Karatasi za kupigia kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Octoba 31 zimewasili Zanzibar leo katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Karume zikitokea nchini Afrika ya kusini.

Akizungumza na Zenji Fm radio katika uwanja huo mkurugenzi wa tume ya uchaguzi Zanzibar Salum Kassim Ali amesema karatasi zilizokuwemo kwnye masanduku 1,161 za kupigia kura ni za aina tatu zikiwemo za rais, uwakilishi na udiwani.

Amesema karatasi hizo za kupigia kura zitasambazwa kwenye vituo vya kupigia kura kuanzia tarehe 30 na kabla ya kusambazwa zitahifadhiwa katika makao makuu ya tume ya uchaguzi Zanzibar chini ya ulinzi wa vyombo vya dola

Karatasi hizo za kupigia kura zilizochapishwa nchini Afrika ya kusini hadi kufika Zanzibar zimegharimu zaidi ya shilingi milioni 270.

Huku karatasi hizo za kupigia kura zikiwasili wananchi waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura katika maeneo ya Unguja na Pemba wanaendelea kuhakiki majina yao katika vituo vya kupigia kura.

Wananchi wa Zanzibar wanatarajia kupiga kura Jumapili ijayo katika uchaguzi utakaowashirikisha wagombea saba wa nafasi ya urais wa Zanzibar na idadi kama hiyo kwa rais wa jamhuri ya muungano Tanzania pamoja wa gombea uwakilishi, udiwani na ubunge

Advertisements