Archive for September, 2010

WATOTO WANAOISHI NA VIRUSI VYA UKIMWI ZANZIBAR INAONGEZEKA

Baadhi ya watoto wanaoishi na virusi vya ukimwi wakipatiwa huduma

Idadi ya watoto yatima ambao wazazi wao wamekufa kutokana na ugonjwa wa ukimwi imeongezeka kutoka mia mbili na 50 mwaka uliopita hadi kufikia mia sita na 68 Unguja na Pemba.

Mwenyekiti wa jumuiya ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi Zanzibar ZAPHA PLUS Consolata John amesema miongoni mwa watoto hao mia mbili na 30 wanaishi na virusi vya ukimwi.

Akizungumza na Zenji Fm radio huko afisini kwake amesema idadi hiyo inaweza kuongezeka kutokana na walezi wao kutojitokeza kuwasajili watoto wanaoishi na virusi vya ukimwi kwa jumuia hiyo ili kupatiwa misaada.

Amesema watoto wanaoishi na virusi vya ukimwi waliosajiliwa na jumuia hiyo hupatiwa huduma za matibabu kama vile dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa ukimwi na kujengewa uwezo wa kisaikolojia

Jumla ya watu elfu moja na 600 wanaoishi na virusi vya ukimwi Zanzibar wamejiandikisha katika jumuiya hiyo ambao hupatiwa ushauri nasaha, dawa za kupunguza makli ya ukimwi na matibabu

Advertisements

KESI YA MTANZANIA AHMED GHAILANI ANAETUHUMIWA KWA UGAIDI IMEANZA NCHINI MAREKANI

Mtanzania, Ahmed Khalfan Ghailani

Kesi ya kwanza inayomkabili mfungwa wa zamani wa gereza la Guantanomo imeanza tangu jana kwa uteuzi wa jopo la wazee wa mahakama katika mahakama ya shirikisho mjini New York. Ahmed Ghailani, Mtanzania anayeshitakiwa kwa kuhusika na mashambulio ya mabomu ya mwaka 1998 katika balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya, amekana mashtaka yanayomkabili ya kuwaua watu 224 wakiwemo raia 12 wa Marekani.

Kesi hiyo inasikilizwa wakati Rais Barack Obama wa Marekani akijitahidi kutimiza ahadi yake ya kuifunga jela ya Guantanamo Bay iliyoko Cuba na kuwafikisha watuhumiwa wa ugaidi mahakamani kwa kufuata taratibu za kawaida za mahakama.

Kesi ya Ghailani huenda ikaleta ushawishi katika kesi ya Khalid Sheikh Mohammed kiongozi aliyekiri kuhusika na mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11, mwaka 2001 mjini New York na Washington. Hata hivyo, Ghailani amekanusha kuhusika na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, kundi linalodaiwa kuhusika na mashambulio katika balozi hizo na yale ya Septemba 11.

Haramia wa Kisomali akamatwa Tanzania

Maharamia wa KisomaliMaharamia wa Kisomali

Jeshi la Tanzania limesema limemkamata mshukiwa mmoja wa Uharamia raia Somalia, kufuatia makabiliano makali ya ufyatulianaji wa risasi katika bahari ya Hindi.

Ripoti zinasema tukio hilo lilitokea siku ya Jumapili iliyopita katika eneo la Kusini mwa pwani ya Tanzania, eneo ambalo meli ya kampuni ya kuchimba mafuta ya Ophir inafanya utafiti ili kubainisha ikiwa eneo hilo lina utajiri wa mafuta ya Petroli.

Msemaji wa jeshi la wanamaji nchini Tanzania, Steve Buyuya, amesema manuawari ya kijeshi ilishambuliwa kwa risasi na maharamia waliokuwa kwenye mashua ndogo.

Lakini baada ya ufyatulianaji wa risasi uliodumu kwa muda, maharamia kadhaa walifanikiwa kutoroka huku mmoja wao akikamatwa na wanamaji wake.

MABAHARIA WA ZANZIBAR KUADHIMISHA SIKU YA MABAHARIA DUNIANI

Chama cha mabaharia Zanzibar kinaungana na vyama vingine duniani vya mabaharia katika kuadhimisha siku ya usafiri wa baharini.

Akizungumza na Zenji Fm radio katibu mkuu wa chama cha mabaharia Zanzibar Abrahaman Chande amesema hii ni mara ya kwanza kwa Zanziar kuadhimisha sherehe hizo.

Amesema maadhimisho hayo yatajumuisha shughuli za kazi za meli duniani kwa kufanya ukaguzi wa usalama wa meli, kuandaa kongamano litakalozungumzia masuala ya usalama, utunzaji wa mazingira baharini, haki za mabaharia na kutoa elimu ya kujikinga na ukimwi.

