Dr. Ali Mohammed Shein

Mjumbe wa kamati kuu ya CCM taifa Dr. Ali Mohammed Shein amesema wanachama na viongozi wa CCM wameojitolea muhanga katika kukiimarisha chama hicho na kuwashangaa wale wanaodai kimepoteza dira

Akizungumza katika mkutano wa kilele cha kusherehekea miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM huko Muembekisonge amesema wanaotoa madai ni wale waliokihama chama hicho.

Dk. Shein amesema CCM iko imara na itaendelea kwa vile kinaongozwa na Katiba ya chama, misingi ya demokrasia na maadili ya Chama yenye kuamini umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Amesema CCM ikiwa inatimiza miaka 34 tangu kuzaliwa kwake wanaCCM wataendelea kuwa wamoja katika kukiimarisha chama chao ili kizidi kuleta ushindi na maendeleo kwa wananchi.

Dr. Shein amefahamisha CCM ndio chama kilichowakomboa wanyonge hivyo kuna kila sababu ya kuendelea kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama ili kizidi kuwa imara.

Aidha, Dk. Shein amesisitiza haja ya kuimarisha amani na utulivu ili Zanzibar izidi kuimarika na kujiletea maendeleo.

Amesema Zanzibar imejijengea sifa kubwa kitaifa na kimataifa kutokana na kuendesha uchaguzi uliokuwa huru na wa  haki na ulikuwa wa amani na utulivu.

Kwa upande wa serikali, Dk. Shein amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatekeleza Ilani ya CCM na kazi imeanza vizuri ambapo kila Wizara imekuwa ikifanya kazi vizuri licha ya kuongozwa na vyama viwili.

Wakati huo huo makamo mwenyekiti wa CCM, Zanzibar Dr. Amani Abeid Karume chama hicho kitaendeleza sera zake za kudumisha amani na utulivu kwa maslahi ya taifa na wananchi.

Dr. Karume amesema leo katika kilele cha sherehe za miaka 34 zilizofanyika Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba.

Advertisements