Rais Karume akifanya uzinduzi wa mmoja wa miradi ya maendeleo

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume, amesema kuwa juhudi za makusudi za kupambana na umasikini  na kukuza uchumi zimechukuliwa hapa Zanzibar kupitia MKUZA  na kuweza kupata mafanikio makubwa.

Rais Karume aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa Mabalozi wa Heshima wanaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nje ya nchi,  yaliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Rais Karume alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupambana na Umasikini, MKUZA umeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika suala zima la kupambana na umasikini na kukuza uchumi hapa Zanzibar.

Rais Karume alieleza kuwa juhudi za makusudi zimeweza kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuhakikisha maendeleo endelevu yanaimarika nchini kwa kuweza kuimarisha Mkakati huo.

Rais Karume alisema kuwa Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa katika kuimarisha miradi yake ya maendeleo hatua ambayo imeweza kustawisha ustawi wa jamii na ukuzaji uchumi.

Aidha, Rais Karume aliueleza ujumbe huo kuwa mafanikio makubwa yameweza kupatikana Zanzibar katika sekta zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Akieleza kwa upande wa sekta ya utalii, Rais Karume alisema kuwa Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika sekta hiyo ambayo hivi sasa imekuwa ni muhimili mkuu wa uchumi.

Alieleza kuwa wawekezaji mbali mbali wameweza kuekeza Zanzibar katika sekta ya utalii ambayo imeonekana kuimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Rais Karume pia, aliupongeza ujumbe huo wa Mabalozi wa Heshima kwa ujio wao hapa Zanzibar sanjari na mafunzo waliyoyayapata ya wiki moja yaliyofanyika hapa nchini.

Pamoja na hayo, Rais Karume aliueleza ujumbe huo kuwa ujio wao umekuja wakati muwafaka ambapo Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa katika kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wake kwa lengo la kujipatia maendeleo endelevu kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Nae kiongozi wa ujumbe huo wa Mabalozi wa Heshima, Balozi Dallas Browne alimueleza Rais Karume jinsi ujumbe huo ulivyofarajika kufika Zanzibar na kujionea hatua mbali mbali za maendeleo zilizofikiwa.

Dk. Dallas alieleza kuwa  hatua za maendeleo yaliyofikiwa Zanzibar ni ya kujivunia na kuyatangaza ndani na nje ya nchi.

Aidha, ujumbe huo ulipongeza mafanikio yote ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yaliyopatikana Zanzibar.

Pamoja na hayo, ujumbe huo ulimpongeza Rais Karume kwa hatua na juhudi kubwa za maendeleo zilizofikiwa Zanzibar, chini ya uongozi wake.

Advertisements