HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI KATIKA UFUNGAJI WA MKUTANO WA NNE WA BARAZA LA WAWAKILISHI, TAREHE 28 JANUARI 2011

Balozi Seif Idd akilihutubia baraza la wawakilishi

Mheshimiwa Spika, kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenye wingi wa rehema kwa kutuwezesha kutekeleza kwa ufanisi mambo yote tuliyoyapanga katika mkutano wetu huu wa nne kwa salama na amani na kutekeleza wajibu wetu katika Baraza lako tukufu.  Nakushukuru wewe Mhe. Spika kwa kuendesha mkutano huu kwa mafanikio makubwa.

 

Halikadhalika, nawashukuru sana Waheshimiwa Wawakilishi wenzangu kwa kuuliza maswali mazuri kuhusu utendaji wa shughuli za Serikali na kutoa maoni yao wakati wa kujadili miswada na hoja mbali mbali zilizowasilishwa hapa Barazani. Vile vile, nawashukuru kwa dhati Waheshimiwa Mawaziri kwa kuyajibu vizuri na kwa ufasaha maswali yaliyoulizwa pamoja na kutoa ufafanuzi wa hoja mbali mbali.  Ni matumaini yangu kwamba wananchi wamefaidika na majibu hayo.

 

Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu jumla ya maswali ya msingi 90 yaliulizwa na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri pamoja na maswali mengi ya nyongeza.  Pia Baraza lilijadili hoja mbili, taarifa mbili na kufanya semina mbili kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Halikadhalika Baraza lilipitisha Miswada miwili ya Sheria ambayo ni kama ifuatayo:-

1.        Mswada wa Sheria ya Kuweka Masharti ya Uendelezaji, Ukuzaji na Uwekaji wa Viwango Bora wa Bidhaa na Usimamizi wa Huduma Zinazolingana na hizo na

2.        Mswada wa Sheria ya Kuweka Miundo, Uendeshaji na Usimamizi wa Utumishi wa Umma Zanzibar na Mambo Mengine yanayohusiana na Hayo.

 

Mheshimiwa Spika, Mswada wa kwanza kujadiliwa katika Baraza lako Tukufu ulikuwa na lengo la kuimarisha huduma za biashara kwa pande zote mbili, mnunuzi na muuzaji na kuimarisha hadhi ya nchi yetu kibiashara.  Kama tunavyofahamu kuwa kwa muda mrefu Zanzibar ilikuwa ikijulikana kuwa kitovu cha biashara kwa Kanda ya Afrika Mashariki kabla na baada ya Mapinduzi.  Jambo hili lilipelekea wafanyabiashara na watu wa mataifa kadhaa kuja kutembelea na kufanya bishara zao hapa Zanzibar.  Hali hiyo ndio iliopelekea hivi leo kuwa na makabila mchanganyiko yenye kupendeza na haiba katika jamii yetu.

 

Katika siku za hivi karibuni hali hii ilibadilika na nchi yetu kukaribia kuwa jaa la makachara kwa bidhaa zisizokuwa na viwango vinayohitajika na pia watu wetu kuhatarishiwa maisha kwa kuingizwa nafaka na bidhaa zilizopitwa na muda wa matumizi.  Hii ni hatari tena kubwa sana sio kwa afya ya wateja na walaji pekee bali hata katika suala zima la kuimarisha uchumi wetu.  Matokeo yake hadhi ya ufanyaji biashara imepotea na hivi sasa tunalazimika kuchukuwa juhudi kubwa ili kuweza kuirudisha hadhi hiyo jambo ambalo linahitaji muda na gharama kubwa.

 

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, moja ya mitaji yetu mikuu ni utalii, huduma bora, uwaminifu na biashara, kwa maana hiyo suala la kuwa na viwango vya biashara vinavyokubalika lina umuhimu mkubwa kwetu.

Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kwa kusema kuwa Zanzibar bila ya biashara haijakamilika, hata kihistoria umaarufu wa Visiwa vya Zanzibar umetokana na biashara. Hivyo ndiyo kusema kuwa biashara ndio mhimili muhimu wa kuinua fursa za ajira hapa Zanzibar na ndio sehemu kubwa ya mapato na nguvu za kiuchumi kwa watu wa Zanzibar na itaendelea kuwa hivyo kwa muda mrefu ujao.  Kutokana na hali hiyo, Serikali lazima iendelee kuchukua jukumu la kusimamia kazi ya uendelezaji, ukuzaji na uwekaji wa viwango na ubora wa bidhaa zinazoingia au kutoka nchini.

