Makao makuu ya UNDP

 

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo(UNDP) limeeleza kuwa mafanikio makubwa yaliopatikana Zanzibar katika sekta zote za maendeleo yanatokana na uongozi madhubuti wa Rais Amani Abeid Karume.

Ujumbe wa Shirika la UNDP nchini Tanzania ulioongozwa na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika hilo Dk. Alberic Kacou, ulieleza hayo leo wakati ulipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume, Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Kacou alimueleza Rais Karume kuwa UNDP inajivunia mafanikio makubwa yaliopatikana Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Karume.

Dk. Kacou alieleza kuwa UNDP inathamini sana na itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikiali ya Mapinduzi Zanzibar katika suala zima la kupambana na umasikini ambapo hatua hiyo imefika pazuri chini ya uongozi wa Rais Karume.

Alisema kuwa katika uongozi wa Rais Karume UNDP imeweza kujionea hatua kubwa ya mafanikio katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu, miundombinu ya barabara, mawasiliano, maji, umeme, afya na nyenginezo.

Aidha, Dk. Kacou alieleza kuwa Rais Karume ameweza kuipeleka Zanzibar katika maisha ya amani, utulivu na umoja hali ambayo imeonesha wazi kuwa amepevuka kisiasa.

Alisema kuwa hatua ya maridhiano imeweza kuifanya Zanzibar kuwa na amani kubwa hasa katika kipindi hichi cha Kampeni za kisiasa ambazo zimeweza kufanikiwa na kufanyika katika hali ya ustaarabu na utulivu wa hali ya juu.

“UNDP, imefarajika kwa kiasi kikubwa na uongozi wako Dk. Karume kwani juhudi kubwa umezichukua katika kuimarisha sekta za maendeleo kiuchumi, kisiasa na kijamii”,alisema Dk. Kacou.

Nae Mwakilishi wa UNFPA Bi Julitta Onabanjo, ambaye ni miongoni mwa viongozi walioambatana na Dk. Kacou alimueleza Rais Karume kuwa juhudi kubwa zimefanyika katika kuimarisha huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na huduma kwa mama na watoto.

Alieleza kuwa sekta ya afya nayo imepiga hatua kubwa hapa Zanzibar kiasi ambacho suala zima la afya kwa wananchi limeweza kupewa kipaumbele kwa kuwapelekea karibu wananchi huduma hizo.

Alisema kuwa hatua ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Karume ya kuanzisha Chuo cha Madaktari Wazalendo waliochini ya wakufunzi kutoka Cuba ni za kupigiwa mfano na anamatumaini zitazidi kuimarisha sekta ya afya hapa Zanzibar.

Bi Onabanjo alieleza kuwa UNFPA itaendelea kutoa mashirikiano yake kwa kuweza kusaidia programu mbali mbali sanjari na kutoa mashirikiano katika upatikanaji wa elimu, uimarishaji sekta ya afya, fedha na mipango kabambe ya hapo baadae.

Akieleza juu ya mashirikiano yao katika sekta ya kilimo, Bi Onabanjo alisema kuwa Shirika lake litaendelea kuunga mkono juhudi zilizochukuliwa katika kuimarisha sekta ya kilimo.

Alieleza kuwa tayari juhudi zimeshachukuliwa na Shirika hilo kwa mashirikiano na Wizara ya kilimo katika kuongeza uzalishaji wa mbegu zikiwemo mbegu za mpunga sanjari na kuendelea kutafuta ufumbuzi wa maradhi ya matunda kama embe.

Aidha, viongozi hao walieleza kuwa wataendelea kutoa ushirikiano wao katika kuhakikisha soko la bidhaa ndogo ndogo linapatikana pamoja na kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Nae Rais Karume kwa upande wake alitoa pongezi kwa Shirika la UNDP kwa mashirikiano yake makubwa kati yake na Zanzibar hali ambayo imepelekea mafanikio makubwa kuweza kupatikana.

Alieleza kuwa             Shirika hilo limeweza kusaidia shughuli mbali mbali za kijamii na kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kuunga mkono Mkakati wa Kupunguza Umasikini na Kukuza Uchumi Zanzibar (MKUZA).

Rais Karume alisema kuwa juhudi zilizofanywa na Zanzibar kwa kuweza kuziweka pamoja afisi zote za Umoja wa Mataifa (ONE UN), kuwa kwenye jengo moja ni hatua moja wapo ambayo itasaidia kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kwa haraka.

Sambamba na hayo, Rais Karume alisema kuwa kufanikiwa katika kupiga vita Malaria kumeweza kusaidia hata kupunguza vifo vya akinamama na watoto sanjari na kujijengea sifa na kutoa mafunzo kwa nchi ambazo zimo katika kupambana na maradhi hayo.

Rais Karume alisema kuwa huduma za afya zimeweza kuimarika kiasi ambacho Zanzibar imeweza kutoa huduma hiyo hata kwa wananchi wageni kutoka nchi mbali mbali  ikiwemo Comoro, ambapo baadhi ya wananchi wake huja Zanzibar kufuata huduma za afya.

Aidha, alieleza kuwa kuwepo kwa miundombinu bora katika sekta zote nako kumechangia kuimarika kwa sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya.

Akieleza juu ya mafanikio ya kisiasa yaliofikiwa Zanzibar, Dk. Karume alisema kuwa Zanzibar hivi sasa ni shuwari ambapo kila mtu analishuhudia hilo hali ambayo imetokana na azma ya kujenga umoja, amani na utulivu kwa nchi na wananchi wake.

Akieleza juu ya mafanikio yaliopatikana kisiwani Pemba, Rais Karume alisema kuwa kwa upande wa uimarishaji wa sekta za maendeleo kisiwa cha Pemba kimepata mafanikio makubwa na yanaendelezwa.

Rais Karume alisema kuwa juhudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha maendeleo zaidi yanapatikana katika visiwa vyote vya Unguja na Pemba na kutoa pongezi kwa washirika wa maendeleo yakiweno Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.

Advertisements