Hospitali ya mnazimmoja inayotarajiwa kupandishwa daraja kuwa hospitali ya rufaa

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuifanya hospitali ya Mnazi Moja kuwa hospitali ya Rufaa.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na kikao cha pamoja cha mazungumzo na viongozi pamoja na watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ikiwa ni mwanzo wa mtiririko wa mikutano Wizara zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kikao hicho kilichofanyika Ikulu mjini Zanzibar,  kilihudhuriwa na Makamo wa Kwanza na Rais, Mhe. Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Balozi Seif Ali Idd, ambapo Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya lengo hilo la kuiimarisha hospitali hiyo ya MnaziMmoja pia, baadhi ya hospitali kuzipandisha daraja na kuwa  hospitali za Wilaya na Mikoa.

Katika mazungumzo hayo, Dk Shein alieleza kuwa juhudi za makusudi zitafanywa na Serikali yake anayoiongoza ya kuhakikisha sekta ya afya inaimarika ikiwa ni pamoja na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote zinazoikabili sekta hiyo ikiwa ni pamoja na maslahi kwa wafanyakazi wake, vifaa na majengo ya hospitali na taasisi za Wizara hiyo.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa mashirikiano ya pamoja yanahitajika katika kuendeleza sekta ya afya nchini na kusifu hatua iliyofikiwa katika sekta hiyo hivi sasa na kuahidi kuiendeleza zaidi kwa mashirikiano ya pamoja na viongozi pamoja na watendaji wa Wizara hiyo kwa manufaa ya wananchi wote.

Nao viongozi na watendaji wa Wizara ya Afya walimueleza mafanikio yaliofikiwa katika sekta hiyo sanjari na changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na kueleza mikakati waliyoiweka katika kupambana na changamoto hizo.

Pamoja na hayo, watendaji hao wamemuahidi Dk. Shein kuwa wataendeleza mashirikiano ya pamoja katika kuimarisha sekta hiyo ya afya

Advertisements