 

Nimepata faraja kuona kuwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu wametumia fursa hii kuujadili kwa kina mswada huu.

 

Madhumuni ya sheria hii, Mhe. Spika, ni kukuza shughuli za uwekezaji nchini pamoja na kudhibiti viwango na ubora wa bidhaa zinazoingizwa na zile zinazozalishwa nchini. Kwa mujibu wa mswada huu hapana shaka kazi ya Taasisi husika itaweza kufanyika kwa ufanisi zaidi, ikitiliwa maanani kuwa juhudi za kuimarisha ubora wa viwango vya bidhaa mbali mbali kwa ajili ya biashara ni suala muhimu.

 

Mheshimiwa Spika, ni muhimu kuainisha kuwa chini ya mswada huu, Serikali itakuwa na mamlaka ya kuunda Vyombo au Taasisi za kisheria zitakazotumiwa kuhakikisha kuwa wafanyakazi wa Taasisi hizo wanawajibika katika kudhibiti ubora wa bidhaa, ukaguzi wake pamoja na kuimarisha mashirikiano na wadau wengine ndani na nje ya nchi.

 

Aidha, sheria hii itaweka mazingira mazuri katika mfumo wa ushindani wa kibiashara na kushajiisha uzalishaji wa bidhaa za ndani na kuiwezesha sekta binafsi kwenda sambamba na kufuata masharti ya viwango vya kimataifa kwa kuzingatia mpango wa kitaifa wa usafirishaji bidhaa nje ya nchi.

 

Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili tukufu, wenyewe ni mashahidi wa kuwepo kwa mtindo hivi sasa kwa baadhi ya wafanyabiashara ndogo ndogo kuuza bidhaa zilizopitwa na wakati kwa punguzo kubwa la bei ili kuwavutia wateja ambao pasi na kujuwa kuwa wanahatarisha maisha yao na familia zao.

 

Mheshimiwa Spika, maeneo kama vile Darajani na Soko kuu la Zanzibar kumeshamiri kuwepo kwa biashara ya bidhaa hizo zilizopitwa na wakati kama vile juisi za mapaketi, tungule za vibati, mafuta ya kupikia, samli na hata vipodozi.  Tabia hii sio nzuri inaweza kuhatarisha afya za wananchi wetu.  Wananchi hawana budi kuwa waangalifu wa bidhaa za aina hii.

 

Mheshimiwa Spika, Mswada wa pili kujadiliwa katika Baraza hili tukufu ulikuwa mswada wa Sheria ya kuweka miundo, uendeshaji na usimamizi wa utumishi wa umma, ambao mtakubaliana nami kuwa mswada huu nao ni mzito sana kwa vile unagusa moja  kwa moja  masuala ya maslahi ya rasilimali watu katika jamii yetu.

 

Rasilimali watu ndio yenye mchango mkubwa katika njia za kuinua au kuangusha uchumi wa nchi, kwa sababu hata ikiwa kutakuwepo na nyenzo bora za mapato, kama hakuna watendaji bora na makini wa kuyasimamia vyema katika ukusanyaji na utunzaji wake, Serikali haitafaidika nayo.  Aidha, utendaji kazi katika uzalishaji ukiwa hafifu tija haitopatikana. Kwa mnasaba huo suala la utumishi wa umma na nidhamu kazini linahitaji mazingatio makubwa sana.  Kwa hivyo, mswada huu umekuja katika wakati muafaka na ninawashukuru sana Waheshimiwa wajumbe wa Baraza hili tukufu kwa kuupa mswada huu uzito unaostahili.

 

Mheshimiwa Spika, ni jambo lililowazi kabisa kuwa kutokana na sababu mbali mbali za kiutumishi yakiwemo maslahi ya wafanyakazi, utendaji wetu Serikalini umeshuka na hivyo kupunguza ufanisi na tija kwa kiasi fulani.  Hili halihitaji mwenge wa kulimurika liko wazi kwa sababu baadhi ya athari zake zinaonekana.  Mathalan tumekuwa tukiambiwa hatuna wataalamu wa kutosha katika fani mbali mbali, lakini Serikali inachukuwa juhudi kila siku kusomesha watu wake, hata hivyo kutokana na mazingira magumu ya utumishi tuliyokuwa nayo wengi kati yao hukosa uzalendo na kukimbilia nchi jirani jambo ambalo huzidisha matatizo kwetu.

