Archive for February, 2011

WAKULIMA KASKAZINI UNGUJA WAKUMBWA NA UKAME

Wakulima wa mpunga wa mabonde ya Mkoa wa Kaskazini Unguja yaliokumbwa na ukame wameiomba Serikali kuwapatia mbegu ndogo wakati wa mvua za Masika ili wazipande tena katika konde zao zilizoharibika kwa jua kali.

 

Ombi hilo la Wakulima liliwasilishwa kwenye ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika mabonde ya Mpunga ya Kilombero, Kibokwa, Machekechuni na Kibonongwa alipofika kuwapa pole kufuati mpunga wao kuunguliwa na jua kali.

 

Akitoa maelezo kuhusu kadhia hiyo mkulima Bw. Ame Haji na wenzake walimpongeza Mhe Balozi Seif kwa uwamuzi wake wa kuwatembelea na kuwafariji, jambo ambalo limeonesha anavyojali shida za wananchi.

 

Halikadhalika, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maliasili Ndg Afani Othman Maalim alitoa ufafanuzi juu ya maharibiko hayo ya konde za mpunga na pia alieleza maandalizi yaliokwishafanywa na Wizara yake kukabiliana na tatizo hilo.

 

Kwa upande wake Mhe Makamu wa Pili wa Rais alieleza kusikitishwa kwake na kadhia hiyo na kusema kuwa ni mambo ya Mungu hayakutarajiwa bali mabadiliko ya hali ya hewa yamebadilisha miongo na mvua. Pia alikubali ombi la wakulima la kuwapatia mbegu na pembejeo.

 

Kuhusu umuhimu wa kilimo Mhe Balozi Seif aliwaambia wakulima kuwa kazi yao ya kilimo ni muhimu sana kwa taifa kwakuwa wanaisaidia Serikali kupunguza matumizi ya uwagiziaji na pia kutotegemea sana vyakula kutoka nje.

 

Aidha. baadhi ya wakulima walieleza tatizo la maji safi linalowakabili wakati huu wa kiangazi. lakini walisifu matayarisho mazuri ya mwaka huu kwa kulimiwa na matrekta mapema.

MAHAKAMA ZANZIBAR YATOA KIFUNGU CHA MIEZI 24 KWA MTU ALIECHOMA QUR-ANI

Mahakama ya Wilaya Mwanakwerekwe imemuhukumu Ramadhan Handa Tuma mwenye umri wa miaka 28 kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miezi 24 kwa kupatikana na  kosa la kuchoma moto Msahafu na Juzuu za dini ya Kiisilamu.

Hukumu hiyo imetolewa na hakimu Khamis Ali Simai  mara baada ya kumtia hatiani mshitakiwa huyo dhidi ya mashitaka ya kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani pamoja na kukashifu dini.

Akitoa hukumu hiyo, hakimu Khamis amesema shitaka la kwanza la kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani atalipa faini ya shilingi 200,000 na endapo atashindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi sita.

Kosa la pili lililomkabili mshitakiwa huyo ni kukashifu dini, mahakama hiyo imempa adhabu ya kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi 18, na kufahamisha kuwa adhabu zote hizo zitakwenda sambamba.

Upande wa mashitaka ulioongozwa na Raya Issa Mselem, amesema haukuridhishwa na Hukumu hiyo na kusema kwamba anakusudia kukata rufaa dhidi ya adhabu iliyotolewa kwa shitaka la pili la kukashifu dini.

Hata hivyo Mwendesha mashitaka Raya Mselem ameomba itolewe adhabu kali dhidi ya mshitakiwa huyo  kutokana na kitendo alichokifanya ili iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia kama hiyo.

Kwa upande wake mshitakiwa huyo aliomba apunguziwe adhabu kwa madai ana familia inayomtegea akiwemo mke na mtoto, pamoja kusumbuliwa na maradhi ya tumbo.

Kwa mujibu wa mahakama hiyo, Ramadhan Handa Tuma alifanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani Novemba 16 mwaka jana Mombasa zanzibar ambapo kwa makusudi na bila ya halali alichoma moto msahafu pamoja na juzuu za dini ya Kiisilamu .

