Mtanzania, Ahmed Khalfan Ghailani

Kesi ya kwanza inayomkabili mfungwa wa zamani wa gereza la Guantanomo imeanza tangu jana kwa uteuzi wa jopo la wazee wa mahakama katika mahakama ya shirikisho mjini New York. Ahmed Ghailani, Mtanzania anayeshitakiwa kwa kuhusika na mashambulio ya mabomu ya mwaka 1998 katika balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya, amekana mashtaka yanayomkabili ya kuwaua watu 224 wakiwemo raia 12 wa Marekani.

Kesi hiyo inasikilizwa wakati Rais Barack Obama wa Marekani akijitahidi kutimiza ahadi yake ya kuifunga jela ya Guantanamo Bay iliyoko Cuba na kuwafikisha watuhumiwa wa ugaidi mahakamani kwa kufuata taratibu za kawaida za mahakama.

Kesi ya Ghailani huenda ikaleta ushawishi katika kesi ya Khalid Sheikh Mohammed kiongozi aliyekiri kuhusika na mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11, mwaka 2001 mjini New York na Washington. Hata hivyo, Ghailani amekanusha kuhusika na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, kundi linalodaiwa kuhusika na mashambulio katika balozi hizo na yale ya Septemba 11.

Advertisements