 

Mambo haya hatutaki yaendelee kutokea ndio maana ya kuupitisha mswada huu kwa kauli moja.  Kwa kufanya hivyo, jamii imeona malengo yetu na naamini tutafanikiwa.  Kama Wachina wasemavyo, “safari ya maili elfu moja huanza na hatua moja” sisi tumeanza naomba tuwe na subira ili tufikie malengo yetu.  Natoa wito kwa wafanyakazi wote Serikalini kuona juhudi zetu hizo na kuziunga mkono kwa kutimiza wajibu wao ili hayo tuliyakusudia yafanikiwe.

 

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema kuwa mkutano wetu huu ulitanguliwa na hoja mbili, hoja ya kwanza ilikuwa inahusu marekebisho ya kanuni za Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.  Hoja hii imekuja kufuatia mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yaliofanywa mwaka jana yaliowezesha kuwa na muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

 

Nashukuru kuwa marekebisho hayo yamefanyika vizuri na yametupa uwezo wa kuendesha vikao vyetu kwa ufanisi bila ya matatizo.  Ni matumaini yangu kwamba kila Mjumbe atazipitia kwa makini kanuni hizi.

 

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ilikuwa kujadili Hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein aliyoitoa tarehe 11 Novemba, 2010 wakati alipolizindua Rasmi Baraza hili la Nne la Wawakilishi la Zanzibar. Katika kujadili hoja hiyo, tumejionea wenyewe umuhimu wa hotuba hiyo ambayo sisi Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi tumeiona kuwa ni Dira ya kutuonyesha njia ya tunakotaka kwenda.  Kwa hapa sina la kuliongeza zaidi ya kutoa shukrani kwa Wajumbe wote waliochangia, kwa michango yao mizuri ambayo imewapa wananchi wetu matumaini makubwa juu ya Serikali yao.

 

Mheshimiwa Spika, ni jambo la kawaida kwa Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili kujifunza kwa njia za Semina kabla ya kujadili baadhi ya miswada na mambo yanayohitaji kuwasilishwa hapa Barazani.   Hivyo, Ndugu Wajumbe safari hii walipata fursa ya kuelimishana kwa njia ya Semina Mswada wa Sheria unaohusiana na mambo ya Utumishi wa Umma na semina ya pili ambayo inategemewa kufanyika Jumapili tarehe 30 Januari, 2011 itakayoelezea masuala ya Maendeleo ya Mawasiliano ya Simu Zanzibar kupitia Kampuni ya ZANTEL.  Napenda kuishukuru sana Kampuni ya ZANTEL kwa kututayarishia semina hiyo ambayo itatuelimisha kwa kina mambo wayafanyayo.

 

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya naomba uniruhusu nieleze suala muhimu la kuhusu biashara ndogo ndogo Darajani (Dada Njoo).  Serikali ilikuwa ikipata malalamiko kutoka kwa wananchi kutokana na usumbufu na bughudha wanazopata wanafunzi wa Skuli za Darajani na Vikokotoni.  Kwa kuepuka malalamiko hayo Serikali imetenga eneo la Saateni na kutengenezwa eneo maalum kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo ili kuwapa utulivu wanafunzi wetu.  Ndiyo maana Serikali kupitia Baraza la Mji wa Zanzibar imewataka wafanyabiashara hao kuondoka katika eneo hilo.   Natumia fursa hii kuwapongeza kwa dhati Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko na Mkurugenzi wa Baraza la Mji wa Zanzibar kwa kuchukua hatua madhubuti katika kulisimamia suala la kuwarejesha wafanyabiashara hao Saateni kutoka eneo hilo la Darajani ili kuwapa nafasi ya kutosha na kuwawezesha vijana wetu kupata elimu kwa utulivu.  Aidha, nalishauri Baraza la Mji la Zanzibar kuliendeleza eneo hilo ili liwe zuri, safi na lenye mazingira bora.

 

Kwa sababu ya kutaka kulitunza vizuri eneo hilo, Serikali kupitia Baraza lako Tukufu inapiga marufuku kwa mtu yoyote kufanya biashara katika eneo hilo. Serikali kupitia Baraza la mji wa Zanzibar itajitahidi kuliboresha eneo hilo kwa kuweka bustani ya kupumzikia wananchi kama ilivyo katika ramani ya Mipango Miji.

