Askofu Cosmas Shayo

 

Askofu wa kanisa Katoliki Zanzibar Cosmas Shayo amedai baadhi ya sera za vyama vya siasa zinazonadiwa katika mikutano ya kampeni haziwezi kutekelezeka endapo vitapata ridhaa ya kuingia ikulu.

Amesema wagombea wa vyama hivyo wanatoa ahadi nyingi kwa wananchi, lakini baadhi yake ni usanii  kwa vile haziwezi kutekelezeka katika kipindi cha miaka mitano.

Akifunga warsha ya siku moja ya waandishi wa habari juu ya kuripoti habari za uchaguzi huko Machuwi wilaya ya kati Askofu Shayo amevitaka vyombo vya habari kuwahoji wagombea hao juu ya ahadi hizo ili wananchi wafanye uamuzi sahihi siku ya kupiga kura

Aidha Askofu Shayo amewataka wandishi wa habari kutoegemea upande wowote wa vyama vya siasa kwa lengo la kutoa taarifa sahihi zinazoweza kuwasaidia wananchi wakati huu upigaji kura kwa ajili ya uchaguzi wa urais, uwakilishi, ubunge na udiwani ukikaribia.

Warsha hiyo ya wandishi wa habari wa vyombo vya radio iliyojadili jinsi ya kuripoti habari za uchaguzi imeandaliwa na kanisa katoliki Tanzania chini ya ufadhili wa shirika la maendeleo la umoja wa mataifa UNDP

Advertisements