Makamo wa rais Dr. Ali Mohammed Shein

Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Dr. Ali Mohammed Shein amesema serikali ya CCM haitakubaliana na kiongozi atakaekuwa serikalini kwa kutumia madaraka kwa maslahi yake binafsi.

Akizungumza na wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani huko hoteli ya Bwawani  amesema ukimya wake hautamfanya kuwa mlegevu katika utekelezaji wa majukukumu yake.

Dr. Shein ambae ni mgombea urais wa Zanzibar amewaahidi wanachama hao endapo atapata ushindi atahakikisha anaendesha nchi kwa misingi ya haki, upendo na maelewano huku suala la nidhamu ndio msingi wa wananchi kujikwamua kimaisha.

Amesema viongozi wenye tabia ya kuendeleza chuki na kupenda madaraka hatowapa nafasi kwa vile mambo hayo  yanachangia kuzusha mifarakano ndani ya jamii ya wazanzibari..

Aidha Dr. Shein amewataka wana CCM kusafisha nyoyo zao na kuondokana na chuki na ubinafsi zilizojitokeza katika kinyanganyiro cha urais, ubunge, uwakilishi na udiwani katika kura za maoni.

Amesema wanachama wa CCM wanapaswa kukusanya nguvu zao katika kukipatia ushindi chama hicho na utaratibu wa kura za maoni ulikuwa muhimu katika kutafuta viongozi ndani ya chama.

Nae naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar Saleh Ramadhan Ferouz amesema chama hicho kitaendesha kampeni za zinazotarajiwa kuanza mwezi ujao kuelezea mafanikio ya ilani ya uchaguzi na sio kuelezea kero.

Amesema CCM imeweza kutekeleza ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2005 kwa asilimia kubwa hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kiuchumi na kijamii pamoja na kutekeleza utawala bora ambapo katika kipindi hicho hakukuwa na mfungwa wa kisiasa

Advertisements