Archive for December, 2010

SALAMU ZA MWAKA MPYA 2011 DR. SHEIN AWATAKA WAZANZIBAR KUPIGA VITA UBADHIRIFU

Karibu mwaka mpya wa 2011

Rais wa Zanzibara na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein amewataka viongozi na wananchi kupiga vita ubadhirifu na kutumia raslimali kwa maslahi ya taifa.

Akitoa salamu za kukaribisha mwaka mpya wa 2011 amesema Zanzibar sawa na nchi nyingine dunia zinazokabiliwa na uchumi usiotabirika kutokana na kupanda kwa bei za mafuta

Aidha Dr. Sheina amesema maendeleo ya uchumi wa Zanzibar yataletwa na wananchi wenyewe na wahisani watatoa misaada yao pale wanapoona wazanzibari wanajitahidi katika kuleta maendeleo hayo.

Amesema ni matumaini yake kuona wananchi watashirikiana kuijenga nchi yao kuwa ya neema na kuwataka viongozi waliochaguliwa na wananchi kutumia muda mwingi majimboni mwao ili kutoa muongozo na ushirikiano katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

Dr. Shein pia amewataka wanchi kudumisha umoja na mshikamano uliokuwepo baada ya maridhiano ya kisiasa ili kutekeleza mipango ya maendeleo ya Zanzibar.

Mwaka uliopita Zanzibar iliandika historia kubwa ikiwemo maridhiano ya kisiasa, kura ya maoni, mabadiliko ya kumi ya katiba ya Zanzibar, uchaguzi mkuu uliofanyika kwa amani na utulivu na kuundwa serikali mpya yenye muundo wa umoja wa kitaifa.

WAFANYAKAZI AFISI YA MUFTI PEMBA WAKO HALI MBAYA

Wafanyakazi wa ofisi ya Naibu Mufti Pemba, wamesema wanakabiliwa na wakati mgumu katika utendaji wa kazi zao ikiwemo kufuatilia migogoro ya kidini kutokana na ukosefu wa vitendea kazi.

Wafanyakazi hao wamesema matatizo hayo hasa usafiri yamekuwa yakikwamisha majukumu yao ya kutoa huduma kwa wananchi.

Wakizungumza na waziri wa sheria na utawala bora Abubakar Khamis Bakar kisiwani humo pia wameiomba wizara hiyo kutowa fursa sawa za mafunzo kati ya wafanyakazi wa ofisi hiyo kwa Unguja na Pemba.

Wamesema hali hiyo imesebabisha ushirikiano mdogo kwa watendaji wa ofisi kati ya Unguja na Pemba, na wale wanaokwenda kisiwani Pemba kikazi wanafanya kazi zao bila kuwashirikisha wenzao wa Pemba.

Nae waziri Bakar, amewataka wafanyakazi wa Wizara hiyo Kisiwani Pemba, kufanya kazi kisheria ili kutowa huduma bora kwa Wananchi.

Amesema maslahi ya Wafanyakazi ikiwemo, vitendea kazi na mafunzo yanashughulikiwa kupitia wizara maalumu ya utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Taasisi ambazo zimekutana na waziri huyo ni katiba na sheria, afisi wa mkurugenzi wa mashtaka, kamisheni ya wakfu na watendaji wa afisi kuu ya wizara hiyo Pemba .

KATIBA YA ZANZIBAR HAIJAJITOSHELEZA KUUNDA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA

Aliekuwa mgombea mwenza wa urais wa jamhuri ya muungano Tanzania kupitia chama cha APPT-MAENDELEO Rashid Mchenga amesema katiba ya Zanzibar haijajitosheleza katika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na inahitaji kufanyiwa marekebisho tena.

Akizungumza katika mafunzo juu ya serikali ya umoja wa kitaifa yaliofanyika hoteli ya Ocean View amesema ulimwengu unafahamu Zanzibar ina mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa, lakini amedai kinachonekana ni serikali ya mseto kwa kuvishirikisha vyama vya CCM na CUF pekee katika serikali hiyo.

Mchenga ambae ana mpango wa kumfikisha mahakamani mwanasheria mkuu wa serikali ili kutoa tapsiri sahihi ya serikali ya umoja wa kitaifa, amesema iwapo hataridhishwa na shauri lake hilo suala hilo atalipeleka katika tume ya haki za binadamu.

Nae katibu wa baraza la wawakilishi Ibrahim Mzee akizungumza katika mafunzo hayo amesema kifungu cha tisa cha katiba ya Zanzibar kinaeleza mamlaka ya kuendesha nchi yako kwa wananchi wenyewe.

Amesema uteuzi wa baraza la mawaziri uliofanywa na rais wa Zanzibar umezingatia matakwa ya katiba kwa vile wananchi wamevichagua vyama vya CCM na CUF kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Ibrahimu amesema vyama vya siasa visitegemee kuingizwa serikali bila ya kukubaliwa na wapiga kura, hivyo amevitaka vyama hivyo kufanya kazi ya siasa kwa kuuza sera zao kwa wananchi.

