Uwekezaji katika sekta za afya, elimu, kilimo na mazingira nchini Tanzania bado ni mdogo ikilinganishwa na mahitaji ya ukuwaji wa uchumi kupitia sekta hizo.

Taarifa iliyotolewa na benki ya dunia katika mkutano wa ushauriano ulifanyika mjini Zanzibar imesema uwekezaji wa sekta hizo usiozidi asilimia 12 ni mdogo katika utekelezaji wa mipango ya kupunguza umasikini kwa wananchi.

Mwakilishi wa benki hiyo Tanzania bi Chew amesema jumla ya miradi kumi yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 2.8 imewekeza katika kipindi cha mwaka 2010 kutoka miradi kama hiyo yenye thamani ya dola bilioni 1.6 iliyoekezwa kuanzia mwaka 2007.

Amesema kwa upande wa Zanzibar benki ya dunia imetekeleza maradi wa elimu ya msingi wenye thamani ya dola za Marekani milioni 42 kuanzia mwaka 2007 pamoja na miradi ya MACEMP na TASAF II.

Chew amesema katika kipindi cha mwaka 2011 benki ya dunia itaongeza ufadhili wake kwa Zanzibar katika utekelezaji wa miradi ya utowaji wa huduma mijini wenye thamani wa dola za Marekani milioni 38.

Nao washiriki wa mkutano huo wameiomba benki ya dunia kusaidia mpango wa kuimarisha uchumi na kupunguza umasikini Zanzibar MKUZA hasa katika kilimo cha umwagiliaji maji.

Wamesema sekta ya kilimo ni muajiri mkubwa kwa wananchi, lakini imekosa uwekezaji mkubwa kutokana na wakulima wengi kutomudu gharama za uendeshaji wa kilimo.

Aidha washiriki hao wameishauri benki hiyo kuangalia uwezekano wa kuwasaidia watu wenye ulemavu ambalo ndio waathirika zaidi na umasikini.

Mkutano huo wa siku moja uliofanyika katika hoteli ya Ocean View umewashirikisha wakuu wa taasisi za serikali, jumuiya za kiraia na wandishi wa habari.

Advertisements