Seif Sharif Hamad

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha wananchi CUF Seif Sharif Hamad amevitolea wito vyombo vya ulinzi na usalama kutoegemea upande wowote wakati wa uchaguzi na badala yake kuheshimu maamuzi ya wananchi.

Amesema chaguzi zilizopita baadhi ya vyombo vya dola vimejingiza katika harakati za uchaguzi na kusahau majukumu yao ya kulinda usalama, hivyo amezitaka taasisi hizo kujiepusha na vitendo hivyo vinavyoweza kuchafua uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar katika afisi za tume ya uchaguzi Hamad amesema vikosi vya ulinzi na usalama havina jukumu la kuamuwa nani anaongeze nchi, lakini katiba ndio inayotoa fursa kwa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka….

Aidha Hamad amesema chama cha CUF kitaendesha kampeni za kiungwana ili kuendeleza maridhiano ya kisiasa na hakitaruhusu mgombea wake kutoa maneo ya matusi au kuchafua kampeni za uchaguzi.

Amesema katika kampeni hizo chama chake kitafuata ilani ya uchaguzi ya kushindana kwa hoja na kuvitaka vyama vingine kujiepusha na kampeni za kupakana matope.

Wakati huo huo mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia chama cha Wakulima Said Soud nae amejitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo katika afisi za tume ya uchaguzi Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu hizo amesema chama chake kitashiriki katika uchaguzi huo ili kuotoa ushindani kwa vyama vingine vya siasa

Maalim Seif na Soud ni miongoni mwa wagombea wa nne waliojitokeza kuchukua fomu leo baada ya wiki iliyopita Haji Ambar Khamis kutoka NCCR-MAGEUZI na Juma Ali Khatib kutoka TADEA kuchukua fomu.

Uchaguzi mkuu wa Zanzibar ambao unatarajiwa kuwashirikisha wagombea wa nafasi ya urais sita unatarajiwa kufanyika Octoba 31 mwaka huu na mshindi atakaeshinda atalazimika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Advertisements