Eneo la kisiwa cha Mnemba Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewagiza watendaji wa serikali wakiwemo masheha waliohusika na ugawaji wa ardhi kinyume na sheria kurejesha fedha walizouzia na kufuta nyaraka walizozitoa.

Makamo wa pili wa rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi amesema iwapo watendaji hao hawatotekeleza agizo hilo watafukuzwa kazi.

Akizungumza na wananchi wa jimbo la Kitope amesema Serikali itaendelea kuwatumikia wananchi na kuhakikisha hadhulumiwi haki zao na viongozi wanaotumia nyadhifa zao kwa maslahi yao binafsi.

Balozi Iddi amesema serikali imeliona kero hilo la ardhi ambapo wananchi wananyang’anywa ardhi ovyo au eke zao bila ya kufuatwa taratibu za kisheria au idhini za wamiliki kama viwanja vya michezo na maeneo ya wazi.

Amesema serikali itaendelea kulishughulikia tatizo hilo ili kuona wananchi walionyanganywa aradhi zao na eka wanapata haki zao au kurejeshewa ardhi zao.

Hii ni mara ya kwanza kwa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar kutoa tamko hilo, huku kukiwa na malalmiko mengi ya wananchi wanaonyanganywa maeneo yao hasa katika sehemu za ukanda wa pwani ulioshamiri ujenzi wa hoteli za kitalii.

Advertisements