 

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba wale wote wanaoendelea na mtindo huu wa kulivamia eneo hilo kwa shughuli za kibiashara waache mara moja, na naziagiza Taasisi zote zinazoshughulikia masuala ya biashara pamoja na utoaji wa vibali katika maeneo hayo na hata yale ya maeneo ya ng’ambo kama vile Soko la Mwanakwerekwe kuwachukulia hatua wafanyabiashara wenye tabia hii mbaya ya kukiuka taratibu za Mipango Miji.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ni dira kwetu. Hotuba hii imetusafishia na kutuonyesha njia ya wapi wananchi wa Zanzibar wanakotaka kwenda na namna gani tutawaongoza kufika huko. Tunataka kujenga Zanzibar yenye mshikamano imara ambao siku zote utajali zaidi maslahi ya jamii yetu kuliko ya mtu mmoja mmoja, vikundi vya kijamii au vyama vyetu vya siasa.  Napenda kuwaasa Viongozi wenzangu katika kipindi hiki cha miaka mitano tuwajibike kwa kufuata na kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Maslahi ya wananchi kwanza, na tufanye kazi kwa bidii yetu yote.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi kirefu tangu tuanze mchakato wa uchaguzi hadi sasa tumekuwa tukihubiri haja ya kujenga jamii yenye maelewano, umoja na mshikamano.  Takriban kampeni za vyama vyetu vyote zilitawaliwa na wito wa kujenga Zanzibar mpya yenye mshikamano wa dhati.  Hivyo, marekebisho ya miswada tuliyoijadili katika kipindi chote cha Baraza lako Tukufu ina lengo la kuhakikisha ubora wa kiwango cha utumishi pamoja na kuimarisha utawala bora.  Jambo la msingi ni kuelewa kuwa yote hayo ni miongoni mwa vigezo vya kuweza kupima kiwango cha mshikamano katika jamii. Hivyo, napenda kuwaomba viongozi wenzangu kuwa tuondoke hapa leo tukiwa na lengo moja la kutekeleza kwa vitendo ahadi zetu za kujenga mshikamano, umoja, maelewano na upendo ambao tuliwaahidi wananchi wetu na kama tulivyouonyesha ndani ya Baraza hili katika mkutano wake huu wa nne.  Tuondoke hapa leo tukiwa na moyo huo huo.

Mheshimiwa Spika, uhusiano wa amani na uchumi ni mambo yanayotegemeana sana. Ni mategemeo ya wananchi wengi baada ya marekebisho ya shughuli za utumishi Serikalini, wangependa kuona kuwa matokeo ya marekebisho yake yatawasaidia kuimarisha maisha yao na kuwa na matumaini zaidi. Ni matumaini yangu kuwa nyote hapa mtakubaliana nami nikisema kuwa Serikali ya awamu ya saba imekusudia kujenga uchumi imara ambao utaondokana na utegemezi kwa kutambua wazi kuwa bila ya uchumi imara amani yetu tunayojivunia hivi sasa itakuwa mashakani. Lakini kabla ya yote hayo ni muhimu kuimarisha usimamizi wa kiwango cha uwajibikaji.

Mheshimiwa Spika, kama inavyoeleweka kuwa siku zote shida, maradhi na njaa hujenga hasira ambazo hatimaye huzaa machafuko ndani ya jamii. Katika kujenga uchumi imara, jitihada za Serikali kwa ushirikiano na wananchi wake ndio miongoni mwa mambo ya msingi yanayohitajika katika kujenga Taifa letu hivi sasa.  Kwa upande wangu nitajitahidi kwa uwezo wangu wote nikishirikiana na Viongozi wenzangu kusimamia kazi na changamoto zinazotukabili katika azma ya kujenga maisha bora kwa wananchi wetu kwa kuongeza kiwango cha uwajibikaji ndani ya Serikali.  Naomba viongozi wenzangu kutokubali kushindwa katika kusimamia azma hii kwani naamini kwa dhati kuwa tukiwa pamoja tutashinda. Kwani sote tunatambua wazi kuwa umoja ni nguvu na penye wengi haliharibiki jambo.

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako sasa naomba nieleze machache kuhusu kadhia mbali mbali zinazolikabili Taifa letu ambazo zikiachwa bila ya kuchukuliwa hatua madhubuti tunaweza kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa nchi yetu kutokana na wananchi kukosa imani na viongozi pamoja na Serikali yao.

