Balozi wa Marekani Alfonso akitembelea studio ya Zenji Fm Radio kabla ya kufanya mahojiano na radio hiyo binafsi

Serikali ya Marekani imesema wananchi wa Zanzibar wanapaswa kushikamana katika kuijenga upya nchi yao baada ya kukubali kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kupitia kura ya maoni.

Akizungumza na Zenji fm Radio balozi wa Marekani nchini Tanzania Alfonso Lenhert’s amesema hatua hiyo iliyochukuliwa na wananchi wa Zanzibar itasaidia sana kudumisha uhusiano wa nchi mbili hizo.

Amesema azma ya Marekani ni kuendelea kuisaidia Zanziar katika miradi ya maendeleo ambayo nchi hiyo imekuwa ikitoa misaada yake kama vile mradi wa umeme unaofadhiliwa na shirika la Millenium Challenge.

Aidha balozi Alfonso amesema Marekani inatarajiwa kuisaidia Zanzibar kutekeleza mradi mpya wa karne ya 21 wa elimu ya msingi na mafunzo ya amali utakaozinduliwa hivi karibuni.

Amesema mradi huo utawasaidia wanafunzi kujua na kutumia kompyuta wakiwa katika skuli za msingi, kunyanyua somo la hesabati pamoja na utowaji wa mafunzo kwa walimu wa skuli za msingi.

Marekani pia imetoa misaada kwa Zanzibar katika sekta ya afya ukiwemo mradi wa kukataa malaria, kukabiliana na tatizo la ukimwi na kifua kikuu, utowaji wa vitabu vya sayansi kwa skuli za sekondari na maeneo mengine ya kiuchumi na kijamii.

Kufuatia kura ya maoni iliyopigwa na wanachi wa Zanzibar iliykubali kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa zaidi ya asilimia 60 nchi nyingi za wahisani na mashirika ya kimataifa yameipongeza Zanzibar kwa hatua yake hiyo.

Advertisements