Chande ambae pia ni mwenyekiti wa mwenyekiti wa shirikisho la usafiri duniani kanda ya Afrika amesema mwaka 2010 umetangazwa kuwa wa mabaharia duniani ambapo mabaharia wa Zanziar watatambuliwa mchango wao katika kuchangia uchumi

PROFISA LIPUMBA APATA AJALI TANGA

Profisa Ibrahim Lipumba

Msafara wa mgombea urais wa jamhuri ya muungano Tanzania kupitia chama cha wananchi CUF Profisa Ibrahim Harouna Lipumba umepata ajali leo asubuhi mkoani Tanga.

Ajali hiyo imetokea katika eneo la Handeni imehusisha magari mawili ya yaliokuwa katika kampeni, moja ilimbeba meneja wa kampeni na mgombea urais Profisa Lipumba na nyingine jingine limewabeba wandishi wanne wa habari.

Ajali hiyo imetokea baada ya gari hilo la mgombea kuchomoka tairi na kupoteza mwelekeo. Hata hivyo mgombea huyo na meneja wa kampeni Saidi Miraj hawakupata majeraha, lakini walikimbizwa hospitali kwa ajili ya kuangaliwa afya zao.

Gari ya waandishi wa habari wanne ilipinduka mara mbili, lakinihakuna mwandishi hata mmoja aliepata majeraha makubwa

MUASISI WA MAPINDUZI ZANZIBAR SAID ABDALLA NATEPE AMEFARIKI DUNIA

Waasisi wa mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964

Mmoja wa viongozi 14 wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar,Meja Jenerali Abdallah Said Natepe amefariki dunia jana mchana katika hospitali yajeshi  Lugalo mjini Dar es Salaam.

Marehemu Natepe ni miongoni mwa viongozi wa mapinduzi kumbi na mbili waliofariki dunia ambao walifanikisha kufanikiwa kwa mapinduzi ya Januari 12, 1964 yaliyoindoa serikali ya kisultani visiwa vya Zanzibar,

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, kifo hicho kimetokea jana mchana kwenye hospitali hiyo kuu ya Jeshi la Wananchi.
Taarifa hiyo inamnukuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete akieleza kushtushwa na kuhuzunishwa na kifo cha mwanamapinduzi huyo na kumtumia salamu za rambirambi katibu mkuu wa CCM akielezea jinsi alivyoguswa na kifo hicho cha Mzee Natepe.

“Kifo kimemchukua mwanamapinduzi, mzalendo na mwanachama wetu mwaminifu katika kipindi ambacho taifa na chama bado kinamhitaji sana. Kifo kimetunyang’anya tunu wakati huu tunaoelekea uchaguzi mkuu; ni huzuni kubwa kwetu; ni majonzi makubwa na hatuna neno kubwa linaloweza kuelezea huzuni hii,” Rais Kikwete anakaririwa kwenye taarifa hiyo.

Rais alipokea taarifa za kifo cha Mzee Natepe jana mchana akiwa Njombe mkoani Iringa ambako yuko kwa ajili ya shughuli za kampeni.

Rais Kikwete pia ametuma salaamu za rambirambi kwa familia, ndugu na jamaa wa Marehemu Natepe.

“Mzee Natepe amekuwa sehemu ya maisha yangu ya kisiasa, kijamii na amenipa malezi na maelekezo mengi nikiwa kama kijana wake na amekuwa moja ya nguzo yangu kubwa katika shughuli zangu za kisiasa na kikazi katika maeneo yote niliyotumikia nchi yangu,” alisema rais na kuelezea kwa masikitiko huzuni aliyonayo na kuwahakikishia kuwa yuko nao katika kipindi hiki kigumu.

“Tunamshukuru mwenyezi Mungu kwa kutupa nafasi ya kuishi na Mzee Natepe na kufanya naye kazi. Tunamuomba Mungu amlaze mzee wetu mahali pema peponi na kumpa pumziko la milele, amina”

MGOMBEA WA CUF MALIM SEIF AHADI KUCHIMBA MAFUTA NDANI YA KIPINDI CHA MIAKA MITANO

Chama cha wananchi CUF kimesema endapo kitaingia madarakani kuingoza Zanzibar suala la mafuta na gesi asilia litaondolewa kwenye orodha ya mambo ya muungano ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Mgombea urais kupitia chama hicho Malim Seif Sharif Hamad amesema suala la mafuta na gesi asilia kuondolewa kwenye orodha ya mambo ya muungano halina lengo la kuvunja muungano bali ni kujali uchumi wa nchi ndogo na kubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Ocean View mjini hapa amesema tayari baadhi ya makampuni yameonesha nia ya kutaka kuchimba mafuta yaliopo Zanzibar hivyo serikali yake itatakeleza suala hilo ndani ya kipindi cha miaka mitano.