 

Mheshimiwa Spika, moja ya kadhia hizo ni suala la ardhi.  Sote tunaelewa kwamba ardhi ni uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi yoyote ile.  Ardhi, ikitumika vizuri kutasaidia kuleta maendeleo ya kiuchumi na hasa katika sekta za kilimo, viwanda, biashara na uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, Upimaji na ugawaji wa ardhi hauna utaratibu na utaratibu uliyowekwa baadhi ya nyakati haufuatwi. Matokeo yake nchi yetu kukumbwa na migogoro mingi ya ardhi.  Hakuna hata Mkoa mmoja kati ya Mikoa yetu mitano uliokuwa salama ambao hauna migogoro ya ardhi.  Kwa bahati nzuri, baadhi ya migogoro hiyo imeweza kutatuliwa kwa busara za Serikali za Mikoa.  Hata hivyo, bado ipo migogoro mingi ambayo bado kutatuliwa na migogoro hii kwa bahati mbaya inawahusu wananchi wa kawaida ama kwa kuporwa au kunyang’anywa ardhi zao ambazo wamekuwa wakizitumia kwa muda mrefu kwa kujikimu wao na familia zao na hasa zile ardhi za urithi.

 

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa rai kwamba juhudi zichukuliwe kati ya walalamikaji na walalamikiwa kuimaliza migogoro yao hiyo kwa amani na salama na muafaka kupatikana baina ya pande husika. Ningeomba Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Umeme kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kasoro hizo kwa haraka sana.

 

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za Serikali kukabiliana na migogoro ya ardhi na kutafuta namna ya kuitatua, natoa wito kwa Idara ya Ardhi na Upimaji kuyapima maeneo yote yanayomilikiwa kihalali na Taasisi za Serikali na kuyapatia hati ya umiliki ili kuondosha malalamiko ya baadhi ya Taasisi hizo kuvamiwa maeneo yao na wajanja wachache.  Kwa mfano, uvamizi wa maeneo yanayozunguka maskuli na vyuo mbali mbali Unguja na Pemba pamoja na kuvamiwa kwa mashamba yanayomilikiwa na Serikali.  Sambamba na hilo, naiagiza Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Umeme kuwapimia wananchi maeneo yao ambao kwa muda mrefu waliomba kufanyiwa hivyo ili waweze kupatiwa hati miliki.

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kila jitihada kutoa viwanja kwa wananchi kwa ajili ya kujenga makaazi yao.   Ni bahati mbaya sana kwa baadhi ya wananchi kuhodhi viwanja hivyo kwa madhumuni ya kuvifanyia biashara ya kuviuza kwa bei kubwa sana, hadi kufikia Shilingi Milioni 40 – 50.  Viwanja ambavyo wao walipimiwa na Serikali kwa kiasi cha shilingi 150,000/= tu.  Kwa kupitia Baraza lako Tukufu, Mhe. Spika, napenda kutoa onyo kwamba mtindo huo uachwe.  Serikali hivi sasa itachukua hatua kwa mujibu wa sheria wa kuvirejesha Serikalini viwanja vyote vilivyopimwa na kugaiwa kwa wananchi ambavyo bado havijaendelezwa na muda wa kufanya hivyo kisheria tayari umeshapita.

Mheshimiwa Spika, ujenzi katika maeneo ya wazi ni jambo ambalo halikubaliki.  Siku chache za nyuma nilitoa onyo na leo narudia tena kusisitiza kupitia Baraza lako Tukufu kuwatanabahisha wananchi wasikubali kupimiwa au kuuziwa viwanja katika maeneo ya wazi au viwanja vya michezo.  Kufanya hivyo ni kujitafutia hasara ya bure kwa jengo lolote litakalojengwa katika maeneo hayo.

 

Mheshimiwa Spika, suala la uharibifu wa mazingira na hasa uchimbaji wa mchanga kiholela ni tatizo jingine linalohitaji kuchukuliwa hatua za haraka.  Hali ya mazingira yetu maeneo yanayochimbwa mchanga hasa Mkoa wa Kaskazini, Unguja si ya kuridhisha. Wafanyabiashara wanaochimba mchanga wamekuwa ni tatizo katika kuharibu mazingira yetu maeneo ya Donge, Kazole, Bumbwini, Kianga, Mbuzini na kwengineko.  Kote huko ardhi yake imebakia mashimo tu haifai tena kwa kilimo ma maeneo hayo hayatakarabatiwa haraka.

 

Mheshimiwa Spika, kwa muono wangu mtindo huu mbaya tunaoendelea nao si sahihi katika kulinda, kuhifadhi na kuyaendeleza mazingira ya maeneo yetu.  Sheria za utunzaji mzuri wa mazingira zipo, ni vyema zikafuatwa ili kuinusuru nchi yetu na majanga ya uharibifu wa mazingira.

