Balozi wa Marekani nchini Tanzania Alfonso Lenhardt

MAREKANI , imeeleza kuridhishwa na uchaguzi wa Zanzibar uliopita na kutoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed  Shein pamoja na wananchi wa Zanzibar kwa kuendesha uchaguzi kwa salama na amani.

 

Akizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohammed Shein, Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe. Alfonso Lenhardt aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar.

 

Balozi Lenhardt alimpongeza Dk. Shein kwa kuchaguliwa na wananchi  kuiongoza Zanzibar na kueleza kuwa uchaguzi wa Zanzibar uliopita ni wa kihistoria hatua ambayo inapanua wigo kwa mataifa mengine ya Afrika na nje ya Afrika.

 

Alisema kuwa uchaguzi wa Zanzibar umeenda vizuri na hatua hiyo imechangiwa zaidi na wananchi wa Zanzibar ambao nao wanastahiki pongezi kwa kuweza kufanya uchuguzi kwa amani na utulivu.

 

Katika mazungumzo hayo, Balozi huyo wa Marekani alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo wa kihistoria  kati ya Marekani na Zanzibar na kuahidi kuudumisha na kuuendeleza daima milele.

 

Balozi Lenhardt alieleza kuwa Marekani ina kila sababu ya kujivunia mafanikio yaliofikiwa Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo ambazo Marekani imeahidi kuziunga mkono kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.

 

Akieleza juu ya uimarishaji wa miradi ya maendeleo, Balozi Lenhardt alieleza kuwa Marekani itaendelea kutoa misada yake katika uimarishaji wa miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuutekeleza mradi mkubwa wa pili wa umeme kutoka Ras Kiromoni hadi Fumba chini ya udhamini wa MCC.

 

Alieleza kuwa mbali ya mradi huo tayari Marekani imeshatoa misada yake mingi katika uimarishaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kusaidia mradi wa maji huko Fundo, Pemba.

 

Pamoja na hayo, Balozi Lenhardt alimueleza  Dk. Shein kuwa kuwa nchi yake itaendelea kutoa mashirikiano katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu kwa kuinua kiwango cha elimu ya msingi kwa kuifanya kuwa ya kisasa zaidi kwa kuwawezesha wanafunzi kuweza kutumia compyuta mradi ambao utafadhiliwa na nchi hiyo.

 

Pia, Balozi Lenhardt alieleza kuwa nchi yake itaendelea kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo afya, miundombinu, mawasialino na  nyenginezo.

 

Aidha, Balozi huyo alimuahidi Dk. Shein kuwa ataendelea kuitangaza Zanzibar katika medani ya Utalii kutokana na mafanikio makubwa yaliofikiwa hapa nchini katika sekta hiyo.

 

Nae Dk. Shein alitoa pongezi kwa Marekani, wananchi wake pamoja na Ubalozi wake uliopo hapa nchini kwa kuendeleza ushirikiano na uhusiano mwema ambao umeweza kutoa mashirikiano makubwa.

 

Dk. Shein alitoa shukurani zake kwa Marekani kwa pongezi walizompa kutokana na ushindi wake.

 

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa  katika kuimarisha sekta za maendeleo Zanzibar imepiga hatua kubwa na kazi  kubwa inayohitajika hivi sasa ni kuziimarisha zaidi sekta hizo ili ziendelee kuleta manufaa kwa nchi na wanachi wake.

 

Dk. Shein alisema kuwa lengo la serikali yake ni kuziimarisha zaidi sekta za maendeleo sanjari na kupanua miundombinu ya umeme, maji, mawasiliano na sekta nyenginezo na kusisitiza zaidi kuwa juhudi zitachukuliwa katika kuinua sayansi na teknolojia kutokana na wakati uliopo.

 

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Serikali ya Marekani kwa kusaidia uimarishaji wa sekta ya afya kwa kuweza kushirikiana na Zanzibar katika vita ya kupambana na Malaria, vifo vya akina mama na watoto pamoja na maradhi ya miripuko.

 

Aidha, alitoa pongezi kwa Marekani kwa kuunga mkono mradi wa umeme chini ya udhamini wa MCC .

 

Wakati huo huo China imepongeza hatua za maendeleo zilizofikiwa Zanzibar na kuahidi kuendelea kuyaunga mkono chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohammed Shein.

 

Balozi Mdogo wa China anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Mhe.  Li Yiping aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Shein, Ikulu mjini Zanzibar.

 

Balozi Yiping alimpongeza Dk. Shein kwa kuchaguliwa na wananchi kuiongoza Zanzibar na kumuahidi kuwa China itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar sanjari na kuimarisha misaada yake katika sekta za maendeleo ikiwemo elimu.

 

Nae Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati yake na China ambao ni wa kihistoria ulioasisiwa na viongozi wakuu akiwemo Mzee Abeid Karume na Mwalimu Julius Nyerere.

 

Dk. Shein aliipongeza China kwa mafanikio makubwa iliyoyapata kiuchumi na kueleza kuwa Zanzibar itaendelea kupanua wigo wa kimaendeleo kutoka nchini humo.

 

Advertisements