Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein amewataka viongozi kuendeleza amani na umoja ili kusaidia hatua mpya za kuijenga Zanzibar kimaendeleo na kiuchumi.

Akihutubia baraza la Eddel-hajj Dr. Shein amesema maendeleo ya nchi yanapatikana pale viongozi na wananchi wanapokuwa wamoja, watiifu kwa nchi yao na kuheshimu amani na utulivu.

Amesema serikali ya awamu ya saba itazingatia mambo hayo katika utekelezaji wa shughuli zake za kila siku na kuendelea kuijenga Zanzibar

Aidha Dr. Shein amewataka wazazi kuwafunza watoto wao utiifu kwa mwenyezi mungu, mila na silka za jamii yao ili kuwaepusha na maovu kama vile matumizi ya dawa za kulevya na hatimae kuambukizwa ukimwi.

Amesema serikali itaendelea kuimarisha sera na sheria za kuwalinda watoto, kuwapatia haki zao na kuwafunza utiifu ili kuinua maendeleo yao kama ilivyoelezwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010.

Dr. Shein pia amewataka wafanyabiashara wasitumie fursa za siku za skuu kupandisha bei ya vyakula na vinywaji baridi pamoja na vitu vya kuchezea na huduma za watoto ili watoto wote waweze kuzimudu.

Akizungumzia utekelezaji wa ibada ya Hijja Dr. Shein amezitaka taasisi zinazosafirisha mahujaji kupunguza gharama ambazo zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wale wanaotaka kwenda kutekeleza ibada hiyo.

Amesema mifano ya kuigwa ipo kwa nchi za Indonesia, Misri, Sudan na Malaysia ambapo taasisi zinazoshughulikia usafirishaji wa mahujaji zimejenga ushirikiano na kupunguza gharama za usafiri.

Dr. Shein amesema jambo hilo jema na la kheir la utekelezaji wa ibada ya hijja kwa waislamu lisichukuliwe kama ushindani wa kibiashara kwa kujipatia faida nyingi.

Dr. Shein amelihutubia baraza hilo la Eddel –hajj kwa mara ya kwanza tokea kuingia madarakani kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika Octoba 31 mwaka huu kuiongoza serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar

Advertisements