Rais wa Marekani Barack Obama

RAIS wa Marekani Barack Obama ametoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Amani Abeid Karume kutokana na mafanikio ya kisiasa yaliofikiwa Zanzibar.

Pongezi hizo zilitolewa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bwana Alfonso Leinhardt kwa niaba ya Rais Obama, Ikulu mjini Zanzibar na kueleza kuwa miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kupatikana ridhaa ya Wazanzibari katika uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar.

Katika maelezo yake, Bwana Leinhardt alimueleza Rais Karume kuwa hatua hiyo imeonesha wazi kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa kidemokrasia na ndio sababu kubwa iliyomvutia Rais Obama.

Bwana Leinhardt alisema kuwa Marekani inamatumaini makubwa kuwa Zanzibar itazidi kupata maendeleo endelevu kutokana na mafanikio hayo yaliofikiwa sanjari na uongozi imara wa Serikali ya Mpinduzi Zanzibar.

Balozi huyo wa Marekani alimuhakikishia Rais Karume kuwa Marekani itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi mbali mbali ya maendeleo.

Akieleza juu ya mradi wa teknolojia ya kompyuta kwa wanafunzi wa skuli za Zanzibar, Balozi Leinhardt alimueleza Rais Karume kuwa nchi yake itasaidia kuendeleza mradi huo ambao utakuwa kwa Tanzania nzima lakini Zanzibar imechaguliwa kuwa ni sehemu ya kuanzia.

Katika mradi huo lengo ni kumfanya kila mwanafunzi kuwa na kompyuta yake kwa ajili ya kujisomea pamoja na kupata elimu zaidi kupitia kifaa hicho.

Aidha, Balozi Leinhardt alieleza kuwa mbali ya nchi yake kutoa misaada mikubwa katika kuimarisha miradi ya maendeleo hapa Zanzibar kupitia MCC, ikiwemo ujenzi wa baadhi ya barabara kisiwani Pemba pamoja uwekaji wa umeme mpya kutoka Dar-es-Salaam hadi Zanzibar, nchi yake itaendelea kuisaidia zaidi Zanzibar.

Balozi Leinhardt alisisitiza kuwa katika nchi nyingi duniani ambazo zimepata maendeleo juhudi kubwa zimefanywa katika kuimarisha sekta ya nishati na elimu ambazo kwa Zanzibar ni miongoni mwa sekta ambazo zimepata mafanikio makubwa na zimeimarika kwa kiasi kikubwa.

Kutokana na hatua hiyo, Balozi huyo alisema kuwa Marekani inathamini juhudi hizo za Zanzibar na kusisitiza kuwa itaendelea kuwasaidia wananchi wa Zanzibar katika maendeleo yao.

Sambamba na hayo, Balozi Leinhardt alitoa pongezi kwa Rais Karume kwa uongozi wake imara uliopelelea Wizara zote zilizo chini ya  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupata mafanikio mazuri chini ya Mawaziri wake pamoja na  watendaji wake wengineo.

Nae Rais Karume alimueleza Balozi Leinhardt kuwa mafanikio hayo ya kisiasa yaliopatikana Zanzibar si ya viongozi pekee yao bali ni ya Wazanzibari wote.

Rais Karume alieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanajivunia amani na utulivu iliopo nchini mwao na ndio maana waliamua kuuendeleza utamaduni huo kwa lengo la kuimarisha umoja na mshikamano wao.

Alieleza kuwa Wazanzibari wenyewe waliona jinsi nchi yao inavyokuwa wakati wakikaribia kuingia kwenye uchaguzi mkuu ambapo utulivu na mshikamano hupotea kiasi ambacho husababisha kukosekana kwa amani na ndio maana wakaamua kutafuta njia ya kuimarisha umoja na mshikamano wao.

Rais Karume alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini uhusiano, ushirikiano na misaada mbali mbali ya kimaendeleo inayotolewa na Marekani na kuahidi kuwa Zanzibar itaendeleza ushirikiano huo.

Katika mazungumzo hayo, Rais Karume Karume alisema kuwa Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa katika kupiga vita Malaria ambapo juhudi za Serikali ya Watu wa Marekani zilisaidia katika kuunga mkono na hatimae kupata mafanikio makubwa.

Akieleza katika mafanikio yaliopatikana kwenye sekta ya elimu, Rais Karume alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo hivi sasa ni kuimarisha elimu ya Sekondari ambapo tayari mikakati maalum imeshawekwa katika kufanikisha changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kujenga skuli mpya za kisasa Unguja na Pemba.

Rais Karume alisema kuwa katika kuhakikisha kila mwanafunzi anapata kitabu chake cha kujisomea tayari hatua hiyo imefikiwa na kuishukuru Serikali ya Marekani kwa msaada wake wa vitabu.  Aidha, Rais Karume alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar tayari imeshapiga hatua kubwa katika kutekeleza malengo ya Milenia kwa kuweza kuimarisha sekta zake za maendeleo

Advertisements