Rais wa Zanzibar Dr. Ali Shein akisalimiana na Balozi wa Saudia nchini Tanzania Ali Al-Jarbou Ikulu mjini Zanzibar (picha Ramadhan Othman)

SAUDI ARABIA imeeleza azma yake ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu na afya.

Balozi wa Saudia nchini Tanzania Mhe. Ali Al-Jarbou aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar .

 

Katika mazungumzo yake Balozi Jarbou alimueleza Dk. Shein kuwa Saudi Arabia inakusudia kuleta madaktari kwa muda maalum pamoja na madawa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wote ikiwa ni msaada kutoka kwa Kamisheni ya Kiislamu ya nchini humo.

 

Balozi Jarbou alisema kuwa Saudi Arabia inajivunia uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar na kusisitiza kuwa lengo na madhumuni ya msaada huo kwa Zanzibar ni kuwasaidia ndugu zao wa Zanzibar.

 

Alisema kuwa msaada huo ambao pia, unatarajiwa kutolewa kwa wananchi wote wa Tanzania bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

 

Aidha, Balozi huyo alieleza kuwa Ubalozi wake una mpango wa kuleta watalamu maalum kwa ajili ya kutoa mafunzo juu ya sekta ya elimu.

 

Pamoja na hayo, Balozi huyo ameonesha nia ya kuitangaza Zanzibar kibiashara kwa kuwakaribisha wafanyabiashara mbali mbali wa Saudi Arabia kuja kufanyabiashara Zanzibar pamoja na kuekeza vitega uchumi vyao.

 

Mbali ya wafanyabiasahara hao, Balozi huyo alieleza kuwa tayari amekuwa akitangaza Zanzibar kwa wananchi wa nchi yake ambao wamekuwa wakivutika kuja Zanzibar kwa ajili ya mapumziko ya baada ya harusi na tayari wengi wameshakuja hapa Zanzibar.

 

Balozi huyo alieleza imani yake na matarajio  kwa Zanzibar kwa kuendelea kupata maendeleo endelevu kutokana na uongozi thabiti wa Dk. Shein na kusisitiza kuwa ni kiongozi mwenye upendo na mshikamano.

 

Balozi huyo wa Saudia alimuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa wananchi wa Zanzibar amani, utulivu, upendo na mshikamano ili waendelee kujiletea maendeleo nchini mwao sanjari na kusifu ukarimu wao.

 

Pamoja na hayo, Balozi huyo alieleza kuvutiwa na maendeleo yaliofikiwa Zanzibar na kueleza kuwa anamatumaini makubwa kuwa maendeleo hayo yataimarika kutokana na uongozi wa Dk. Shein.

 

Balozi huyo pia, alitoa salamu za pongezi kwa ushindi wa Dk. Shein wa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar, salamu zilizotoka kwa mtumishi wa misikiti miwili Sheikh Abdul-Aziz.

 

Nae Dk. Shein alieleza kuridhishwa  kwake na azma ya Saudi Arabia katika kuendelea kushirikiana na Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha sekta ya afya, elimu pamoja na sekta nyenginezo.

 

Alieleza kuwa kwa upande wa sekta ya afya lengo la kuleta dawa pamoja na madaktari ni muhimu sana katika kuwasaidia wananchi katika kuimarisha huduma za afya hapa nchini.

 

Pia, Dk. Shein alisema kuwa amevutiwa na semina ya elimu  inayotarajiwa kutolewa na wataalamu kutoka nchini humo na kupongeza juhudi za nchi hiyo za kuisaidia Zanzibar katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na nafasi za masomo kwa vijana.

 

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Balozi huyo kutokana na nchi yake kuendelea kutoa nafasi za masomo na kupelekea vijana wengi kupata kusoma nchini humo na wengine bado wako nchini Saudi Arabia wakiendelea na masomo.

 

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alieleza kuwa ziara ya Dk. Jakaya Marisho Kikwete aliyoifanya nchini humo mwaka jana nayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na Saudi Arabia.

 

Akieleza juu ya salamu za pongezi alizozituma mtumishi wa misikiti miwili na Mfalme wa nchi hiyo Sheikh Abdul- Azizi kwa Dk. Shein pamoja na wananchi wa Zanzibar kwa kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu na hatimae wananchi walio wengi kumchagua Rais Dk. Ali Mohamed Shein.

 

Dk. Shein alisema kuwa ipo haja ya kuimarisha uhusiano uliopo baina ya nchi mbili hizo na kueleza umuhimu mkubwa wa mashirikiano na nchi hiyo.

 

Dk. Shein alimpongeza Balozi huyo wa Saudia na kueleza kuwa hatua ya Balozi huyo kuitangaza Zanzibar katika sekta ya utalii na uwekezaji ni muhimu sana katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar.

 

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikifanya juhudi ya kuimarisha sekta hizo za utalii na uwekezaji na kusisitiza kuwa hatua ya Balozi kuitangaza Zanzibar zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta hizo.

 

Dk. Shein alisema kuwa kwa upande wa sekta ya utalii, Zanzibar imekuwa ikiimarisha sekta ya Utalii unaozingatia silka, mila na utamaduni wa Zanzibar na ndio maana umekuwa kivutio kikubwa cha wageni

 

Advertisements