Spika wa baraza la wawakilishi Pandu Ameir Kificho

Wajumbe wa baraza la wawakilishi Zanzibar wamemchagua tena Pandu Ameir Kificho kuwa spika wa baraza hilo kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015.

Hii ni mra ya nne mfululizo kwa Spika Kificho kuliongoza baraza la wawakilishi Zanzibar.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi wa spika uliofanywa na wajumbe wa baraza la wawakilishi, katibu wa baraza hilo Ibrahim Mzee Ibrahim amesema spika Kificho ameshinda kwa kupata kura 45 dhidi ya mpinzani wake aliwania nafasi hiyo Abass Juma Mhunzi aliepata kura 32

Nae spika Kificho baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo kabla ya kuwapisha wajumbe 78 waliokuwemo ndani ya ukumbi wa baraza la wawakilishi alikula kiapo cha uaminifu

Akitoa salamu zake mara baada ya kula kiapo hicho Spika Kificho amewataka wajumbe wa baraza la wawakilishi kulinda mfumo mpya wa serikali ya umoja wa kitaifa ulioridhiwa na wananchi.

Amesema baraza la saba lililopita lilifanya marekebisho ya nane ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 baada ya kufanyika kura ya maoni iliyoridhia serikali ya umoja wa kitaifa, hivyo ni vyema kwa viongozi hao kuheshimu uwamuzi wa wananchi walio wengi.

Hatua hiyo ya kuapishwa kwa wajumbe wa baraza la wawakilishi itatoa fursa kwa rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mpinduzi Dr. Ali Mohammed Shein kuteuwa mawaziri na manaibu miongoni mwa wajumbe hao..

Advertisements