 

Natoa wito kwa Mamlaka zinazoshughulikia mazingira kusimamia vyema sheria za mazingira na kuwatoza faini kali wale wote wanaochimba mchanga bila kufuata sheria, ikiwa ni pamoja na kutaifishwa kwa magari yao yanayotumika kubebea mchanga huo ambao huchimbwa katika maeneo yasiyoruhusiwa.

 

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa muda mrefu imekuwa ikihamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika miradi mbali mbali ya kiuchumi.  Nia ya kufanya hivyo ni kuiwezesha Serikali yetu kufaidika na uwekezaji huo kimapato na kukuza uchumi wake. Lakini kufaidika huko siyo kwa Serikali peke yake, bali hata wananchi pia ama kimapato au kiajira.  Kutokana na uhamasishaji huo wawekezaji wengi kutoka ndani na nje waliwekeza katika Sekta ya Utalii kwa kujenga mahoteli.  Mahoteli haya yalisaidia kutoa ajira kwa wananchi wetu na pia kuwawezesha kuuza bidhaa zao mbali mbali kwa mahoteli hayo ambazo zimekuwa zikitumiwa na wenye Mahoteli kuwahudumia wageni wao.

 

Kwa masikitiko makubwa Mhe. Spika, hoteli moja ambayo iko katika eneo la Kiwengwa, Venta Club imetelekezwa na wawekezaji wake wakiwaacha wananchi wengi kutowalipa mishahara yao na pia wale waliokuwa wanapeleka bidhaa mbali mbali kutowalipa fedha zao walizostahili. Wawekezaji hao wameacha deni la zaidi shilingi 600 Milioni.  Naziagiza ZIPA na Kamisheni ya Utalii wawafuatilie wawekezaji wa aina hii kuwadhibiti ili tabia ya namna hiyo iachwe.  Uwekezaji wa aina hii ambao siyo wa uaminifu, umewaacha wananchi wetu wamefilisika na kuwa katika hali ya umaskini badala ya kunufaika.  Hivi sasa Serikali inajaribu kuona namna inavyoweza kuwasaidia wananchi hao ili waweze kulipwa madeni yao.

Mheshimiwa Spika, kama tunavyojua maji ni uhai.  Pamoja na juhudi kubwa za Serikali kuwatatulia shida ya maji wananchi wake bado maeneo mbali mbali ya nchi yetu yanakabiliwa na tatizo la maji.  Bado juhudi mbali mbali zinafanyika katika kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma hii kwa uhakika.  Nawasihi wananchi wazidi kuwa wastahmilivu wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika jitihada za kutafuta suluhisho la kudumu juu ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama hapa Zanzibar.

 

Mheshimiwa Spika, tunalo tatizo kwa baadhi ya maeneo yanakabiliwa na nguvu ndogo za umeme (low voltage).  Ninafuraha kulieleza Baraza lako Tukufu kuwa tatizo hilo karibu litapatiwa ufumbuzi.  Hivi karibuni Shirika la JICA la Japan litaweka “transformer” mbili kubwa katika Kituo cha Umeme, Saateni ili kuongeza nguvu za umeme.  Aidha, Shirika hilo la JICA litasambaza waya mpya katika maeneo yote yenye matatizo ya nguvu ndogo ya umeme “Voltage drop”.  Kazi hizi zinatarajiwa kuanza mwezi wa Machi, 2011 na kumalizika mwezi wa Juni, 2013.  Mradi ambao utagharimu kiasi cha Dola za Kimarekani 33 Milioni chini ya msaada wa JICA.

 

Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza hotuba yangu, nachukuwa fursa hii kulipongeza kwa dhati Baraza lako Tukufu kwa kuendesha uchaguzi ulio huru na haki uliowezesha kukamilika kwa safu ya uongozi ndani ya Baraza letu.   Kwa niaba yangu binafsi na Wajumbe wa Baraza lako Tukufu napenda kuwapongeza kwa dhati kabisa.

Mhe. Ali Abdalla Ali    –        Kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia napeda kukushukuru tena wewe Mhe. Spika kwa kuliongoza Baraza letu kwa umahiri mkubwa.  Aidha, napenda kuwashukuru Wajumbe wote wa Baraza hili kwa ushirikiano wao mkubwa waliouonyesha katika kipindi chote cha majadiliano.  Nawatakia kila la kheri na safari njema ya kurejea nyumbani.

 

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu haya sasa naomba kutoa hoja ya kuliahirisha Baraza lako Tukufu hadi tarehe 23 Machi, 2011.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Advertisements