Archive for October, 2010

TUME YA UCHAGUZI TANZANIA IMEAHIRISHA UCHAGUZI WA MAJIMBO MANNE YA ZANZIBAR

Tume ya taifa ya uchaguzi NEC katika wilaya ya magharibi imeahirisha uchaguzi wa wabunge katika majimbo matatu ya wilaya ya magharibi kwa muda usiojulikana.

Akizungumza na Zenji Fm radio msimamizi wa uchaguzi NEC wilaya ya magharib Amina Talib Ali ameyataja majimbo hayo ni Magogoni, Mtoni na Mwanakwerekwe.

Amesema kuahirishwa kwa uchaguzi huo kunatokana na upungufu wa karatasi za kupigia kura zilizopokelewa kwa wagombea hao na kutaja upungufu huo ni wa kibinadamu

Hata hivyo Amina amewataka wapiga kura katika majimbo hayo kutovunjika moyo na kuwataka kuzitunza shahada za kupigia kura hadi pale itakapotangazwa tarehe nyingine ya kufanyika uchaguzi huo.

Wakati huo huo tume ya uchaguzi ya taifa NEC imeahirisha uchaguzi katika jimbo la Wete kutokana na jina la mgombea ubunge wa chama cha TLP kutoonekana katika karatasi ya kupigia kura.

Hata hivyo kazi za upigaji kura katika mkoa wa Kaskazini Pemba zimendelea vizuri licha ya kujitokeza matatizo katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Katika jimbo la Ole kumejitokeza upungufu wa karatasi za kupigia kura kwa wabunge na rais wa jamhuri ya muungano Tanzania hali iliyosababisha kuchelewa kuanza kwa upigaji kura.

ZANZIBAR YAFANYA UCHAGUZI KWA AMANI NA UTULIVU

Uchaguzi Mkuu wa Tanzania umeanza vizuri, licha ya kuwepo kwa kasoro ndogo zilizosababisha baadhi ya majimbo ya matatu ya ubunge na wadi tisa kwa Zanzibar kutofanyika kutokana na hitilafu za karatasi za kupigia kura. Miongoni mwa wadi zilizoahirishwa uchaguzi huo ni Kajengwa, Mangapwani, Mchangani, Kwahani Miembeni, Nyerere na wadi tatu za Pemba na majimbo yaliohirishwa uchaguzi ni Mtoni, Mwanakwerekwe na Magogoni. Mwandishi wetu alietembelea vituo vya kupigia kura Mwanakwerekwe amesema baadhi ya mawakala wamelalamikia uhaba wa vitabu vya kupigia vya urais wa jamhuri ya muungano. Wakala wa CUF katika kituo cha Mwanakwerekwe amesema vitabu vilivyotarajiwa kuwepo katika vituo hivyo ni vitano, lakini vimefika vitatu hivyo kuna uwezekano kwa watu wengine kukosa kupiga kura. Akizungumzia suala hilo mkurugenzi wa tume ya uchaguzi Tanzania Rajab Kiravu amesema tayari makamishna wa tume hiyo wanafuatilia matatizo hayo katika vituo vya Tanzania bara na Zanzibar…

Nae mgombe mwenza wa chama cha ATPP-MAENDELEO Rashid Mchenga amesema iwapo baadhi ya wananchi watakosa kupiga kura kutokana na uchache wa vitabu uchaguzi utarejewe kulingana na sheria Hata hivyo akizungumza na Zenji Fm radio amesema uchaguzi umefanyika kwa amani na utulivu na kuwataka wagombea kukubali matokeo kwa maslahi ya taifa lao…

Na huko Tanzania bara baadhi ya wapiga kura mjini Dar es Salaam walilalamika tatizo la kutokuwemo kwa majina yao katika orodha ya wapiga kura. Kazi za kuhesabu kura zinatarajiwa kuanza katika vituo vyote vya kupigia kura na matokeo yake yatabandikwa katika vituo hivyo

TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR IMEAHIRISHA UCHAGUZI KATIKA WADI NNE ZA MKOA WA MJINI MAGHARIBI

Tume ya uchaguzi Zanzibar imeahirisha uchaguzi wa madiwani katika wadi nne za mkoa wa mjini magharibi kutokana na kukosewa kwa uchapishaji wa karatasi za kupigia kura kwa wagombea hao.

Akizungumza na waandishi wa habari huko hoteli ya Bwawani mkurugenzi wa tume hiyo Salum Kassim Ali amezitaja wadi hizo ni Mchangani jimbo la Mji mkongwe, Kwahani jimbo la Kwahani, Miembeni jimbo la Kikwajuni na wadi ya Nyerere jimbo la Magomeni.

Amesema hali hiyo inatokana na baadhi ya majina ya wagombea kuonekana katika wadi ambazo hawahusiki kupigiwa kura na baadhi ya wapiga kura kulazimika kupiga kura wadi sio zao.

Hata hivyo mkurugenzi huyo amesema uchaguzi wa madiwani katika wadi hizo utafanyika Jumapili ijayo  tarehe 28 mwezi ujao na hakutakuwa na kampeni wala uteuzi wa wagombea.

Wakati huo huo Ali amesema vifaa vya kupigia kura zikiwemo karatasi za kupigia kura tayari vimeshasambazwa katika vituo vyote vya kupigia kura vya Unguja na Pemba vipatavyo elfu moja, 291.

Uchaguzi mkuu wa nne wa Zanzibar wa mfumo wa vyama vingi unatarajiwa kufanyika kesho ambapo jumla ya wapiga kura laki nne elfu saba, 658 watapiga kura kuwachagua wagomea urais wa Zanzibar, muungano, wawakilishi, wabunge na madiwani.

