Jengo la afisi ya Manispaa Zanzibar

Mkurugenzi wa baraza la manispaa Zanzibar Rashid Alli Juma amepelekwa jijini Dar es salaam kwa matibabu zaidi baada ya kumwagiwa tindi kali na watu wasiojulikana usiku wa jana alipokuwa akitoka msikitini.

Akizungumza na ZENJ FM mstahiki Meya wa Manispaa ya Zanzibar Khatib Abdulrahman Khatib amesema mkurugenzi huyo ameumia zaidi usoni, kifuani, mikononi na mapajani.

Amesema kuwa hali yake inaendelea vizuri licha ya maumivu makali aliyoyapata kutokana na kumwagia tindi kali.

Akizungumza juu ya tukio hilo katibu msaidizi wa hospitali ya Mnazi mmoja Omar Abdalla Alli amesema mkurugenzi huyo amefikishwa hospitalini hapo majira ya saa 5.00 usiku.

Amesema daktari alimhudumia amethibitisha kwamba ameungua sehemu za usoni, kifuani na miguuni na amepelekwa katika hospitali ya Muhimbili mjini Dar es Salaam kwa matibu zaid.

Nae kamanda wa polisi mkoa wa mjini Magharibi Azizi Juma amesema tukio hilo limetokea majira ya saa 2.00 usiku wakati mkurugenzi huyo akiwa amekaa barazani baada ya kutoka msikitini kwa sala ya Isha.

Mtuhumiwa aliemwagia maji maji hayo yanayosadikiwa tindikali alifika karibu na mkurugenzi Rashid na kumwagia maji maji hayo

Hata hivyo hakuna mtu hata mmoja aliekamatwa kuhusiana na tukio hilo hadi sasa.

Hivi karibuni mkurugenzi huyo alisimamia kazi za kuondoa makontena ya biashara ya eneo la Darajani ili kupisha ujenzi wa bustani ya kupumzikia katika eneo hilo.

Advertisements