NORWAY KUSAIDIA MFUKO WA MAENDELEO YA VIJANA ZANZIBAR

Flag of Norway

Wizara ya ustawi wa jamii na maendeleo ya vijana, wanawake na watoto kwa kushirikiana na ubalozi wa Norway umezindua mfuko wa maendeleo ya vijana utakaosaidia miradi ya kiuchumi ya vijana.

Norway ambayo imeahidi kufadhili mfuko huo kwa kiasi kikubwa utatoa zaidi ya shilingi milioni 149 kila mwaka ili kusaidia upatikanaji wa ajira kwa vijana kupitia vikundi vya uzalishaji walivyoanzisha.

Akizungua mfuko huo waziri wa wizara hiyo Zainab Omar amewataka vijana kutumia mfuko huo ili kuongezewa fedha zaidi zitakazowezesha mfuko huo kutoa huduma zake nchi nzima

Nae waziri wa mazingira na maendeleo wa Norway Eric amesema lengo la kutoa msaada wa fedha hizo kila mwaka ni kuhakikisha vijana wanapafa nafasi za ajira ili kujiendeleza kiuchumi.

Hivyo amewataka kubuni miradi ya uzalishaji itakayowezesha kunufaika na mfuko huo.

Masharti ya kuomba fedha katika mfuko huo ni lazima vikundi vya vijana viwe na usajili, ripoti ya matumizi ya fedha ya kila mwaka na kabla ya kupatiwa fedha hizo vikundi hivyo vitapatiwa mafunzo

ZANZIBAR INAWEZEKANA KUWA NA TAASISI MOJA YA KODI-ZRB

Bodi ya mapato Zanzibar ZRB imesema mazungumzo ya Zanzibar kuwa na taasisi moja ya ukusanyaji kodi yanaendelea vizuri.

Mmsaidizi wa elimu kwa walipa kodi wa ZRB Safia Ishaq amesema mazungumzo hayo yanayoendelea katika ngazi za juu yamefikia katika hatua nzuri ili kuona wafanyabiashara wa Zanzibar wanalipa kodi katika taasisi moja badala ya mbili za sasa.

Hata hivyo amesema endapo kutakuwa na taasisi moja kodi zitakazolipiwa hazitabadilika, lakini mfumo huo wa kulipia kodi katika taasisi moja kutaondoa usumbufu kwa wafanyabiashara.

Safia amesema watalamu wengi wanaoishauri Zanzibar juu ya ukusanyaji wa kodi wamesema nchi ndogo kama Zanzibar kuwa na taasisi mbili za ukusanyaji kodi ni kikwazo kwa wafanyabishara kulipia kodi.

Kwa muda mrefu sasa wafanyabiashara wa Zanziar wanalalamikia kulipia kodi katika taasisi mbili za Bodi ya mapato Zanzibar ZRB na mamalaka ya mapato Tanzania TRA wakisema wanapata ufumbufu ikiwemo gharama za kuzifuata taasisi hizo kuwasilisha kodi za wananchi.

MKURUGENZI MANISPAA AMWAGIWA TINDI KALI

Jengo la afisi ya Manispaa Zanzibar

Mkurugenzi wa baraza la manispaa Zanzibar Rashid Alli Juma amepelekwa jijini Dar es salaam kwa matibabu zaidi baada ya kumwagiwa tindi kali na watu wasiojulikana usiku wa jana alipokuwa akitoka msikitini.

Akizungumza na ZENJ FM mstahiki Meya wa Manispaa ya Zanzibar Khatib Abdulrahman Khatib amesema mkurugenzi huyo ameumia zaidi usoni, kifuani, mikononi na mapajani.

Amesema kuwa hali yake inaendelea vizuri licha ya maumivu makali aliyoyapata kutokana na kumwagia tindi kali.

Akizungumza juu ya tukio hilo katibu msaidizi wa hospitali ya Mnazi mmoja Omar Abdalla Alli amesema mkurugenzi huyo amefikishwa hospitalini hapo majira ya saa 5.00 usiku.

Amesema daktari alimhudumia amethibitisha kwamba ameungua sehemu za usoni, kifuani na miguuni na amepelekwa katika hospitali ya Muhimbili mjini Dar es Salaam kwa matibu zaid.

