Rais Jakaya Kikwete

Mgombea urais wa Tanzania kupitia chama cha Mapinduzi rais Jakaya Mrisho Kikwete amelazimika kukatisha hutoba yake ya ufunguzi wa kampeni muda mfupi kutokana na matatizo ya afya.

Hata hivyo rais Kikwete alirejea tena jukwani, lakini alichukua muda mfupi kuendelea na hutuba hiyo hali iliyowashangaza wananchi na wana CCM waliohudhuria uzinduzi wa kampeni…..

Hata hivyo bado hakujatolewa taarifa rasmi nini kilichomsibu rais Kikwete kutoendelea na hutuba yake hiyo ambayo alitarajiwa kuchukua muda mwingi kuzungumza mambo mengi kama ilivyo kawaida yake.

Hii ni mara ya pili kwa rais Kikwete kushindwa kuendelea kutoa hutuba za kampeni za uchaguzi kwa chama chake wakati akiwa jukwani ambapo mara ya kwanza ilimtokezea hali hiyo katika kampeni za 2005.

Akifungua kampeni hizo rais Kikwete amewataka wananchi kuendelea kukiunga mkono chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao ili kuendeleza sera zake za kuwaletea maendeleo wananchi.

Amesema serikali za CCM zimefanikiwa kulinda usalama wa raia na mali zao, utawala bora, usimamizi wa mapato, kuheshimu uhuru wa watu, mapambano dhidi ya rushwa na uhuru wa kuabudu.

Amesema endapo CCM itapata ridhaa tena ya wananchi kuongoza itafanya mambo mengi zaidi, hivyo ni vyema kwa wananchi kuendelea kukiunga mkono chama hicho.

Rais Kikwete amesema chama cha CCM kimetimiza ahadi zake ilizozitoa kwa wananchi wakati ikiomba ridhaa ya kuongoza mwaka 2005, lakini yako machache ambayo hayajatekelezwa kutokana na sababu za kimsingi zinzaokubalika.

Nae makamo mwenyekiti wa CCM, Zanzibar rais Amani Abeid Karume akizungumza katika kampeni hizo amesema chama cha Mapinduzi bado kinahitajika kuiongoza Tanzania, kutokana na kufikia maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii ambayo misingi yake imwekwa katika ilani zake za uchaguzi.

Rais Karume amesema CCM imeweka wagombea wake makini katika nafasi za urais, ubunge na udiwani hivyo ni vyema kwa wananchi na wana CCM kuwaunga mkono wagombea hao

Advertisements