Rais Amani Abeid Karume

Ukuwaji wa uchumi wa Zanzibar unakabiliwa na ongezeko la idadi ya watu. Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dr. Amani Abeid Karume amesema licha ya uchumi wa Zanziar kupata mafanikio, lakini  unaendelea kuathiriwa na kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watu.

Amesema juhudi maalum zinahitaji ili kuona onezeko la idadi ya watu linakwenda sambamba na ukuwaji wa uchumi pamoja na kudhibiti kuzuwia athari za kimazingira zinazosababishwa na ongezeko hilo.

Akilihutubia baraza la wawakilishi rais Karume ametaja baadhi ya mafanikio ya ukuwaji wa uchumi nchini ni pamoja na ukuwaji wa pato la taifa kutoka shilingi bilioni 349.9 mwaka 2005 hadi bilioni 878.4 mwaka 2009.

Amesema kutokana na ukuwaji huo wastani wa pato la mtu binafsi limeongezeka kutoka shilingi laki tatu na elfu 68 mwaka 2005 hadi shilingi laki saba na elfu 28 sawa na dola za Marekani 557 kwa mwaka.

Aidha rais Karume amesema serikali yake katika kipindi cha miaka mitano imepata mafanikio makubwa katika sekta ya afya, elimu, miundo mbinu ya uchumi,  ukusanyaji wa mapato, maji safi na nishati.

Akizungumzia hali ya kisiasa Zanzibar ameitaka tume ya uchaguzi, vyama vya siasa na wananchi kuungana ili kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unaandika historia mpya inayoendana na maridhiano ya kisiasa

Amesema matumaini ya wazanzibari ni kuwa na uchaguzi safi na huru ili kufanikisha kiu yao ya maendeleo ya kijamii, utulivu wa kisiasa na ukuwaji wa uchumi wenye tija.

Katika hutuba hiyo ya kukamilika miaka mitano ya baraza la saba la wawakilishi rais Karume ametangaza kuanzia Ijumaa ijayo baraza hilo limevunjwa rasmi

Advertisements