Dr. Wilbord Slaa

Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimejitokeza kumuunga mkono mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha wananchi CUF, Seif Sharif Hamad katika uchaguzi mkuu ujao.

Mgombea urais wa Tanzania wa CHADEMA Dr. Wilbord Slaa amesema uwamuzi huo umechukuliwa kwa lengo la kukiongezea nguvu chama hicho ili kushindana na CCM katika uchaguzi wa urais wa Zanzibar

Dr. ambae alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara wa kutafuta wadhamini huko Kibandamaiti mjini hapa amedai Tanzania imejaa ufisadi unaosababisha watanzania kupoteza haki zao zikiwemo ardhi ambao hayana mtetezi.

Amesema suala la maisha bora linalodaiwa na viongozi walioko madarakani bado halijaleta maslahi kwa wananchi hivyo linahitaji mabadiliko hasa katika kudhibiti mfumko wa bei za bidhaa.

Dr. Slaa amesema CHADEMA bado inaendelea kutetea sera ya kuwa na serikali tatu ili wazanzibari na watanzania bara wawe na maamuzi katika mambo yao wanayowahusu.

Amesema chama chake kitaisimamia sera hiyo kwa vile nchi nyingi duniani zilizoungana hazina mfumo wa serikali mbili kama ilivyo Tanzania hali ambayo inainyima Zanzibar fursa za kimataifa ikiwemo misaada na mikopo

CHADEMA kimekuwa chama cha siasa cha pili kutangaza hadharani kumuunga mkono mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia CUF Malim Seif Sharif Hamad baada ya chama cha APPT-maendeleo kutangaza kufanya hiyo.

Advertisements