Bendera ya KOrea ya Kusini

KOREA Kusini imeeleza azma yake ya kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo cha umwagiliaji maji.

Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania Mhe. Young-Hoom Kim aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.

 

Katika mazungumzo hayo, Balozi Kim alimueleza Dk. Shein kuwa tayari Ripoti ya upembuzi yakinifu ya mradi wa umwagiliaji maji imefikia pazuri na itakamilika hivi karibuni.

 

Alieleza kuwa Korea Kusini imeridhishwa na mashirikiano inayoyapata katika taratibu na mikakati ya kuimarisha mradi huo wa umwagiliaji maji hapa Zanzibar.

 

Aidha, Balozi huyo alimuhakikishia Dk. Shein kuwa nchi yake itaendeleza uhusiano na ushirikiano na Zanzibar.

 

Balozi Kim alisema kuwa ana matumaini makubwa ya mafanikio ya maendeleo kutokana na uongozi wa Dk. Shein na kumueleza kuwa nchi yake itaendelea kumuunga mkono na kutoa ushirikiano wake kwa Zanzibar ili kufikia malengo yaliokusudiwa.

 

Pamoja na hayo, Mhe. Kim alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake imevutiwa na hatua za Zanzibar za kuwa na  Maeneo huru ya kiuchumi na kuahidi kuwa Balozi wa nchi yake kuitaingaza Zanzibar kutokana na sifa ilizonazo.

 

Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uchumi wa Zanzibar na kusisitiza kuwa kutokana na nchi yake kuimarika kitekonolojia hatua hiyo itasaidia kuendeleza miradi hapa Zanzibar.

 

Katika maelezo yake pia, Balozi Kim alipongeza hatua zilizofikiwa katika kuimarisha sekta ya utalii na kuahidi kuitangaza Zanzibar kiutalii sanjari na kutoa mashirikiano yake katika kuimarisha sekta ya afya hapa Zanzibar.

 

Akieleza juu ya uimarishaji wa chuo cha kilimo cha Zanzibar, Balozi Kim alieleza kuwa chuo hicho ni muhimu katika kuendeleza sekta ya kilimo hapa Zanzibar na kueleza kuwa nchi yake itaangalia njia za kukisaidia chuo hicho ili kizidi kuimarika.

 

Nae  Dk. Shein alitoa pongezi na shukurani kwa Korea Kusini kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar hatua ambayo amesema itaweza kukuza mashirikiano katika sekta mbali mbali za kimaendeleo.

 

Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano kati yake na Korea Kusini na kusema kwamba hatua ya nchi hiyo kuunga mkono kilimo cha umwagiliaji maji itaiwezesha Zanzibar kupunguzakwa kiasi kikubwa uagizajiwa chakula hasa mchele kutokana na kukuza kilimo cha mpunga

 

Katika maelezo hayo, Dk. Shein alisema kuwa anamatumaini makubwa kuwa iwapo mashirikiano yataimarishwa kwa pande mbili hizo mafanikio makubwa yatapatikana katika sekta zote za maendeleo na kiuchumi.

 

Alieleza kuwa hatua hiyo ya Korea kusini  ya kushirikiana katika kuimarisha sekta ya kilimo itasaidia  kukiimarisha kilimo pamoja na sekta nyenginezo na kusisitiza kuwa jambo muhimu kwa wakulima ni kuwapa elimu juu ya sekta ya kilimo.

 

Dk. Shein alieleza kwamba  mbali ya kuimarisha sekta ya kilimo pia, Zanzibar imeweka eneo la maeneo huru ya kiuchumi kwa ajili ya uwekezaji na kutoa fursa kwa nchi hiyo kuja kuekeza Zanzibar.

 

Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya pamoja na sekta ya utalii na kueleza kufarajika kwake na azma ya Balozi Kim kuitangaza Zanzibar kiutalii huko nchini mwake.

Advertisements