TANZANIA YAINGIA KATIKA UCHAGUZI MKUU

Wananchi wakiwa katika foleni ya kupiga kura

Wananchi wa Tanzania wanapiga kura katika uchaguzi mkuu wa rais, bunge, uwakilishi na udiwani  Jumapili ya tarehe 31 Octoba mwaka 2010.

Uchaguzi huo wa nne wa vyama vingi vya siasa kwa upande wa Zanzibar unaonekana kuwa na mchuano mkali kati ya mgombea wa urais wa CCM Dr. Ali Mohammed Shein na mgombea wa CUF Seif Sharif Hamad.

Jumla ya wapiga kura laki nne, elfu saba, 658 kwa upande wa Zanzibar watapiga kura kuwachagua wagombea urais wa jamhuri ya muungano Tanzania, urais wa Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani katika vituo vya kupigia kura vipatavyo elfu moja, 291 Unguja na Pemba.

Na huko Tanzania bara wapiga kura watawachagua wagomea urais wa jamhuri ya muungano, wabunge na madiwani. Kampeni za uchaguzi huo mkuu zinatarajiwa kumalizika rasmi hapo kesho

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetenga zaidi ya shilingi bilioni 2.5 kugharamia uchaguzi mkuu wa Zanzibar.

MAALIS SEIF AHIDI KUKUBALI MATOKEO YA UCHAGUZI

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha wananchi CUF Seif Sharif Hamad amesema yuko tayari kukubali matokeo ya uchaguzi na kuwataka wafuasi wa chama hicho kutiofanya vurugu wakati wa kutangazwa matokeo hayo.

Hata hivyo mgombea huyo ametoa wito kwa tume ya uchaguzi Zanzibar kuendesha uchaguzi wa haki na huru na kuwasimamia maafisa wake wa wilaya ambao wanatiliwa shaka ya kutaka kuchafua uchaguzi.

Akizungumza katika mkutano wa mwisho wa kampeni za uchaguzi huko viwanja vya Maisara Maalim Seif amesema wakati umefika kwa wazanzibar kuachana na siasa za chuki na kuanza kutafuta njia za kujiiinua kimaendeleo.

Amesema wazanzibar wana kila sababu ya kuendeleza maridhiano ya kisiasa yanayolenga kuijenga Zanzibar mpya

Kuhusu serikali ya umoja wa kitaifa itakayoundwa baada ya uchaguzi amesema endapo ataingia madarakani atahakikisha serikali hiyo inawajumuisha wazanzibari wote bila kujali udini na ukabila.

Amesema ataingoza Zanzibar kwa kutumia utawala wa sheria na hakuna kiongozi hata mmoja atakaekuwa juu ya sheria ili kuona kila mwananchi anapata haki yake.

Aidha mgombea huyo amesema endapo wananchi watamchagua serikali yake itaimarisha uchumu kwa asilimia 15 utakaolenga kuinua maisha ya wananchi kwa kuongeza nafasi za ajira.

 

RAIS KIKWETE KUONDOA SUALA LA MAFUTA KWENYE MUUNGANO

Mgombea urais wa Jamhuri ya muungano Tanzania kupitia chama cha Mapinduzi Dr. Jakaya Kikwete ameahidi kulipatia ufumbuzi tatizo la uchimbaji wa mafuta ya Zanzibar katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Amesema matatizo mengi yaliodaiwa kuwa kero ya muungano tayari yameshapitiwa ufumbuzi, kupitia kamati ya pamoja ya waziri mkuu na waziri kiongozi na maeneo yaliobakia ikiwemo suala la uchimbaji wa mafuta ya Zanzibar kuondolewa katika muungano litapatiwa jawabu

Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari ambapo Zenji Fm radio imetangaza moja kwa moja rais Kikwete pia ameahidi kuimarisha sekta ya uwekezaji ili kulipatia ufumbuzi tatizo la ajira.

Amesema tatizo la ajira kwa vijana bado ni kubwa nchini, lakini amesema endapo atachaguliwa tena kuiongoza Tanzania serikali yake itawavutia wawakezaji kwa kuwawekea mazingira mazuri.

Rais Kikwete amesema mpango huo utakwenda sambamba na kuwawezesha wakezaji wazalendo kwa kuwapatia mikopo ya kuwekeza katika viwanda, huduma na biashara ili kusaidia ukuwaji wa uchumi.

Aidha Dr. Kikwete amesema serikali yake itaanzisha benki ya wakulima na kuongeza fedha katika taasisi za fedha zinazotoa mikopo yenye masharti nafuu ili kuwawezesha wananchi kujiajiri na kuwajiri wengine…….)

RAIS KARUME ATOA MSAMAHA KWA WAFUNGWA

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dr. Amani Abeid Karume ametoa msamaha kwa wafungwa kumi na moja walioko katika vyuo mbali mbali vya mafunzo Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa na idara ya mawasiliano ikulu mjini Zanzibar imesema msamaha huo utaanza tarehe 30 Octoba mwaka huu.

Rais Karume ametoa msamaha huo kwa mujibu wa kifungu cha 59 ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Hatua hiyo ya rais Karume anaemaliza muda wake baada ya kuapishwa rais mpya inatokana na kukubali kwake maombi ya msamaha yaliowasilishwa kwake na kamati ya msamaha ya rais.

Taarifa hiyo imesema msamaha huo utatolewa kwa wafungwa wenye umri mkubwa, maradhizi sugu na wenye vifungo vidogo walionesha nidhamu.

Aidha taarifa hiyo imesema wanafunzi wenye makosa kama vile kutumia nguvu, wizi wa mali za serikali, makosa ya kudhalisha wanawake na watoto, makosa ya dawa za kulevya huwa hawapewi msamaha