Nae kamanda wa polisi mkoa wa mjini Magharibi Azizi Juma amesema tukio hilo limetokea majira ya saa 2.00 usiku wakati mkurugenzi huyo akiwa amekaa barazani baada ya kutoka msikitini kwa sala ya Isha.

Mtuhumiwa aliemwagia maji maji hayo yanayosadikiwa tindikali alifika karibu na mkurugenzi Rashid na kumwagia maji maji hayo

Hata hivyo hakuna mtu hata mmoja aliekamatwa kuhusiana na tukio hilo hadi sasa.

Hivi karibuni mkurugenzi huyo alisimamia kazi za kuondoa makontena ya biashara ya eneo la Darajani ili kupisha ujenzi wa bustani ya kupumzikia katika eneo hilo.

MABOMU YARIPUKA TENA TANZANIA, 20 WAFARIKI DUNIA

 

Baadhi ya wahanga wa mabomu ya Gongolamboto mjini Dar es Salaam wakiwa katika uwanja wa Uhuru wakisubiri hatma yao

Serikali ya Tanzania imesema inaendelea na uchunguzi ili kujua chanzo cha mripuko wa mabomu uliotokea katika eneo la Gon go la Mboto na kuuwa zaidi ya watu 20 huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania amesema ataunda tume maalum ya kuchunguza tukio hilo na kutoa taarifa yake.

Huku kauli hizo za kuunda tume ambayo pia imesisitizwa na na waziri mkuu Mizengo Pinda ya kuunda kwa tume hiyo na rais kuitisha baraza la usalama nchini hali ya  taharuki imetanda mji wa Dar Es Salaam, nchini Tanzania, huku wakaazi wakiamka kuomboleza vifo vya zaidi ya watu kumi na zaidi ya wengine 60 kujeruhiwa kufuatia milipuko iliyotokea kwenye ghala la kuhifadhi silaha za kijeshi, lililo karibu na uwanja wa kimataifa wa ndege.

Wakaazi wa eneo la Gongo la Mboto lililo karibu na ghala hilo wamekesha nje baada ya makaazi yao kubomoka kutokana na mtikisiko wa milipuko hiyo iliyodumu kwa saa kadhaa. Milipuko hiyo ilisikika kwa umbali wa zaidi ya kilomita ishirini kutoka kituo hicho cha kijeshi.

Inaarifiwa kuwa milipuko hiyo ilianza mwendo wa saa mbili usiku.

Msemaji mmoja wa jeshi amesema kuwa kuna watu wengi ambao wamepoteza maisha yao lakini idadi kamili haijajulikana.

Kamanda wa polisi jijini Dar-es-Salaam, Suleiman Kova, ametoa wito kwa raia wa mji kuwa huo watulivu huku maafisa wa ulinzi wakiendelea na mikakati ya kurejesha hali ya uthabiti.

Kova amesema uchunguzi wa awali umebainisha kuwa mlipuko huo ni ajali na wala sio shambulio la kigaidi.

Ni hii mara ya pili kwa milipuko kama hiyo kutoka jijini Dar es Saalam katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

mwaka wa 2009 zaidi ya watu ishirini waliuawa na wengine 300 kujerihiwa

Wapinzani wa vyama vya siasa wameitaka serikali kuwajibisha wakuu wanaohusika na masuala ya ulinzi.

Mwenyekiti wa chama cha upinzani DP amesema watanzania wanasikitika juu ya tatizo hilo na kuitaka serikali kuharakisha kutoa taarifa hiyo.

Watu wengine waliozungumzia tukio hilo wamewataka wataalamu wa jeshi kujipanga vizuri ili kuona tukio kama hilo halitokei tena.

aidha wametaka kambi za kijeshi zitanganishwa na makaazi ya wannchi ili kuepusha hali hiy.

Taarifa za hospitali ya Muhimbili zimesema hali sio mbaya na madaktari wamefanya kazi zao vizuri ili kuepusha msongomano wa wagonjwa.

Jumla ya mejeruhi 85 walipokelewa katika hospitali hiyo wakikatika viungo vya miguu, mikono na waliofariki walikuwa watano.

