Chama cha Jahazi Asilia kimesema suala la ufisadi kwa Zanzibar bado ni dogo ikilinganishwa na nchi nyingine duniani kutokana na kuwa na vyanzo vichache vya mapato.

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho Kassim Ali Bakar amesema hayo huko tume ya uchaguzi Zanzibar wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.

Amesema Zanzibar inategemea zaidi sekta ya utalii na karafuu kama mihimili wa uchumi, hali iliyosababisha kuwa na pato dogo lisilozidi shilingi bilioni moja kwa mwezi

Mgombea huyo amesema endapo chama chake kitaongeza Zanzibar katika uchaguzi ujao kitaanza kupiga vita ufisadi huo mdogo kabla ya kuanzisha vianzio vikubwa vya ukusanyaji wa mapato.

Aidha amesema mabadiliko ya katiba yaliofanywa hivi karibuni na baraza la wawakilishi yamekisaidia chama hicho kuifanya Zanzibar kuwa na sera yake ya kiuchumi badala ya kutumia sera ya muungano.

Bakar amesema matatizo yaliomo ndani ya muungano yanaendelea kuathiri uchumi wa Zanzibar na kuonekana tofauti na uchumi wa Tanzania bara, hivyo asema suluhisho lake ni kuunda serikali tatu.

Amesema mwelekeo wa Jahazi Asilia katika mfumo mpya wa serikali ijayo ya umoja wa kitaifa ni kuendeleza uzanzibari na maridhiano ya kisiasa yaliofikiwa hivi karibuni

Hadi sasa jumla ya wagombea saba wa vyama vya siasa  wamejitokeza kuchukua fomu za  kuwania urais wa Zanzibar ambao ni kutoka chama cha CCM, CUF, AFP, SAU, NCCR-Mageuzi na Jahazi Asilia, huku chama cha NRA kimejitoa kutokana na mgombea wake Rashid Ahmmed Joy kuugua shindikizo la damu.

Advertisements