Aliekuwa mgombea mwenza wa urais wa jamhuri ya muungano Tanzania kupitia chama cha APPT-MAENDELEO Rashid Mchenga amesema katiba ya Zanzibar haijajitosheleza katika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na inahitaji kufanyiwa marekebisho tena.

Akizungumza katika mafunzo juu ya serikali ya umoja wa kitaifa yaliofanyika hoteli ya Ocean View amesema ulimwengu unafahamu Zanzibar ina mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa, lakini amedai kinachonekana ni serikali ya mseto kwa kuvishirikisha vyama vya CCM na CUF pekee katika serikali hiyo.

Mchenga ambae ana mpango wa kumfikisha mahakamani mwanasheria mkuu wa serikali ili kutoa tapsiri sahihi ya serikali ya umoja wa kitaifa, amesema iwapo hataridhishwa na shauri lake hilo suala hilo atalipeleka katika tume ya haki za binadamu.

Nae katibu wa baraza la wawakilishi Ibrahim Mzee akizungumza katika mafunzo hayo amesema kifungu cha tisa cha katiba ya Zanzibar kinaeleza mamlaka ya kuendesha nchi yako kwa wananchi wenyewe.

Amesema uteuzi wa baraza la mawaziri uliofanywa na rais wa Zanzibar umezingatia matakwa ya katiba kwa vile wananchi wamevichagua vyama vya CCM na CUF kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Ibrahimu amesema vyama vya siasa visitegemee kuingizwa serikali bila ya kukubaliwa na wapiga kura, hivyo amevitaka vyama hivyo kufanya kazi ya siasa kwa kuuza sera zao kwa wananchi.

Kwa mujibu wa marekebisho ya kumi ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 vyama vya siasa vitakavyounda serikali ya umoja wa kitaifa vinapaswa kuwa na uwakilishi wa wananchi ndani ya baraza la wawakilishi.

 

 

Advertisements