Chama cha siasa cha NLD, kimekuwa chama cha kwanza cha upinzani kutangaza kumuunga mkono mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia chama cha Mapinduzi CCM Dr. Ali Mohammed Shein katika uchaguzi mkuu ujao. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, naibu katibu mkuu wa NLD, Zanzibar Rashid Ahmme Joy amesema chama hicho kimeamuwa kumuunga mkono mgombea huyo kutokana na sera zake zenye kulenga siasa za umoja na kuweka mbele maslahi ya Zanzibar. Amesema chama hicho bado kina wasiwasi na wagombea wengine wa vyama vya kwamba hawatoweza kuendeleza siasa za umoja kwa kile alichodai kuwa na ulafi wa madaraka… “Sisi tutamuunga mkono mgombea atakaeleta mabadiliko na wagombea wa vyama vya upinzani watakapokuja hujui watafanya nini, hivyo mgombea wa CCM Dr. Shein ameonesha mwelekeo wa kufuata sera za siasa za umoja wa nchi”. Alisema Joy. Joy ambae kwa muda wa miezi kadhaa hajaonekana hadharani kutokana na kuugua shindikizo la damu amesema hali yake inaendelea vizuri na wiki mbili zijazo anatarajia kushiriki katika harakati za siasa. Hivyo amewaahidi wafuasi na wapenzi wa chama cha NLD ataendelea kuwepo katika ulingo wa kisiasa kwa lengo la kuleta mabadiliko ya mfumo wa siasa wa vyama vingi hasa Zanzibar. Chama cha NLD hakijasimamisha mgombea wa nafasi ya urais Zanzibar kutokana na Joy alietarajiwa kugombea nafasi hiyo kuugua siku chache baada ya tume ya uchaguzi Zanzibar kuanza kazi za utowaji wa fomu kwa wagombea wa nafasi hiyo kupitia vyama vya siasa. Hivi karibuni chama kingine cha upinzani cha APPT-MAENDELEO kimetangaza kumuunga mkono mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia chama cha wananachi CUF Seif Sharif Hamad. END

Advertisements