Mke wa rais wa Zanzibar Shadya Karume

Mke wa rais wa Zanzibar mama Shadya Karume amesema bado makundi ya vijana na wanawake yanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira linalosababisha baadhi yao kujingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya.

Amesema Zanzibar sawa na nchi nyingine zinazoendelea sehemu kubwa ya nguvu kazi ni vijana na wanawake, hivyo wanahitaji kuendelezwa kitaaluma ili kuleta ushindani katika soko la ajira na uzalishaji.

Mama Shadya amesema hayo alipokuwa akifungua kituo cha utowaji wa taarifa za ajira na masoko za ndani na nje ya nchi huko wizara ya kazi, maendeleo ya vijana, wanawake na watoto Mwanakwerekwe.

Amesema ukosefu wa ajira na taarifa za soko la bidhaa za wazalishaji nchini ni jambo linalowachanganya vijana, hivyo kuwepo kwa kituo hicho kutawasaidia kupata taarifa za ajira na soko la bidhaa wanazozalisha.

Hata hivyo Mama Shadya amewataka vijana kutochagua kazi kwa kutegemea kazi serikalini na badala yake wajiingize katika sekta binafsi ambazo zina mchango mkubwa wa pato la taifa..

Nae waziri wa kazi, maendeleo ya vijana, wanawake na watoto Asha Abdala Juma amesifu ushirikiano uliopo kati ya serikali na shirika la kazi duniani ILO kwa kushughulikia matatizo ya vijana hasa ukosefu wa ajira.

Amesema kituo hicho kitaweka mitandao itakayowawezesha makundi ya vijana na wanawake kupata taarifa za ajira na soko la bidhaa pamoja kuwasaidia wawekezaji kupata wafanyakazi.

Ujenzi wa kituo hicho ulioanza mwaka 2009 umegharimu zaidi ya shilingi milioni 155 chini ya ufadhili wa umoja wa mataifa kupitia mradi wa J.P-5 unaolenga kuijengea uwezo Zanzibar.

 

 

Advertisements