Moja ya ndege ya shirika la ADAC

KAMPUNI ya viwanja vya ndege ya Abudhabi (ADAC) imeeleza nia yake ya kuekeza katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Karume Zanzibar na kueleza namna ilivyovutiwa na hatua zilizofikiwa katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini.

Rais wa Kampuni hiyo, Bwana Jeff Reynolds alieleza hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume, Ikulu mjini Zanzibar.

Katika maelezo yake, Bwana Reynolds ambaye alifika Ikulu na ujumbe wake, alimueleza Rais Karume kuwa Kampuni ya ADAC imevutiwa na mazingira ya Zanzibar sanjari na maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimaitaifa wa Zanzibar.

Kiongozi huyo wa Kampuni ya ADAC,alimueleza Rais Karume kuwa tayari kampuni yake hiyo kwa mashirikiano na Idara ya Anga na Wizara husika ya mawasiliano zimo katika mchakato wa kufanikisha zoezi hilo.

Alieleza kuwa Kampuni ya ADAC ambayo ni Kampuni ya Kiserikali inashughulikia viwanja mbali mbali vya ndege katika ukanda wa nchi za Kiarabu.

Bwana Reynols, alieleza imani yake kuwa uwanja wa ndege wa Kimataifa uko imara na unakubalika kimataifa.

Pamoja na hayo, Bwana Reynolds alieleza kuwa mafanikio ya utanuzi wa barabara ya uwanja wa ndege wa Zanzibar sanjari na ujenzi wa jengo jipya la abiria katika kiwanja hicho cha ndege kutaimarisha sekta ya utalii.

Alieleza kuwa ni imani yake kubwa kuwa sekta ya utalii hapa Zanzibar itaimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na nia hiyo ya kuekeza hapa nchini. Aidha Kiongozi huyo alimueleza Rais Karume lengo la Kampuni hiyo kuzivutia Kampuni za ndege za Arabuni kufanya safari zake hapa Zanzibar.

Nae Rais Karume alimueleza kiongozi huyo na ujumbe wake kuwa lengo na madhumuni ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha miundombinu ya barabara ikiwemo barabara ya kutulia na kurukia ndege ni kukuza uchumi na kuimarisha maendeleo endelevu yaliopatikana hapa nchini.

Rais Karume alieleza kuwa kuimarika kwa uwanja wa ndege ni jambo moja wapo linalopelekea kuimarika kwa maendeleo na uchumi wa nchi, hivyo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuimarisha uwanja wake wa ndege ni njia moja wapo ya kuimarisha uchumi wake.

Katika maelezo yake, Rais Karume alitoa shukurani kwa Kampuni hiyo kwa kuja Zanzibar na kujionea wenyewe hatua zilizofikiwa katika uimarishaji wa uwanja wa ndege sanjari na kutangaza nia yake ya kuekeza katika kuimarisha shughuli za kiwanja cha ndege cha Zanzibar.

Rais Karume alisema kuwa sekta ya Utalii ni sekta muhimu hapa nchini na kuimarika kwa shughuli za uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar kutasaidia kukuza sekta hiyo hapa nchini.

Aidha, Rais Karume alisema kuwa mbali ya sekta ya utalii, sekta ya biashara ina nafasi kubwa hapa Zanzibar ambayo imekua kwa kiasi kikubwa na kusisitiza kuwa kuimarika kwa safari za ndege kutoka mashirika ya ndege ya Arabuni kuja Zanzibar yatasaidia kwa kiasi kikubwa hapa nchini.

Rais Karume alieleza kuwa ni imani yake kubwa kuwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar utapata mafanikio makubwa hivi sasa na hata hapo baadae kutokana na mikakati madhubuti inayowekwa katika kuuimarisha uwanja huo wa ndege.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya sita iliendeleza lengo la kuipatia suluhisho la kudumu barabara ya kurukia na kutulia ndege katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Karume Zanzibar .

Matengenezo makubwa yamefanywa kwa barabara iliyokuwepo awali ambayo ilikuwa na mita 2462 na kuiongeza kwa urefu wa mita 560 kufikia mita 3022. Serikali ilichukua juhudi za makusudi kwa kushirikiana na Benki ya Dunia katika matengenezo ya marabara hiyo.

Advertisements