WAGOMBEA kadhaa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Wananchi (CUF) wamewabwaga wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwemo mawaziri na viongozi wengine waandamizi waliokuwa katika Serikali iliyopita.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, pia wameshinda ubunge mkoani Kilimanjaro.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zitto, ametangazwa kuwa ni mshindi katika uchaguzi wa ubunge kwenye jimbo la Kigoma Kaskazini.

Msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya (bongo flava), Joseph Mbilinyi (Mr II au Sugu) ameshinda katika uchaguzi wa ubunge jimbo la Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chadema.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Lindi Mjini, Ahamad Sawa jana alitangaza ushindi kwa CUF baada ya kukamilika kuhesabu kura zilizopigwa.

Alisema CCM ambayo ilikuwa na mgombea, Mohammed Abdulaziz, alishindwa kwa kupata kura 11,402 huku mpinzani wake wa CUF Salumu Barwani akipata kura 13,155.

Kutoka Tarime, Samson Chacha anaripoti kwamba mgombea wa CCM Nyambari Nyangweni, amewabwaga wagombea wenzake kutoka vyama vya upinzani kwa kupata kura 28,064.

Mgombea wa Chadema, Mwikwabe Waitara alipata 27,334, wa NCCR-Mageuzi Peter Wangwe (7,811), wa CUF, Charles Mwera (7,368), wa UDP Mchungaji Jacob Mwita (185) na wa TLP, Nyaronyo Kicheere (145).

Jasmin Shamwepu, anaripoti kutoka Dodoma, kuwa Msimamizi wa uchaguzi Dodoma Mjini Suzan Bidya, alimtangaza mgombea wa CCM, David Malole, kuwa mshindi kwa kura 52,243 sawa na asilimia 73.

Aliwashinda wagombea wengine, wa Chadema, Enock Muhembano aliyepata kura 15,806 sawa na asilimia 22, wa CUF Haruna Kamwelwe kura 1,903 sawa na asilimia 2.7.

Mgombea wa NCCR–Mageuzi, Mohamed Kabutali, alipata kura 714 sawa na asilimia moja na wa UPDP, Bona Masawe kura 589 sawa na asilimia 0.83.

Kutoka Shinyanga, Shangwe Thani, anaripoti kwamba msimamizi wa uchaguzi Meatu, Upendo Sanga, alimtangaza mgombea wa Chadema, Meshack Opurukwa kuwa Mbunge wa jimbo hilo, baada ya kupata kura 13,850 na wa CCM, Salum Khamis (12,824).

Kutoka Musoma, taarifa rasmi iliyotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi Musoma Mjini, ilithibitisha ushindi wa Vincent Nyerere wa Chadema, kuwa mbunge mpya baada ya kumshinda Vedasto Manyinyi wa CCM.

Nyerere alipata kura 21,335 (56.71%), Manyinyi 14,072 (39.38%), Mustapha Wandwi wa CUF 253 (0.71%) Chrisant Nyakitita wa DP 53 (0.15%) na Tabu Machibya wa NCCR–Mageuzi, 19 (0.05%).

Kutoka Mbeya, Merali Chawe anaripoti kuwa Nec ilimtangaza mgombea ubunge wa CCM Mbarali, Dickson Kilusi kuwa mshindi baada ya kupata kura 34,869 dhidi ya wa Chadema, Kazamoyo Kangwa (16,090), TLP, Getrude Dwila (487) na Mwantange Damas wa UDP aliyeambulia kura 237.

Kutoka Ruvuma, Mbunge aliyemaliza muda wake Peramiho, Jenista Mhagama ameshinda tena kiti hicho kwa kupata kura 28,753 dhidi ya mpinzani wake, Mchungaji Chilokota aliyepata kura 2,562.

Katika udiwani, CCM ilizoa kata 17 na Chadema moja. Tunduru Kaskazini, Ramo Makani wa CCM alishinda kwa kupata kura 19,573 na kuwashinda wagombea wengine watatu: Mzee Rajabu wa CUF kura 17,365; Randi Daudi wa Chadema kura 604 na Makamanya Simbili wa UDP kura 72. Kwa udiwani, CCM ilipata kata 16, CUF nne na Chadema moja.