Kwa mujibu wa marekebisho ya kumi ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 vyama vya siasa vitakavyounda serikali ya umoja wa kitaifa vinapaswa kuwa na uwakilishi wa wananchi ndani ya baraza la wawakilishi.

 

 

KOREA YA KUSINI KUISAIDIA ZANZIBAR KILIMO CHA UMWAGILIAJI MAJI

Bendera ya KOrea ya Kusini

KOREA Kusini imeeleza azma yake ya kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo cha umwagiliaji maji.

Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania Mhe. Young-Hoom Kim aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.

 

Katika mazungumzo hayo, Balozi Kim alimueleza Dk. Shein kuwa tayari Ripoti ya upembuzi yakinifu ya mradi wa umwagiliaji maji imefikia pazuri na itakamilika hivi karibuni.

 

Alieleza kuwa Korea Kusini imeridhishwa na mashirikiano inayoyapata katika taratibu na mikakati ya kuimarisha mradi huo wa umwagiliaji maji hapa Zanzibar.

 

Aidha, Balozi huyo alimuhakikishia Dk. Shein kuwa nchi yake itaendeleza uhusiano na ushirikiano na Zanzibar.

 

Balozi Kim alisema kuwa ana matumaini makubwa ya mafanikio ya maendeleo kutokana na uongozi wa Dk. Shein na kumueleza kuwa nchi yake itaendelea kumuunga mkono na kutoa ushirikiano wake kwa Zanzibar ili kufikia malengo yaliokusudiwa.

 

Pamoja na hayo, Mhe. Kim alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake imevutiwa na hatua za Zanzibar za kuwa na  Maeneo huru ya kiuchumi na kuahidi kuwa Balozi wa nchi yake kuitaingaza Zanzibar kutokana na sifa ilizonazo.

 

Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uchumi wa Zanzibar na kusisitiza kuwa kutokana na nchi yake kuimarika kitekonolojia hatua hiyo itasaidia kuendeleza miradi hapa Zanzibar.

 

Katika maelezo yake pia, Balozi Kim alipongeza hatua zilizofikiwa katika kuimarisha sekta ya utalii na kuahidi kuitangaza Zanzibar kiutalii sanjari na kutoa mashirikiano yake katika kuimarisha sekta ya afya hapa Zanzibar.

 

Akieleza juu ya uimarishaji wa chuo cha kilimo cha Zanzibar, Balozi Kim alieleza kuwa chuo hicho ni muhimu katika kuendeleza sekta ya kilimo hapa Zanzibar na kueleza kuwa nchi yake itaangalia njia za kukisaidia chuo hicho ili kizidi kuimarika.

 

Nae  Dk. Shein alitoa pongezi na shukurani kwa Korea Kusini kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar hatua ambayo amesema itaweza kukuza mashirikiano katika sekta mbali mbali za kimaendeleo.

 

Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano kati yake na Korea Kusini na kusema kwamba hatua ya nchi hiyo kuunga mkono kilimo cha umwagiliaji maji itaiwezesha Zanzibar kupunguzakwa kiasi kikubwa uagizajiwa chakula hasa mchele kutokana na kukuza kilimo cha mpunga

 

Katika maelezo hayo, Dk. Shein alisema kuwa anamatumaini makubwa kuwa iwapo mashirikiano yataimarishwa kwa pande mbili hizo mafanikio makubwa yatapatikana katika sekta zote za maendeleo na kiuchumi.

 

Alieleza kuwa hatua hiyo ya Korea kusini  ya kushirikiana katika kuimarisha sekta ya kilimo itasaidia  kukiimarisha kilimo pamoja na sekta nyenginezo na kusisitiza kuwa jambo muhimu kwa wakulima ni kuwapa elimu juu ya sekta ya kilimo.

 

Dk. Shein alieleza kwamba  mbali ya kuimarisha sekta ya kilimo pia, Zanzibar imeweka eneo la maeneo huru ya kiuchumi kwa ajili ya uwekezaji na kutoa fursa kwa nchi hiyo kuja kuekeza Zanzibar.

 

Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya pamoja na sekta ya utalii na kueleza kufarajika kwake na azma ya Balozi Kim kuitangaza Zanzibar kiutalii huko nchini mwake.

SMZ YAIKEMEA TRA BARA KUENDELEA KUWATOZA KODI MARA MBILI WAFANYABIASHARA WA ZANZIBAR

Nassor Ahmmed Mazurui

Waziri wa biashara, viwanda na masoko Nassor Ahmed Mazrui  ameelezea kusikitishwa na watendaji wa TRA kuendelea kuwanyanyasha wafanyabiashara wa Zanzibar wanapopelea bidhaa zao Tanzania bara.

Akizungumza na Zenji Fm radio amesema licha ya tatizo la wafanya biashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili wanapopeleka bidhaa zao Tanzania kuondolewa na vikao halali vya ngazi ya muungano  bado maafisa wa TRA wanaendelea kuwatoza kodi wafanyabiashara hao kwa utashi wao binafsi.