Jumla ya majeruhi wawili ndio walioruhusiwa kuondoka na asilimia 20 walijeruhiwa ni watoto.

Kutokana na idadi hiyo majeruhi uongozi wa hospitali ya Muhimbili uluiwaita wafanyakazi walioko mafunzoni ili kuwahudumia majeruhi hao

 

DR. SHEIN ATEUWA WAKURUGENZI WENGINE

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein jana amefanya uteuzi wa wakuu wa mbali mbali katika baadhi ya wizara za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Waliotuliwa kushika nafasi hizo katika Wizara ya Habari Utamaduni, Utalii na Michezo Mashaka Hassan Mwita ambaye atakuwa Mkurugenzi Idara ya Mipango, Sera na Utafiti.

Wengine ni Joseph John Kilangi ambaye ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji na Utumishi, huku Hamad Bakari Mshindo akiteuliwa kuwa Kamishna wa Utamaduni na Michezo.

Mkurugenzi Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Dk. Amina Ameir Issa, ambapo Yussuf Omar Chunda ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Idara ya Habari Maelezo.

Hassan Abdulla Mitawi ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Zanzibar , ambapo Rafii Haji Makame ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Sauti ya Tanzania Zanzibar, Sufiani Khamis Juma akiteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Televisheni Zanzibar .

Aidha Dk. Shein amemteua Abdulla Mohamed Juma kuwa Mhariri Mtendaji Shirika la Magazeti, ambapo Saleh Yussuf Mnemo Mkurugenzi Chuo cha Uandishi wa Habari, huku Chande Omar Omar akiteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji ya Zanzibar .

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar ni Hassan Khairalla Tawakal, ambapo Khadija Bakari Juma ameteuliwa kuwa Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili la Zanzibar .

Ali Khalil Mirza ameteuliwa kuwa Mkuu Kamisheni ya Utalii, huku Zuleikha Kombo Khamis akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Chuo cha Maendeleo ya Utalii na Ali Nassor Mohammed ameteuliwa kuwa Ofisa Mdhamini Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Pemba .

Katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Katibu wa Rais Haroub Shaib Mussa, Naibu Katibu wa Rais Maryam Haji Mrisho, ambapo Amour Hamil Bakari ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mipango Sera na Utafiti.

Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji na Utumishi aliyeteuliwa ni Makame Juma Khamis, huku Mohamed Juma Ame akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Ofisi ya Usajili na Vitambulisho.

Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni Naimu Ramadhan Pandu, Khamis Ali Khamis akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Ushirikiano wa Kimataifa na Wazanzibari Waliopo Nje.

Aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu ni Hassan Khatib Hassan, ambapo Shaaban Ramadhan Hilika kuwa Mnikulu, huku Ofisa Mdhamini Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Pemba ni Jokha Khamis Makame.

Walioteuliwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Madina Majaka Mwinyi anakuwa Mkurugenzi Idara ya Mipango Sera na Utafiti, huku Vuai Khamis Juma akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji na Utumishi ambapo Maryam Abdulla Yussuf ameteuliwa kuwa Kamishna wa Elimu.

Mkurugenzi Idara ya Elimu ya Maandalizi na Msingi aliyeteuliwa ni Uledi Juma Wadi, huku Khadija Ali Mohamed akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Idara ya Elimu ya Sekondari.

Mkurugenzi Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima aliyeteuliwa ni Fatma Mohamed Said, Hamid Rajab Juma akiteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo ya Ualimu.

Omar Said Ali ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Yahya Idris Abdulwakil anakuwa Mkaguzi Mkuu wa Elimu.

Ameir Suleiman Njeketu ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Upimaji na Tathmini katika Elimu, Bodi ya Upimaji na Tathmini katika Elimu Zanzibar.

Sichana Haji Foum ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Huduma za Maktaba, Bodi ya Huduma za Maktaba Zanzibar, Idrissa Muslim Hijja akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Mafunzo ya Amali.

Mkurugenzi Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume Abdulhamid Idrisa Haji, Suleiman Yahya Ame akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Taasisi ya Elimu ya Zanzibar na Mohammed Iddi Juma ameteuliwa kuwa Ofisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba