Eneo la bandari ya Dar es Salaam

Jumuiya ya wafanyabishara, wenyeviwanda na wakulima imesema tatizo la wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili wanapopeleka bidhaa zao Tanzania bara bado halijaondoka.

Rais wa Jumuiya hiyo Bw. Mbarouk amesema hayo katika mkutano wa tano wa baraza la biashara Zanzibar uliokuwa chini ya mwenyekiti wake rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dr. Amani Abeid Karume huko katika ukumbi wa zamani wa baraza la wawakilishi.

Amesema wafanyakazi wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA wamekuwa wakiwatoza kodi mara mbili wafanyabiashara hao kwa kile alichodai bado halijatolewa agizo kutoka ngazi za juu

Malalamiko hayo yametolewa huku kukiwa na kauli za baadhi ya viongozi wa serikali wakisema miongoni mwa kero za muungano zilizopatiwa ufumbuzi ni pamoja kusitishwa kwa wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili wanaposafirisha bidhaa Tanzania bara.

Nae mwenyekiti wa baraza hilo anaemaliza muda wake rais Karume amesema ipo haja kwa Zanzibar kutangazwa kama kituo cha uwekezaji wa sekta ya viwanda, vidogo na kati kwa kushirikiana na wawekezaji wa nje.

Aidha amezitaka taasisi za serikali na binafsi kuendeleza uvuvi wa bahari kuu, usindikaji wa mazao ya baharini, matunda, nafaka pamoja uwekezaji wa kilimo cha umwagiliaji maji.

Rais Karume amesema kuimarishwa kwa sekta hizo kutatoa fursa kwa Zanzbiar kukuza biashara na kusaidia upatikanaji wa ajira kwa wananchi

Mkutano huo wa tano wa baraza la biashara umejadili vikwazo vya sekta ya utalii kama vile mapapasi, kutokuwepo misamaha ya kodi kwa wawekezaji wazalendo na kodi ya asilimia mbili ya mifugo.

Advertisements