Watu watatu wamefariki dunia na wengine sita wamenusurika baada ya mashua waliokuwa wakisafiria kuzama katika eneo la Sumbe karibu na nchi jirani ya Kenya katika bahari ya Hindi.

Watu hao waliokuwa katika mashua hiyo ijulikanayo Twiga walikuwa wakifanya biashara ya pweza kutoka kisiwani Pemba na kupeleka nchini Kenya.

Kamanda wa polisi mkoa wa kaskazini Pemba Yahya Rashid Bugi amewataja waliofariki dunia ni Othman Abdalla mkaazi wa Migurani, Juma Amin na mwengine aliyefahamika kwa jina moja la Mtumwa wote wakaazi wa Kenya.

Kamanda Bugi amesema mashua hiyo ilikuwa ikitokea katika bandari ya Mchangamle Makangale wilaya ya Micheweni kuelekea Shimoni Mombasa.

Amesema mara baada ya kupata taarifa za tukio hilo walienda eneo la tukio na kukutana na mmiliki wa chombo Hakimu Makame Shaame ambae alithibithisha kutokea kwa tukio hilo.

Amesema wakati wa tukio hilo chombo hicho kilikuwa na wafanyakazi sita na abiria watatu ambapo kiliondoka Makangale juzi jioni kuelekea nchini Kenya katika shughuli zake za kila siku.

Chombo hicho kilizama kutokana na upepo mkali uliovuma na kusababisha kubiruka na kuzama karibu na mlango wa kuingilia Shimoni Mombasa nchini Kenya.

Advertisements