUME AFUNGUA NYUMA YA WATOTO YATIMA ZANZIBAR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Amani Abeid Karume,akifungua pazia kama ishara ya Uzinduzi wa Nyumba mpya ya watoto Yatima iliyopo Mazizini nje ya Mji wa Zanzibar

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dr. Amani Abeid Karume amewataka wazazi na walezi kuchukuwa tahadhari ya kutowachia watoto wao kudhubaa mitaani.

Akifungua nyumba mpya ya kulelea watoto huko Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar mesema tabia hiyo itawajenga watoto kuishi maisha ya taabu na yasiokuwa na malengo yao ya baadae.

Dr. Karume amesema serikali ya Mapinduzi Zanzibar haiwezi kuiachia hali hiyo ikitokea kwa vile wazanzibari wote ni familia moja na wanadhamana ya kuwalea watoto wote.

Amesema mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 rais wa kwanza Abeid Karume ameanzisha kituo cha kulelea watoto huko Forodhani ili kuona watoto hao wanalelewa katika mazingira mazuri

Aidha Dr. Karume amesema serikali imeamuwa kuwahamisha watoto wanaolelewa katika kutuo cha Forodhani kutokana na mazingira yaliopo katika eneo hilo hayafai tena kulelea watoto.

Amesema jengo hilo la Forodhani litaendelea kuwa mali ya serikali na kutumika kwa shughuli za makumbusho ya usafiri wa bahari ya Hindi chini ya usimamizi wa taasisi ya Agakhan Foundation.

Akizungumza katika ufunguzi wa kituo hicho katibu wa afisi ya Mufti mkuu Zanzibar Sheikh Fadhili Soraga amewataka waislamu kuendelea kuwatunza watoto yatima kulingana na mafundisho ya dini yao.

Amesema watu wanaowadhulumu watoto yatima kwa kula mali zao ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini ya kislamu na watu hao tayari wameshabashiriwa kuingia motoni

Nyumba hiyo mpya ya kulelea watoto yenye ghorofa moja, vyumba vya kuishi watoto 80 kwa wakati mmoja, ukumbi wa mikutano, vyumba vya kompyuta, kusomea, na zahanati ujenzi wake umesimamiwa na taasisi ya ZAYADESA na kugharimu zaidi ya shilingi milioni 883.

MGOMBEA URAIS WA ZANZIBAR KUPITIA CCM DR. SHEIN AREJESHA FOMU

Dr. Ali Mohammed Shein

Mgombea wa urais Zanzibar kupitia CCM Dr. Ali Mohammed Shein amesema ataitumikia Zanzibar kwa ufanisi mkubwa na kuweka mbele maslahi ya wananchi.

Akizungumza na wana CCM huko Kisiwandui muda mfupi baada kurudisha fomu za kuwania nafasi hiyo katika tume ya uchaguzi Zanzibar amesema atashirikiana vizuri na viongozi watakaokubali kufanyakazi kwa maslahi ya Zanzibar.

Aidha Dr. Shein ameonya kuwa hatamvumilia kiongozi yoyote ambae atakwenda kinyume na matakwa ya Wazanzibar endapo ataingia madarakani ……

Dr. Shein amesema katika uchaguzi ujao, CCM imejiandaa kuendesha kampeni za kistaarabu zenye kuwaelekeza wananchi malengo ya chama hicho ili wakipe ridhaa tena ya kuiongoza Zanzibar.

Nae naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar Saleh Ramadhan Ferouz amewataka wafuasi wa chama hiho kupuuza matamshi yanayotolewa na baadhi ya watu kwamba kumtilia kura kiongozi wa upinzani ni sawa na kumpigia mgombea wa CCM.

Amesema watu hao wanaopotosha wana CCM kwa kusambaza vipeperushi vyenye ujumbe huo, amewataka wafuasi wa chama hicho kuwa makini juu ya mbinu hizo zinazofanywa na vyama vya upinzani.

Dk . Shein anakuwa mgombea wa pili kurejesha fomu zake kwa tume ya uchaguzi Zanzibar kati ya wagombea wanane waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Octoba 31 mwaka huu.