Mazuri amefahamisha kuwa TRA ni moja katika Zanziar na Tanzania bara hivyo uwamuzi uliotolewa wa bidhaa kutoka Zanzibar kwenda Tanzania bara na Tanzania bara kuja Zanzibar usitozwe kudo mara mbili unahitaji kuheshimiwa

Kamati ya kero za muungano iliyokuwa chini ya mwenyekiti wake aliekuwa makamo wa rais wa jamhuri ya muungano ambae kwa sasa ni rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein imelipatia ufumbuzi suala la wafanya biashara kutozwa kodi mara mbili, lakini bado wafanyabiashara wa Zanzibar wanadai maamuzi ya kamati hiyo yamepuuzwa

MAMIA YA WAISLAMU WAFUATILIA KESI YA KUCHOMWA MOTO QUR-ANI TUKUFU

Mamia ya wafuasi wa dini ya kiislamu leo wamejitokeza katika hakama ya wilaya mwanakwerekwe kusikiliza kesi ya mtuhumiwa wa anayedaiwa kuchoma moto msaafu na juuzuu za dini ya kiislamu.

Kesi hiyo iliyokuwa ikiongozwa na waendesha Mashtaka Hamis Jafar Mfaume ,Othman Kassim na Raya Mselem wamewasikilia mashahidi watatu waliotoa ushahidi huo ikiwa ni pamoja na Tausi Abdallah mwenye umri wa miaka 34,Khafidh Kassim mtoto mwenye umri wa miaka 12 na Saidi Omar  Hamad mwenye umri wa miaka 57.

Waendesha mashtaka hao wamedai kuwa mshitakiwa Ramadhan Hamda Tuma mwenye umri wa miaka 28 Mkaazi wa Mombaza Wilaya ya Magharib  alitenda makosa mawili ikiwemo kufanya kitendo cha uvunjifu wa amani kinyume na sheria za Zanzibar .

Hata hivyo Kosa la Pili la Mshitakiwa huyo ni kukashifu dini kinyume na kifungu cha sheria cha 117 na 27 sheria namba 6 ya mwaka 2004 .

Imedaiwa Mahakamani hapo Novemba 16 mwaka huu majira ya saa mbili Usiku Mombasa Wilaya ya Magharib mshitakiwa huyo alichoma moto hadharani Msahafu na Juzuu ya dini ya kiislam.

Hata hivyo Katibu wa Mufti ambae pia alifika Mahakamani hapo aliwataka waislamu kuwa na moyo wa subira wakati shauri hilo likiendelea mahakamani.

SMZ BADO HAIJAIMARISHA HAKI ZA BINADAMU KWA WAFUNGWA

Serikali ya mapinduzi Zanzibar imeelezewa bado haijafikia vigezo vya umarishaji wa haki za binadamu kwa watu wanaotumikia adhabu za kifungo katika vyuo vya mafunzo na wale walioekwa kizuizini.

Washiriki waliohudhuria mafunzo ya haki za binadamu na mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa yaliyofanyika hoteli ya Ocean View wamedai wanafunzi wa vyuo hivyo wanakosa lishe bora, uhuru wa faragha na kuabudu pamoja na upatikanaji wa taarifa.

Wamesema pamoja na kunyimwa haki hizo wanafunzi hao pia wanavishwa mavavi mafupi yanayokwenda kinyume na maadili yao na hali hiyo wameitaja ni uvunjaji wa haki za binadamu.

Mafunzo hayo yaliowashirikisha maafisa wa polisi, vikosi vya SMZ na waandishi wa habari pia vyombo vya sheria ikiwemo mahakama na jeshi la polisi vimedaiwa kuchangia uvunjaji wa haki za binadamu kwa kuchelewesha ushahidi na utowaji wa hukumu.

Akitoa ufafanuzi wa madai hayo mratibu wa vyuo vya mafunzo Zanzibar Mussa Issa amesema suala la lishe bora kwa wanafunzi hao limepatiwa ufumbuzi kwa kutolewa mikate ya bofulo na chai wakati wa asubuhi na chakula cha mchana.

Amesema wanafunzi wa vyuo vya mafunzo pia wanapewa fursa za kuwasiliana na familia zao kwa njia ya barua, kuhudhuria misiba, kutoa idhini ya ndoa na kupata taarifa kwa njia ya redio na televisheni.

Hata hivyo mratibu huyo amekiri kuwepo kwa ndoo ya kwendea haja kubwa wakati wa usiku na ufinyu wa malazi kutokana na vyuo vya mafunzo nchini kujengwa tokea utawala wa kikoloni.

Amesema hivi sasa Idara ya vyuo vya mafunzo Zanzibar inaendelea na mipango ya kujenga vyuo vipa vya mafunzo vitakavyokuwa na miundo mbinu ya kisasa ya utowaji wa huduma.

Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na afisi ya mkurugenzi wa mashataka Zanzibar na kudhaminiwa na shirika la maendeleo la umoja wa mataifa UNDP.