Walinzi katika bustani ya Forodhani wamelalamikiwa na watu wenye ulemavu wanaotumia baskeli za magurudumu matatu kwa kuwazuwia kuingia katika bustani hiyo.

Akitoa malalamiko hayo kupitia Zenji Fm radio mlemavu wa miguu Juma Abdalla Juma mkaazi wa Mkele amesema kitendo cha kuzuwia kilichofanya na walinzi hao kinamnyima haki zake za binadamu.

Amesema walinzi hao walimkatalia kuingia na baskeli yake hiyo ambayo anaitumia kutembelea kutokana na ulemavu wa miguu na kuiomba serikali kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu katika sehemu za umma

Nae mkurugenzi wa baraza la manispaa Zanzibar Rashid Ali Juma akitoa ufafanuzi wa madai ya mlemavu huyo amesema baraza hilo linazingatia hali za watu wenye ulemavu, lakini baadhi yao wamekuwa wakivunja utaratibu kwa kuegesha baskeli zao sehemu zisizostahiki.

Amesema wengi wao wanaweka baskeli zoa katika bustani na inapotokea hali hiyo walinzi wa bustani hiyo wanalazimika kuchukua hatua

Bustani ya Forodhani iliyofanyiwa matengenezo kwa gharama ya dola za Marekani milioni 3.3 chini ya ufadhili wa mfuko wa utamaduni wa Aga Khan na benki ya dunia imekuwa kivutio cha kupumzikia kwa wenyeji na wageni.

Advertisements