Wafanyakazi wa ofisi ya Naibu Mufti Pemba, wamesema wanakabiliwa na wakati mgumu katika utendaji wa kazi zao ikiwemo kufuatilia migogoro ya kidini kutokana na ukosefu wa vitendea kazi.

Wafanyakazi hao wamesema matatizo hayo hasa usafiri yamekuwa yakikwamisha majukumu yao ya kutoa huduma kwa wananchi.

Wakizungumza na waziri wa sheria na utawala bora Abubakar Khamis Bakar kisiwani humo pia wameiomba wizara hiyo kutowa fursa sawa za mafunzo kati ya wafanyakazi wa ofisi hiyo kwa Unguja na Pemba.

Wamesema hali hiyo imesebabisha ushirikiano mdogo kwa watendaji wa ofisi kati ya Unguja na Pemba, na wale wanaokwenda kisiwani Pemba kikazi wanafanya kazi zao bila kuwashirikisha wenzao wa Pemba.

Nae waziri Bakar, amewataka wafanyakazi wa Wizara hiyo Kisiwani Pemba, kufanya kazi kisheria ili kutowa huduma bora kwa Wananchi.

Amesema maslahi ya Wafanyakazi ikiwemo, vitendea kazi na mafunzo yanashughulikiwa kupitia wizara maalumu ya utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Taasisi ambazo zimekutana na waziri huyo ni katiba na sheria, afisi wa mkurugenzi wa mashtaka, kamisheni ya wakfu na watendaji wa afisi kuu ya wizara hiyo Pemba .

Advertisements