Tunduru Kusini, Mtutura Abdallah Mtutura wa CCM alirejea bungeni kwa kuzoa kura 16,856 dhidi ya kura 10,930 za Mohamed Mambo wa CUF.

Kwa udiwani, CCM ilizoa viti 13 na CUF kimoja. Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo wa Chadema alishinda tena kwa kuzoa kura 28,797 akifuatiwa na Justine Salakana wa CCM aliyepata kura 16,792.

Wengine ni Seif Madongo wa CUF 97; Godfrey Malisa wa TLP 55; Issack Kireti wa SAU 42; Faustine Sungura wa NCCR-Mageuzi 42 na Ndesanyo Godlisen wa UDP 34.

Watu waliojiandikisha walikuwa 112,479; waliojitokeza kupiga kura ni 46,053; kura halali ni 45,759 na zilizoharibika ni 294. Katika jimbo hilo, Chadema ilishinda kata 17 na CCM nne za udiwani.

Mwanga, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe ameshinda kwa kura 20,730 dhidi ya Shafii Msuya wa Chadema aliyepata kura 4,719.

Mgombea mwingine Khadija Hajia wa CUF alipata kura 556; wakati waliojiandikisha ni 63,669; waliopiga kura ni 26,005 na kura 284 ziliharibika.

Kutoka Singida Hudson Kazonta, anaripoti kwamba Msimamizi wa Uchaguzi Singida Mjini, Yona Maki alimtangaza Mohamedi Dewji wa CCM, kuwa mshindi baada ya kupata kura 21,169, dhidi ya wapinzani wake watatu.

Dewji alipata ushindi huo na kuwaacha mbali wapinzani hao; Josephat Isango (Chadema) kura 3,457, Rashidi Mindicar wa CUF (648) na Omari Sombi wa AFP (190).

Maki alisema idadi ya wapiga kura waliojitokeza ni sawa na asilimia 40.4 tu, hivyo ni ndogo ikilinganishwa na watu 64,515 ya waliojiandikisha kwenye Daftari.

Arusha Mjini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Batilda Burian, ameshindwa na mgombea wa Chadema, Godbless Lema.

Dk. Burian alipata kura 37,460 huku Lema akizoa kura 56,551, na Maximillian Lyimo wa TLP akipata kura 722 na Balawi Balawi wa CUF 150.

Waliojiandikisha katika jimbo hilo ni watu 240,822, na waliopiga kura ni 96,313. CCM imeshinda kata tisa, sawa na Chadema wakati TLP ina kata moja.

Arumeru Magharibi, Godluck ole Medeye wa CCM ameshinda kwa kura 35,544, akifuatiwa na Jackson ole Kisambo wa Chadema kura 27,425.

Katika jimbo hilo, CCM imepata kata 33 na Chadema kata nne. Katika urais, Rais Jakaya Kikwete amepata kura 33,470 na Dk. Willibrod Slaa kura 27,587.

Mkinga, Mgombea wa CCM, Dustan Kitandula ameibuka na ushindi wa kura 16,967 dhidi ya mgombea pekee wa upinzani kutoka CUF, Bakari Mbega aliyejizolea kura 11,252.

Nyamagana, mgombea wa Chadema, Ezekiel Wenje amepata kura 38,171 dhidi ya Lawrence Masha wa CCM aliyepata kura 27, 883.

Kibaha Vijijini, mgombea wa CCM, Hamoud Jumaa ameshinda kwa kura 11,361, akifuatiwa na Agnes Emmanuel wa Chadema, 2,201 na Abdallah Zugo wa CUF kura 1,086.

Katika urais, Jakaya Kikwete kura 11,711; Dk. Willibrod Slaa 2,021; Profesa Ibrahim Lipumba 1,001. Kwa upande wa udiwani, CCM imeshinda kata 11 kati ya 12 na kata moja ya Janga haijafanya uchaguzi.

Kutoka Pangani, kura zilizopigwa ni 15,412, halali 15,085 na zilizoharibika ni 327. Mshindi ni mgombea wa CCM, Salehe Pamba 9,342 dhidi ya mgombea wa CUF, Omari Ally 4,521 na wa Chadema, Abdallah Omari 1,222.

Advertisements